********
Baada ya kizaazaa cha wiki iliyopita ambapo mawaziri wanne
walipoteza kazi zao kutokana na kuwajibishwa kwa vitendo vya ukatili na
mauaji vilivyotokea wakati watendaji katika wizara zao walipokuwa
wakiendesha ‘Operesheni Tokomeza Ujangili’ nchi nzima, kinachosubiriwa
na wananchi hivi sasa ni Rais Jakaya Kikwete kuunda Baraza jipya la
Mawaziri.
Kutokana na udhaifu mkubwa katika utendaji ambao
kwa muda mrefu umeonyeshwa na mawaziri wengi katika Baraza la Mawaziri,
hatudhani kama kuna mwananchi hata mmoja anayemtarajia Rais Kikwete
kujaza tu nafasi za mawaziri aliowafukuza wiki iliyopita.
Nderemo na vifijo vilivyotokana na furaha ya
wananchi katika kila kona ya nchi baada ya mawaziri hao kuondolewa
katika nyadhifa zao ni ishara tosha kwamba hawamtarajii Rais Kikwete
kuishia hapo, isipokuwa kuwaondoa mawaziri wengine wengi ambao tayari
wamethibitika na hata kutajwa na chama chao cha CCM kuwa ni ‘mawaziri
mizigo’.
Hii bila shaka ni fursa nzuri kwa Rais Kikwete
kusoma alama za nyakati, kwamba wananchi wamefika kikomo cha uvumilivu
na sasa wamechoka na uzembe unaotokana na mawaziri dhaifu walio katika
Baraza lake la Mawaziri. Hao ni mawaziri ambao karibu muda wote
wamekuwa nyuma ya matukio na kuishia kuwa watazamaji, huku shughuli za
Serikali zikienda ndivyo sivyo kutokana na kutochukua hatua stahiki
dhidi ya vitendo vya rushwa, uzembe, ubadhirifu wa fedha za umma na
ufisadi uliokithiri.
Kutokana na mawaziri wengi kutokuwa na dhamira
wala uwezo wa kuthubutu na kutenda, programu za Serikali kama ‘Kilimo
Kwanza’ na ‘Matokeo Makubwa Sasa’ zimebakia kuwa vichekesho vya karne,
pamoja na kuanzishwa kwa mbwembwe na fedha nyingi za walipakodi.
Ni bahati mbaya kwamba Rais Kikwete amebaki na
muda mfupi mno kabla ya kumaliza kipindi chake cha uongozi Oktoba 2015.
Kwa kifupi, amebakiwa na miezi 22. Kutokana na kuwapo programu nyingi
ambazo hazijatekelezwa, anahitaji sasa kujipanga upya na kupata Baraza
jipya la Mawaziri lenye watendaji waadilifu na wachapakazi.
Baadhi ya
wananchi wamekuwa wakielekeza lawama nyingi kwake kwamba uteuzi wake wa
mawaziri kwa kiasi kikubwa umekuwa siyo wa umakini kwa maelezo kuwa,
hauzingatii vigezo vya ufanisi na utumishi wa umma uliotukuka. Kwamba
wengi wamekuwa ni mawaziri wa kufunga tai na kupeperusha bendera kwenye
‘mashangingi’ yao.
Tunakubaliana na wanaosema kwamba mawaziri
wachapakazi katika Baraza lake wanahesabika katika kiganja cha mkono na
kwamba Baraza hilo ni kubwa mno kupita kiasi. Jambo la kusikitisha ni
kwamba ni mawaziri wasiozidi saba wanaoweza kusimama leo na kuonyesha
kitu walichokifanya na kukisimamia mpaka mwisho. Rais Kikwete atafanya
vyema iwapo ataweka mfumo wa kupima utendaji wa mawaziri wake na
kuwawajibisha wale wasiofikia viwango, badala ya kusubiri shinikizo la
Bunge kama tulivyoshuhudia mwishoni mwa wiki.
Tunamshauri Rais Kikwete sasa aepuke kigezo cha
ukanda na ukabila katika kuteua Baraza la Mawaziri. Hoja yetu ni kwamba
siyo lazima kila kanda au mkoa kuwakilishwa na idadi sawa ya mawaziri
hata kama baadhi yao hawana uwezo hata kidogo. Tunasema vigezo vikubwa
katika uteuzi huo viwe ni uzalendo, uadilifu na utendaji, hata kama
vigezo hivyo vitalazimu kuteuliwa mawaziri wawili kutoka katika
kitongoji, kijiji au kata moja.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment