Afisa mkuu wa kituo cha Polisi, OCS, pia amehamishwa kituo mara moja. Hatua hii tayari imepokewa kwa hisia tofauti huku wakenya wengi wakielezea kutoridhishwa na adhabu hiyo.
Miongoni mwa walioandika malalamiko yao kwa Bwana Kimaiyo, wamesema kuwa mabadiliko yalistahili kufanyika hadi ngazi ya juu zaidi, baadhi hata wakimtaka yeye mwenyewe kama Inspekta wa polisi kujiuzulu.
Tangu kutokea shambulio la Jumapili usiku katika kijiji cha Mpeketoni, karibu na kisiwa cha Lamu pwani ya Kenya, lawama zimeelekezwa kila upande, huku baadhi wakidai kuwa wanasiasa wamehusika na wengine wakilalamikia utepetevu wa polisi katika kutekeleza majukumu yao.
Matamshi ya rais Kenyatta yame kejeliwa na wanasiasa wa upinzani nchini humo waliodai kuwa rais huyo hana ufahamu wa yale yanayoendelea nchini mwake.
Seneta kutoka chama kikuu cha upinzani, Moses Wetangula amesema matamshi ya rais sio ya kweli. '' Badala ya kuitisha usaidizi wa wenzetu wenye teknolojia bora, hata tutumie ndege zisizo na rubani kuwalipua huko waliko, tunakaa hapa Nairobi na kudai AL shabaab hawakuhusika.'' Wetangula aliambia bunge la Kenya. '' Huu ni mzaha,'' Aliongeza bwana Wetangula.
Lakini uchunguzi uliofanywa na BBC umeonesha kuwa huenda kuna uzito kwa madai ya rais Kenyatta. Wakaazi wengi wa Mpeketoni waliozungumza na BBC wametueleza kuwa, wanaamini shambulio la Jumapili usiku linatokana na mzozo wa ardhi kati ya jamii zinazoishi huko. Wakaazi hao wamesema kuwa Al shabaab wamedakia tu kujigamba kwa yaliotokea huko ila wao wanaamini kuwa ni jambo lililokuwa likitokota kwa muda mrefu.
Al shabaab wamefanya mashambulio ya mara kwa mara katika sehemu mbali mbali nchini Kenya tangu majeshi ya Kenya yaingie nchini Somalia mwaka wa 2011, katika oparesheni ya kuwafagia kutoka nchini humo. Shambulio la punde zaidi linadaiwa kufanywa kama kulipiza kisasi ya kuuawa kwa masheikh 2 wa kiislamu katika mji wa Mombasa pwani ya Kenya hivi majuzi. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
No comments:
Post a Comment