Majeshi ya Umoja wa Mataifa katika
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo yameanza kutumia ndege zisizo na rubani
kuchunguza harakati za waasi katika mipaka na Rwanda na Uganda.
Hii ni mara ya kwanza kwa majeshi ya Umoja wa Mataifa kutumia ndege za aina hiyo.
Ndege
mbili za kwanza zilirushwa kutoka mji wa mashariki wa Goma ambao mwaka
jana ulikaliwa kwa muda mfupi na waaasi wa kundi la M23.
Ndege mbili za kwanza zinaundwa na shirika la Italia la Selex ES.
Jeshi la Umoja wa mataifa katika
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ndio kubwa kupita yote duniani na
lilichangia kwa kiasi kikubwa mwezi uliopita ushindi dhidi ya waasi wa
kundi la M23;lakini bado kuna makundi mengine kadhaa ya wanamgambo
nchini humo.
Kikosi kipya kilichoimarishwa nguvu
cha Umoja wa Mataifa kilitumia ndege za helikopta kulisaidia jeshi la
Congo dhidi ya waasi hao wa M23.
Eneo tajiri la madini la mashariki mwa
Congo limekumbwa na vita kwa kipindi cha miongo miwili iliyopita lakini
kushindwa kwa M23 kumeleta matumaini fulani ya kupatikana utulivu zaidi
kwa eneo hilo.
Mwandishi wa BBC, mashariki mwa Congo
Maud Jullien amesema kwa muda mrefu kumekuwa na tuhuma kwamba vikundi
mbalimbali vyenye silaha katika jimbo la Kivu Kaskazini wakipata msaada
kutoka nchi jirani.
Rwanda na Uganda mara kwa mara
zimekanusha tuhuma za kuwasaidia waasi wa M23, kikundi ambacho hivi
karibuni kilipigwa na majeshi ya Congo yakisaidiwa na vikosi vya Umoja
wa Mataifa vinavyolinda amani nchini Congo.
Askari wapatao 22,000 wapo nchini
Congo, kikiwa ni kikosi kikubwa zaidi cha Umoja wa Mataifa katika
shughuli za kulinda amani duniani.
Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa kuhusu masuala ya kulinda amani Herve Ladsous ameiambia BBC kuwa
ndege hizo zisizo na rubani, zitatumika kama njia mojawapo ya
kufuatilia harakati za makundi yenye silaha na mienendo ya raia katika
eneo la mashariki mwa Congo.
"Tunatakiwa kuwa na picha halisi ya kile kinachotokea," amesema.
Amesema kama watafanikiwa nchini DR
Congo, ndege hizo zinaweza pia kutumika katika maeneo mengine ya kulinda
amani ya Umoja wa Mataifa.
No comments:
Post a Comment