Monday, October 14, 2013

HAYA NI MAMBO 11 YALIYOPINGWA NA BABA WA TAIFA, MWALIMU NYERERE

 Ni miaka kumi na nne sasa imepita tangu mzee wetu mpendwa baba wa taifa hayati Mwl Julius Kambarage Nyerere aiage dunia.
Mwalimu Nyerere ni Rais wa kwanza na ni muasisi aliyeliletea taifa hili uhuru wa kweli toka katika makucha ya mkoloni 9 December, 1961. Mwalimu Nyerere alizaliwa April 22, 1922 katika kijiji kidogo cha mwitongo huko Butihama, kasikazini mwa Tanzania karibu kabisa na ziwa Victoria . 
Alikuwa ni mototo wa chifu Burito Nyerere wa kabila dogo la wazanaki
Nyerere alifariki dunia kwa ugonjwa wa kansa ya damu, siku ya Alhamisi Oktoba 14, 1999 saa 4:30 asubuhi [kwa saa za Afrika Mashariki], katika hospitali ya Mtakatifu Thomas London, Uingereza akiwa amezungukwa na timu ya madaktari bingwa.
Ndipo wananchi wote tulipigwa na butwaa kwa kumpoteza kiongozi mwenye msimamo thabiti na busara duniani. 
Mwalimu bado ni taa inayong’aa gizani, umuhimu wake nazidi kuonekana kadiri miaka inavyokwenda licha ya kwanza amekwisha tuacha.
Wakati wa uhai wake Mwalimu Nyerere alichukia na kukemea vikali mambo yasiyofaa kwa mustakabali wa maendeleo ya Tanzania , Afrika na Dunia kwa ujumla. Baadhi ya mambo hayo ni:

1. UJINGA 

Mwalimu Nyerere alikuwa ni miongoni mwa wasomi wachache na ni mtanzania wa kwanza kupata nafasi yamasomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Edinburg , Uingereza na kuhitimu mwaka 1952 akiwa ni gwiji wa uchumi na historia.
Mwalimu hakupenda ujinga na hivyo alipigana vita kali dhidi ya ujinga, na alifanikiwa kwa nafasi yake kuwaondoa ujinga watanzania wengi, wakiwemo viongozi wetu wa sasa ambao walisomeshwa ‘bure’ katika mazingira mazuri yakuridhisha kwa manufaa ya nchi yetu. Ndiyo maana Rais Kikwete Februari 3, 2007 alisema “….sisi tuliwekezwa na ni lazima tuwekeze kwenu ili miaka 30 ijayo Rais atoke miongoni mwenu….”

Kama Nyerere asingechukia ujinga kwa kuboresha mazingira ya elimu, ikiwemo elimu ya watu wazima, basi leo hii tungekuwa na vingozi ‘zezeta’.
Vita ya ujinga sasa si yakuridhisha. Zaidi ya asilimia
28.6 ya watanzania hasa waishio vijijini hawajui kusoma na kuandika, pamoja na kutoa elimu ya msingi bure na kupunguzwa ada ya sekondari na kuongeza idadi ya madarasa, bado shule hizi zinakosa waalimu na vifaa vya kutosha. 
Pia idadi kubwa ya watanzania pamoja na kufaulu hawapati nafasi ya elimu ya juu kutokana na sera chakavu na mifumo kndamizi iliyopo nchini, kama ya kuangalia madaraja [Division] katika utoaji wa mikopo na asilimia za uchangiaji gharama za elimu ya juu.
Kuna usemi usemao “If education is Expensive try ignorance as your option” [kama elimu ni ghali, jaribu ujinga]. Serikali yetu ni wazi kabisa kuwa inaona elimu ni gharama, hivyo imeamua kujaribu ‘ujinga’ kwa kile inachokiita ‘kuchangia elimu ya juu’ eti serikali haina uwezo.
Huku ndiko kuzienzi kuzienzi fikra za Mwalimu Nyerere?


2. UBINAFSI NA UFISADI

Katika mambo aliyoyaamini sana na kuyapa mkazo wa aina yake, ni pamoja na masuala ya haki na usawa. Mwalimu siku zote, alijenga imani katika misngi ya utu, haki na usawa kwa kila raia wa dunia hii. Aidha Mwalimu alipinga sana mianya ya unyonyaji aliyoiita ‘mirija’. Mwalimu alipinga sera zozote zinazweza kuleta matabaka katika Taifa, iwe ni matabaka ya kiuchumi kwa kuwa na kundi la walionacho na wasionacho. 
Mwalimu hakuruhusu ubinafsi na ufisadi ambao ambao leo hii umekithiri miongoni mwa viongozi wengi hapa nchini. 
Mwalimu aliwahi kusema “Hakuna mtu yeyote katika jamii atakayekuwa na mahitaji yote muhimu wakati wengine katika jamii hiyohiyo hawana chochote”.
Mwalimu alijikita katika siasa ya ‘ujamaa’ na kujitegemea na hatimaye Azimio la Arusha mwaka 1967, ili kahakisha keti ya Taifa [National cake] inakuwa na mgawanyo sawa kwa wote.Leo hii Azimio la Arusha limesahauika kabisa, hali ya viongozi wa serikali wanatanguza mbele maslahi binafsi hali ambayo baba wa Taifa aliipinga tabia hiyo chafu inayozidi kuchukua sura mpya kila kukicha.
Mwaka 1978 nchi yetu ilikuwa katika wakati mgumu wa vita dhidi ya Nduli Iddiamin Dada, lakini wabunge walihitaji nyongeza ya mishahara na kupunguzwa posho ya waanafunzi wa elimu ya juu. Hali hii ilipelekea wanafunzi wa enzi hiyo wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam kugoma na kupinga ubinafsi wa waung hao. Hapa tuliona msimamo, uzalendo na busara za Mwalimu aliyetoa kauli kali ya kuamuru mishahara ya wabunge ipunguzwe na posho za vijana zibaki kama awali.
Nyerere asingekuwa mzalendo wa kwelil basi leo hii familia yake wangekuwa ndio mabilionea wan chi hii.


3. UBEPARI

Mwalimu alikuwa ni nuru ing’aayo gizani, alipinga mfumo wa ubepari kwa kuuita ‘mfumo wa ufukarishaji’. Hivyo aliimarisha misingi imara katika itikadi yake ya ujamaa na kujitegemea, ikiwa ndiyo itikadi pekee yenye misingi ya utu, haki na usawa.
Mwalimu alichukizwa sana na mfumo mpya wa kibepari uliozuka baada ya yeye kung’atuka madarakani aliouita ‘ubepari wa pembezoni’ yaani ni ubepari wa kishenzi unaotoa mianya kwa wachache kutumia mirija kuwanyonya wanyonge. 
Tanzania yetu leo hii, bila hata aibu katiba ya Jamhuri ya Muungano katika ibara yake ya 3 inasema, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.
 Hili linaleta utata na mkangnyiko kwani kimaandishi ni wajamaa lakini matendo yaliyopo ni zaidi ya ubepari.
Unaweza kuangalia uuzwaji holela wa nyumba za serikali zilizojengwa kwa jasho la Mzee Nyerere na akina Rashid Kawawa, pamoja na mikataba mibovu inayotanguliza maslahi ya wachache.Mwalimu hakusita kukemea mambo ya kihuni kama haya. 
Katika kitabu chake Ungozi wetu na hatima ya Tanzania ukurasa wa 28 Mwalimu alisema “Halimashauri kuu ya Taifa iliketi unguja, ikabadili Azimio la Arusha bila kwanza kutafuta maoni ya wananchi, na walikuwa na haki ya kufanya hivyo maana sera ni yao.Ubaya wao ni kwamba, jambo lenyewe walilifanya kwa hila na janjajanja na mpaka sasa wanaendelea kuwadanganya wananchi kwamba sera ya CCM ni ya ujamaa na Kujitegemea.”


4. UKABILA NA USEHEMU
Wakati Mwalimu Nyerere alipokuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam , alifanikiwa kuwaunganisha wanafunzi katika jumuiya moja iitwayo USARF ikijumuisha wanafunzi kutoka nchi zote za Afrika. Aliona kuwa ni vema kwani Afrrika ni moja. Leo hii wanafunzi wetu wanajitambulisha na kujitanabaisha kwa makabila na sehemu watokazo. 
USARF imekufa kabisa na imebezwa na vijikundi vya makabila yao . 
Hali hii ya ukabila na usehemu inatawala kona zote za nchi yetu na ndiyo maana watu wengi wakienda kuomba kazi au hata huduma katika sehemu fulani, utasikia anaulizwa ‘wewe ni kabila gani au unatoka mkoa gani?’Hapa tulipofikia nchi yetu imepotea kisiasa, kijamii na hata kiuchumi.
Naamini Roho ya Mwalimu Nyerere inahuzuika sana kuona wanafunzi wanavyomkumbuka wakidai haki zao hasa katika vipindi vya migomo, wakati hili ambalo aliasisi hawalienzi.


5. UBINAFSISHAJI HOLELA WA MALI ZA UMMA

Wakati wa uhai wake Mwalimu alilaani vikali ubinafsishaji holela wa masirika ya umma. Alwakataa Mabeberu waliojiita ‘wawekezaji’ walionuiya kufirisi utajiri wan chi yetu huku wakishibisha matumbo yao .
Leo hii vigogo wa serikali wanajichukulia majumba ya serikali bila kujali wao kutoka madarakani watumishi wa umma hapo baadaye wataishi wapi.
Huku ndiko kumuenzi Mwalimu, aliyekataa kuishi kwenye nyumba kubwa kule Butihama, akisema yeye sio tembo? Uko wapi uzalendo aliotuachia Mzee Nyerere?


