Sakata la
kutupwa kwa viungo vya binadamu bila kufuata utaratibu jana liligeuka
sinema wakati maofisa wanne wa Chuo Kikuu cha Tiba na Teknolojia (IMTU),
walipofikishwa mahakamani Dar es Salaam.
Maofisa hao ambao ni maprofesa na wahadhiri wa
chuo hicho walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni
wakikabiliwa na mashtaka mawili likiwamo la kushindwa kufukia viroba 83
vya miili ya binadamu.
Baada ya mashtaka hayo kusomwa na taratibu za
dhamana kukamilika huku mmoja wao akishindwa kutimiza masharti,
watuhumiwa hao walirejeshwa kizimbani na kufutiwa mashtaka hayo kwa amri
ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DDP) aliyewasilisha hati ya kutokuwa na nia
ya kuendelea na mashtaka hayo.
Hata hivyo, furaha waliyoipata washtakiwa hao,
Venkat Subbaiah (57), Appm Shankar Rao (64), Prabhakar Rai (69) na
Dinesh Kumar (27) ilikuwa ya muda tu, kwani polisi waliokuwapo
mahakamani hapo waliwakamata tena na kuondoka nao.
Hati ya mashtaka
Akiwasomea mashtaka, Mwendesha Mashtaka Mwandamizi
wa Polisi, Magoma Mtani alidai kuwa washtakiwa hao Julai 2014 katika
eneo la Mpigi Majohe, walishindwa kufukia viroba 83 vya miili ya
binadamu waliyoitumia kufundishia wanafunzi wa udaktari kinyume na
Kifungu cha 128 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya mwaka
2002. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Alidai kuwa washtakiwa hao kwa pamoja walishindwa kuandaa hati ya ofisa mchunguzi wa vifo vyenye mashtaka (coroner).
Baada ya kusomewa mashtaka hayo watuhumiwa wote waliyakana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Hakimu Mwandamizi wa mahakama hiyo, Kwey Rusemwa
alitoa masharti ya dhamana akiwataka kila mmoja wao kuwa na wadhamini
wawili ambao ni raia wa Tanzania na wanaofanya kazi kwenye taasisi
zinazotambulika kisheria.
Washtakiwa watatu walikamilisha masharti hayo lakini mmoja alishindwa kutokana na kuwa na mdhamini ambaye si raia wa Tanzania.
Mashtaka yafutwa
Wakati washtakiwa hao wakikamilisha taratibu za
dhamana wakiwa ndani ya mahakama hiyo, Wakili wa Serikali, Salum Ahmed
aliingia na kuiomba mahakama kuifuta kesi hiyo chini ya Kifungu cha 91
(1) cha Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA) kwa kuwa Mkurugenzi wa
Mashtaka (DPP) hana nia ya kuendeleza mashtaka dhidi yao.
Kifungu hicho cha sheria kinampa mamlaka DPP kuifuta kesi
mahakamani wakati wowote pale anapoona hana nia ya kuendeleza mashtaka
dhidi ya mtu yoyote.
Baada ya kuwasilishwa kwa ombi hilo, Hakimu Rusemwa aliwaachia huru washtakiwa hao bila masharti yoyote.
Wakamatwa tena
Muda mfupi baada ya washtakiwa hao kuwa huru,
walianza kutoka mahakamani kwa furaha lakini kumbe furaha yenyewe
ilikuwa inaishia mlangoni mwa mahakama hiyo tu kwani walikutana na
polisi waliowakamata tena na kuwaweka chini ya ulinzi.
Wakati washtakiwa hao wakiwa chini ya ulinzi,
Wakili wao, Gaudiosus Ishengoma alieleza kusikitishwa na kitendo hicho,
akidai DPP aliwafutia mashtaka wateja wake na kuwaachia huru ili
awafungulie mashtaka mengine ambayo hayana dhamana.
Baada ya washtakiwa hao kukamatwa upya walipandishwa katika gari aina ya Toyota Land Cruiser na Toyota RV4 na kurejeshwa polisi.
Akizungumzia kitendo hicho baadaye jana, DPP Eliezer Feleshi alisema kwa ufupi: “Kuna taarifa zilihitaji kufanyiwa kazi kwanza.” Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Na Mwananchi
Na Mwananchi
No comments:
Post a Comment