Mwenyekiti wa tume ya mabadiliko ya katiba, Jaji Warioba. Picha na Maktaba
*********
Dar
es Salaam.Hatimaye Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Mwenyekiti
wake, Jaji Joseph Warioba imekamilisha kazi ya kuboresha rasimu ya
kwanza na kupata rasimu ya pili ya Katiba Mpya tayari kwa hatua
nyingine.
Taarifa zilizotufikia jana
zilieleza kuwa Makamishna na Wajumbe wa Sekretarieti wa tume hiyo,
walianza kurejea ofisini juzi na jana, wakitokea Hoteli ya White Sands
walikojichimbia tangu Desemba Mosi mwaka huu kukamilisha rasimu hiyo.
Awali, Rais Jakaya Kikwete aliiongezea tume hiyo siku 14 zaidi
kukamilisha kazi zake. Siku hizo zitakamilika siku 11 kuanzia leo.
Jaji Warioba, Makamu wake Jaji
Augustino Ramadhan na Katibu wa Tume hiyo, Assaa Rashid hawakupatikana
kutokana na kilichoelezwa kuwa walikuwa kwenye kikao. Gazeti hili
lililazimika kumtafuta Naibu Katibu, Casmil Kyuki ambaye naye
alithibitisha taarifa hizo.
“Ni kweli sisi (Wajumbe wa
Sekretarieti) tumerejea ofsini jana na wenzetu (Makamishna) walirejea
tangu juzi. Kazi zetu tumezikamilisha kilichobaki tunafanya mawasiliano
na Mkuu (Rais Jakaya Kikwete), tujue lini tutawasilisha kazi hii,”
alieleza Kyuki
Hata hivyo, kiongozi huyo
aligoma kutoa taarifa zaidi akisema maelezo kamili yatatolewa kwenye
mkutano utakaohusisha tume na vyombo vya habari wakati wowote kuanzia
kesho.
Akizungumzia uamuzi uliyofikiwa
na Bunge, unaotaka tume hiyo ivunjwe mara baada ya kukabidhi rasimu hiyo
kwa Bunge Maalumu la Katiba, Kyuki alisema wao wanaafikiana na uamuzi
huo.
“Kila
kitu maishani kina uzuri na ubaya wake, hata kama tungetakiwa kuwamo
tungewasaidia wakiwa ndani ya kamati, lakini wangeweza kufanya tofauti
wakiwa kwenye mijadala bungeni kwa hiyo bado kuwepo kwetu kusingesaidia
kitu,” alisema Kyuki ambaye pia ni Mwandishi Mkuu wa Sheria Tanzania.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment