Tuesday, November 19, 2013

WACHUNGAJI WAMKALIA KOONI MZEE WA UPAKO KUHUSU RAMBI RAMBI YA MAREHEMU MOSES KULOLA

WACHUNGAJI wa makanisa mbalimbali nchini wamemkalia kooni Mchungaji wa Kanisa la Maombezi, Antony Lusekelo maarufu kama Mzee wa Upako, kwa kumtaka atoe rambirambi aliyoahidi mbele ya umati wa watu siku ya kuaga mwili wa marehemu Askofu Moses Kulola Temeke, jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mtu wa kamati iliyoratibu mazishi ya kiongozi huyo wa kanisa, viongozi wote wa dini walioahidi kutoa rambirambi hizo wametoa isipokuwa Lusekelo aliyeahidi kwa mbwembwe kutoa shilingi milioni 15.
Katibu Mkuu wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania, Mchungaji David Mwasota alisema anamheshimu Lusekelo kwani ni mtumishi wa Mungu, lakini ni bora angetimiza ahadi yake kama walivyofanya wenzake.

“Mzee wa Upako ni mtu mwenye jina kubwa kwenye jamii na kwa Mungu, hivyo anapaswa kuangalia kwa undani kile anachoahidi kwa muda unaotakiwa na amuache mke wa marehemu apumzike kwa kuwa ametokwa na mpendwa wake na bado hana nguvu,” alisema na kuongeza;


“Haijawahi kutokea popote, mke wa marehemu akaanza kuzunguka mikoani kukusanya rambirambi kwa walioahidi, huko ni kumsumbua, yeye atumie hekima kuipeleka rambirambi hiyo kwa mke wa marehemu,” alisema Mwasota.
Kwa upande wake, Mchungaji Josephat Gwajima ambaye ni mmoja kati ya walioahidi na kutoa, alisema alitekeleza ahadi yake ndani ya muda mfupi, kama alivyoahidi.

“Namshukuru Mungu kwani nimeweza kutimiza niliyoyatamka mbele ya watu siku ile ya kuaga, najua nisingetoa ingenichafua pia ningeweza kuwadhalilisha wachungaji wenzangu, nikiwa kiongozi lazima niwe mfano bora na nionyeshe njia na uaminifu mbele ya jamii,” alisema Gwajima aliyeahidi na kutoa kiasi cha shilingi milioni 10.
 
Alimtaka Mzee wa Upako kutimiza ahadi yake ili kuondoa minong’ono isiyo na tija mbele ya jamii.

Naye Mchungaji Getrude Rwakatare alisema yeye alitoa kiasi cha shilingi milioni moja aliyoahidi siku ile ya kuaga.
“Nisingependa kuzungumzia juu ya Mzee wa Upako, ila kinachotakiwa ni kutoa kile anachokiahidi, hivyo wote walioahidi watekeleze ahadi zao,” alisema.

Naye Makamu wa Askofu Mkuu wa Kanisa la TAG, Askofu Magnus Mhiche amesema hafurahishwi na malumbano juu ya rambirambi na alishauriwa kusiwepo mabishano kwa kitu kilichotamkwa wazi mbele ya jamii.
Na mke wa marehemu, Elizabeth Kulola alisema kwa sasa amekuwa mzee asiyeweza kutembea kutoka  Mwanza kwenda Dar kufuata rambirambi kwa Mzee wa Upako ama tu yeyote.

“Licha ya uzee lakini ni aibu kuanza kutembelea mikoa mbalimbali kukusanya rambirambi kwani walioahidi ni wengi na kutoa ni moyo na wala siyo deni,” alisema na kuongeza:

“Namuomba Mzee wa Upako awatume viongozi wa kanisa lake waniletee au atume mtu yeyote anayemwamini au nimpe namba ya akaunti yangu azitumbukize humo, sijapata taarifa yoyote toka kwake kunihitaji niende kwake na hata ningepata isingewezekana kutokana na uzee.”

Awali Mzee wa Upako alimtaka mama huyo kufuatilia rambirambi ofisini kwake Ubungo Kibangu jijini Dar na wala asimtume mtu yeyote hata kama ni mtoto wake.

Hata hivyo, kiongozi huyo wa kanisa mwenye wafuasi wengi, katika hali ya kushangaza, alikataa kutimiza ahadi yake kwa maelezo kuwa baadhi ya viongozi wa dini wamemdhalilisha, licha ya kushindwa kuainisha.
Stori: Global Publishers

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...