Kocha mpya wa Azam FC Joseph Omog akiwa na Mwenyekiti wa timu hiyo Ndugu Said Mohammed.
Omog na Mwandishi wa habari za michezo,Mwani Nyangasa.
Kocha Omog akikabidhiwa jezi ya Azam FC.
Klabu ya Azam inapenda kuufahamisha umma hususan wapenzi wa mpira wa miguu kuwa imeingia mkataba na kocha Joseph Marius Omog raia wa Cameroon kwa kipindi cha ...
miaka miwili (2) kuanzia leo.
Kocha Omog ni bingwa kwani anakuja kuifundisha Azam akiwa ametoka kuiongoza klabu ya A.C Leopards ya Jamhuri ya Kongo (Brazaville) kutwaa ubingwa wa ligi ya nchi hiyo kwa misimu miwili mfululizo (2012 na 2013).
Timu hii ilikuwa haijatwaa ubingwa wa ligi kwa zaidi ya miaka 30. Kwa mwaka huu wametwaa ubingwa wakiwaacha wapinzani wao, Diables Noirs kwa pengo la pointi kumi (10) wakikusanya pointi 87 katika ligi yenye timu 18.
Pia ni mwaka jana tu (2012) aliiwezesha A.C Leopards kunyakua ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Afrika kwa kuzipiga kumbo timu ngumu na zenye uzoefu mkubwa kama vile Mas de Fes ya Morocco, Heartlands ya Nigeria na Sfaxien ya Tunisia.
Mafanikio hayo ya kutwaa ubingwa wa Afrika yalifikiwa baada ya miaka 38 tangu klabu ya Jamhuri yas Kongo ifanye hivyo, na kumfanya kocha Omog kuwa moja ya makocha wa kupigiwa mfano barani Afrika.
Kadhalika mwaka huu 2013, A.C Leopards chini ya ukufunzi wa Omog ilitinga hatua ya makundi ya Ligi ya mabnigwa Afrika na kupangwa katika kundi moja na timu mbili zilizocheza fainali; Al Ahly ya Misiri (bingwa) na Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Yote hayo ameyafanya akitumia asilimia kubwa ya wachezaji wa ndani ya Kongo huku akiwainua kutoka katika hali ya kuonekana wachezaji wa wastani hadi kuwa tishio na kuhofiwa kote barani Afrika.
Azam Football Club inamuona kocha Omog kuwa anakidhi vigezo vya kuendana na dira ya klabu ambayo ni kukuza na kuwaendeleza wachezaji na kushindana kwa kiwango cha juu kwa lengo la kuwa mabingwa katika mashindano mabalimbali ambayo timu inashiriki.
Uongozi wa Azam FC utampatia ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha malengo na mipango thabiti ya klabu.
Maelezo Binafsi
Kocha Omog ni mchezaji wa zamani wa timu ya Dragon Yaounde Cameroon. Alipata mafunzo ya ualimu wa michezo na elimu ya viungo (Sports and physical education) kutoka chuo cha vijana na michezo (Higher Institute of Youth and Sports, INJS Yaounde).
Baadaye alipata fursa ya kujiendeleza nchini Ujerumani ambako mwaka 1987 alitunukiwa stashahada ya ukufunzi wa mpira wa miguu na leseni B ya ukocha kwa viwango vya Shirikisho la mpira wa miguu barani Ulaya, UEFA.
Aliporejea nyumbani kwao Cameroon Joseph Marius Omog, alifundisha kabumbu katika klabu mbalimbali, zikiwemo; Fovu of Baham na Aigle of Menoua na kufanikiwa kufuzu kwa fainali za kombe la Cameroon. Mwaka 2001 aliteuliwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Cameroon, Indomitable Lions chini ya kocha raia wa Ujerumani Winfried Schafer.
Omog amewahi pia kufundisha timu ya taifa ya Cameroon iliyoundwa na wachezaji wa ndani ijulikanayo kama Intermediate Lions hadi mwaka 2010 na baada ya hapo akelekea Kongo kuionoa A.C Leopards kwa mafanikio makubwa na hasa kutwaa ubingwa wa kombe la Shirikisho wakiifunga Djoliba ya Mali kwa ushindi wa jumla wa magoli 4-3 katika michezo miwili ya fainali.
Uongozi,
No comments:
Post a Comment