Wednesday, March 12, 2014

RIDHIWANI, "SIKUSHINIKIZWA KUGOMBEA"

RidhiwaniKikwete_11ac5.jpg
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Chalinze kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ridhiwani Kikwete ameahidi kuwa atajitahidi kutatua kero za maji, umeme na ajira kwa vijana. Alisema hayo jana baada ya kuchukua fomu katika ofisi za Msimamizi wa Uchaguzi wa Wilaya ya Bagamoyo, Shija Andrew.
Leo anatarajia kurudisha fomu hiyo. Ridhiwani alipokuwa akienda kuchukua fomu hiyo, alisindikizwa na mamia ya wanachama wa CCM wa majimbo ya Chalinze na Bagamoyo, wakiwa wanaimba na kucheza kumshangilia mgombea huyo.
Baada ya kuchukua fomu kutoka kwa Ridhiwani alimhakikishia ofisa huyo kuwa atazingatia taratibu zote za uchaguzi na kutoendesha kampeni za matusi na vurugu.
Baada ya kuchukua fomu hiyo na nakala nyingine muhimu za uchaguzi, aliongozana tena na mamia ya wafuasi wake, kuelekea kwenye ofisi za CCM Wilaya ya Bagamoyo, ambapo alizungumza na waandishi wa habari.
Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like page ya facebook ya Jambo Tz
Katika mazungumzo yake hayo, Ridhiwani alitaja vipaumbele vyake kwa kuleta maendeleo kwa wakazi wa Chalinze. Alisisitiza kuimarisha upatikanaji wa maji salama na ya uhakika, kuimarisha afya, elimu na kukuza ajira kwa vijana.
"Kama mnavyofahamu kuwa Chalinze ni eneo ambalo linakabiliwa na changamoto nyingi kama vile maji, umeme na hata suala zima la ajira kwa vijana, sasa pindi nikipata Ubunge kwangu mimi nitahakikisha kuwa napunguza kama sio kumaliza kabisa tatizo hilo," alisema Ridhiwani.
Aliongeza kuwa "Mimi nimeguswa na changamoto mbalimbali zinazowakuta wakazi wa wilaya hii na kama ambavyo nilisema kuwa sikushinikizwa, ila ni kwa matakwa yangu mwenyewe, naona kabisa kuwa nipo katika hali na nguvu ya kushirikiana na wakazi hawa kumaliza shida za Chalinze".
Ridhiwani pia alisema kuwa atasaidia kutatua ugomvi wa mara kwa mara, unaowakumba wakulima na wafugaji na kuwataka wakazi wa Chalinze kumchagua.
Wakati huo huo, mgombea wa Ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Matayo Torongey alisema kuwa anavyo vipaumbele vingi na kimojawapo ni kuinua maisha ya wakazi wa Chalinze.
Alisema hayo baada ya kuchukua fomu. Kipaumbele chake kingine kutatua tatizo la ajira kwa vijana wa Chalinze na pia kupambana na umasikini.
Tongorey alisema pia kuwa atajitahidi kutatua kero za maji, barabara na umeme katika jimbo hilo. Alisema yeye analijua vema jimbo hilo na aliomba wananchi wamchague siku ya kupiga kura.
Mgombea Ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Alliance For Tanzania Farmers Party (AFP), Ramadhan Mgaya, akizungumza baada ya kuchukua fomu, alisema atajitahidi kuinua kilimo na ufugaji katika kukuza maisha ya wakazi wa Jimbo la Chalinze.
Wagombea wa AFP na Chadema walipokutana, wakati wakichukua fomu hizo, walianza kutaniana, ambapo Ramadhan Mgaya wa AFP alimwambia mgombea wa Chadema, Matayo Torongey kuwa ataongoza Ubunge huo na kisha kumwachia nafasi ya pili Matayo.
Matayo alionekana kushangaa vazi la Mgaya wa AFP, kuwa linafanana na lile la Chadema.
Alimtaka mgombea huyo wa AFP, kujiunga na Chadema ili waweze kuchukua jimbo hilo. Uchaguzi wa jimbo la Chalinze unafanyika, kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Saidi Bwanamdogo aliyefariki Januari 22 mwaka huu.
CHANZO:HABARILEO
Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like page ya facebook ya Jambo Tz

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...