Kampuni za simu
za mkononi za Tigo, Airtel na Zantel zimeunganisha huduma zao za kutoa,
kutuma na kuweka fedha na sasa mteja anaweza kutuma fedha kutoka mtandao
mmoja kupitia mwingine.
Taarifa ya pamoja na kampuni hizo iliyotolewa
jana, ilisema kuwa wote wanaotumia huduma za kifedha za mitandao hiyo,
wataweza kutumiana fedha kupitia simu zao za mikononi pasi na tatizo
baada ya kampuni hizo kuunganisha huduma zao.
Huduma hiyo inayotarajiwa kuanza kutumika mwishoni
mwa mwezi huu, itawafanya wateja wa mitandao hiyo kutumiana na kupokea
fedha moja kwa moja kwenye akaunti zao tofauti na ilivyokuwa awali. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Taarifa hiyo ilisema ushirikiano huo unaweka
rekodi ya hatua muhimu katika ukuaji wa sekta ya mawasiliano nchini na
Afrika kwa kuwa si rahisi kwa kampuni zinazoshindana kufanya uamuzi wa
kibiashara wa aina hiyo.
“Ikumbukwe kuwa makubaliano ya namna hii hapo
awali yalifanywa na kampuni za simu kuwawezesha wateja wao kupata huduma
za kupigiana simu na kutumiana ujumbe mfupi pekee,” ilisema sehemu ya
taarifa hiyo ya pamoja na kuongeza kuwa, wateja wao watapata pia punguzo
la gharama za uhamishaji fedha, pia hawatahitajika kuwa na namba ya
siri.
Kwa sasa, ili mteja aweze kupokea fedha
alizotumiwa kutoka mtandao mwingine, anahitajika kuonyesha namba ya siri
(pin) wakati wa kutoa fedha jambo ambalo limekuwa likitatiza ufanisi wa
miamala hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Zantel, Pratap Ghose alisema
kampuni hizo zina dhamira ya dhati kuhakikisha huduma na ushirikiano huo
vinawawezesha wateja kufanya biashara zao kwa ufanisi na urahisi zaidi
nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Tigo, Diego Gutierrez alisema
anafurahi kushirikiana na washindani wake, Airtel na Zantel katika
jitihada za kuendeleza huduma za kutuma na kupokea fedha kupitia simu za
mkononi nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Airtel, Sunil Colaso alisema
kampuni yake imejikita katika kuwapa wateja wake huduma zenye ubunifu wa
hali ya juu bila kujali ushindani wa kibiashara.
Matumizi ya simu za mkononi kufanya miamala ya
kifedha yamezidi kukua kwa kasi nchini na kwa mujibu wa Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa hadi sasa
kuna watumiaji wa huduma za fedha kwa simu za mkononi 12,330,962. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Na, Mwananchi
Na, Mwananchi
No comments:
Post a Comment