Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema waliofurahi na kuhuzunika naye pia watashinda pamoja naye.
Bila kufafanua kauli yake jana, Lowassa aliwaambia wakazi wa Monduli mkoani Arusha kuwa: "Kumbukeni kaulimbiu yangu wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita, tulifurahi pamoja, tulihuzunika pamoja na tutashinda pamoja".
Mbunge
huyo wa Monduli alikuwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara mara baada
ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa wodi mbili za ghorofa za wazazi
katika Hospitali ya Wilaya ya Monduli.
Katika
hotuba yake fupi, pia alitamba kwamba atayashinda majaribu. Hata hivyo,
hakufafanua majaribu hayo... "Kuna vita kubwa, lakini ambacho naweza
kusema ni kuwa nayaweza yote kwa yeye anitiaye nguvu."
Kuhusu
afya yake ambayo mara kadhaa imeelezwa kuwa siyo imara, kiongozi huyo
alisema kwa sasa ni nzuri na imeimarika kupita kipindi kingine chochote.
Lowassa
alisema kuanza ujenzi wa majengo hayo ambayo ni utekelezaji wa ahadi
zake, ni moja ya ushindi na kuwataka wakazi wa Monduli, kumshukuru Mungu
kwa yanayotokea.
Mwenyekiti
wa CCM wa Mkoa wa Arusha, Onesmo Nangole aliwataka wakazi wa Monduli,
kumshukuru Mungu kwa kuwa na mbunge Lowassa ambaye anapendwa nchi nzima.
"Monduli
Mungu awape nini, Lowassa anaitwa kila mahala kusaidia kutokana na moyo
wake wa huruma na hapa ametekeleza ilani yote ya uchaguzi," alisema.
Kauli ya
Lowassa imekuja siku chache tangu mtangulizi wake katika nafasi ya
Waziri Mkuu, Frederick Sumaye alipomtuhumu hadharani kwamba amekuwa
akimhujumu na kumwekea vikwazo vya kisiasa kwa kutumia mbinu chafu.
Miongoni mwa mambo yaliyoonekana kumkera Sumaye ni habari iliyoandikwa
na gazeti hili Septemba 16, mwaka huu inayohusu mradi wa maji Ziwa
Victoria, ambayo Lowassa alinukuliwa akisema kuwa wakati akiwa Waziri wa
Maji, aliungwa mkono na mawaziri watatu tu alipopendekeza mradi huo wa
maji.
Sumaye
alisema: "Najua mhusika ametumia sana mradi huu kisiasa na sisi wengine
tumenyamaza japo ukweli tunaujua. Amenilazimisha niseme ukweli kuhusu
mradi huu kwa sababu mimi nilikuwa Waziri Mkuu na mradi umetekelezwa
chini ya uangalizi wangu," alisema na kuongeza:
"Kama
waziri anaweza kubuni na kutekeleza mradi mkubwa hivyo peke yake, sasa
akiwa Waziri Mkuu si maji yangefika Dodoma? Mbona hata bado kuna sehemu
za Kanda ya Ziwa bado kuna shida ya maji?"
Tangu
Sumaye atoe tuhuma hizo ambazo zinahusishwa na vita ya kuwania urais wa
2015, Lowassa hakuwahi kujibu chochote wala kusikika akizungumza
hadharani, hadi jana.Lowassa alisema mafanikio yaliyopatikana katika
jimbo lake na mengine nchini, yanatokana na utekelezaji wa Ilani ya
Uchaguzi ya CCM, ambao umefanywa na Rais Jakaya Kikwete.
"Hakuna
kipindi ambacho ilani ya uchaguzi imetekelezwa kwa kiasi kikubwa kama
kipindi cha Rais Kikwete naomba sote tumpongeze," alisema Lowassa.
Alisema
hivi karibuni amekutana na Rais Kikwete ambaye ametoa Sh3 bilioni za
ujenzi wa mabwawa 10 katika wilaya hiyo ili kukabiliana na tatizo la
maji.
Wodi hizo
za kisasa zinajengwa na Kampuni za Meelo Constraction na Bulem
Constraction za Arusha kwa gharama ya Sh1.9 bilioni na zitakuwa na uwezo
wa kulaza wagonjwa 140 wakati mmoja.
No comments:
Post a Comment