6. KUONGOZWA KWA RIMOTI NA NCHI MATAJIRI

Nakumbuka siku moja Mwalimu Nyerere akiwa katika viwanja vya mnazi mmoja [Dar es salaam] aliwahi kusema “Tangu lini IMF ikawa International Ministry of Finance?” [Wizara ya fedha ya kimataifa].
Leo hii viwanja hivyohivyo vinatumika kuusifu ubeberu wa IMF na wawekezaji wake, huku tukiwekewa masharti magumu ya kuongoza nchi yetu kwa maslahi ya mabeberu.
Mwalimu aliwaonya mataifa tajiri wasiingilie mambo yetu ya ndani, pale walipoona maslahi yao hayazingatiwi, mara kwa mara walimuhoji Mwalimu ambapo yeye aliwaamuru waondoke haraka na misaada yao yote. 
Mwalimu hakupenda misaada ya kinafiki iliyolenga kuwaangamiza wananchi wake, alipinga amri na maagizo ya taasisi za fedha kama Benki ya Dunia [WB] na IMF [International Monetary Fund].Hivyo aliheshimu maamuzi yake sahihi katika kulinda heshima ya nchi yetu na watu wake.
Kipindi chote cha uhai wake Mwalimu alisisitiza haja ya mataifa ya Afrika kujitawala na kuwa huru katika kujiamulia mambo yake. “Inapotokea taifa kuuza uhuru wake kwa ajili ya misaada ya kiuchumi au kukubali kukaliwa na majeshi ya nje, taifa hilo linakuwa limepotea na litanyonywa na watu wake watakuwa wanakandimizwa popote pale” alisema Mwalimu.
Kama tungekuwa na misimamo kama Nyerere, tungeheshimika. Lakini leo hii Mwalimu angefufuka angefadhaika sana kuona jinsi tunavyomuenzi.


7. UBABE NA VITISHO KATIKA UONGOZI

Mwalimu aliamini kuwa kiongozi bora hapaswi kuwa na jazba na asiyetumia ubabe wala vitisho katika maamuzi au katika kutatua tatizo ambalo jamii inataka litatuliwe kwa maslahi na manufaa ya Taifa. Aliamini kuwa kiongozi bora ni yule anayeruhusu mianya ya majadiliano baina yake na wale anaowaongoza. Asiyetumia lugha chafu au kashfa na kejeli kwa watu wake.
Leo hii tawala mbalimbali zikiwemo taasisi za elimu ya juu na hata chombo cha juu kabisa cha maamuzi [Bunge] vinatumia ubabe na vitisho katika maamuzi.
Tunashuhudia migomo ya vyuo vikuu kila kukicha huku maamuzi ya ‘kibabe’ yakitumika na watawala wa vyuo katika kukandamiza haki za wanafunzi. 
Masikini wanafunzi hawa wanabaki wanalia huku wakiimba “… kama siyo juhudi zako Nyerere na ...angesoma wapi…”
Tunaona pia Bunge linavyopitisha maamuzi yasiyo na maslahi kwa wananchi ‘kibabe’ na hata kuadhibu wale wanaojaribu kutetea maslahi ya wanyonge. Bunge hilohilo linatumia pia lugha za kejeli na dharau kuwatisha wananchi, ubabe na vitisho si misingi ya demokrasia na utawala bora.


8. UMANGIMEZA NA UKIRITIMBA

Wakati wa uhai wake Mwalimu aliheshimu mipaka, taasisi za utawala na mali za umma. Alichukia matumizi mabaya ya rasilimali za umma, pia aliheshimu mawazo yake mwenyewe na ya wenzake.
Mwalimu aliamini kwamba, kiongozi asiyepeda ukiritimba na umangimeza ni lazima awe mfuasi mzuri wa maadili anayoyasimamia, mwaminifu na mwadilifu kwa manufaa ya Taifa lake. Mwalimu hakupenda kutetea uovu wa viogozi eti kwa kutunza heshima zao au kulinda vyama vyao bila kujali uhusiano wao wala majina yao . Hivyo katika serikali yake Mwalimu hakuawa na ubia na mtu yeyote duniani.
Leo hii ni viongozi wangapi wanadumisha fikra na misimamo ya Mwalimu kwa vitendo?


9. USIRI WA MIKATABA NA MAKAMPUNI YA KIGENI

Mwalimu alisisitiza uwazi katika mikataba mbalimbali ambayo serikali iliingia na makampuni ya kigeni.
Katika kitabu chake cha Uhuru na Maendeleo Mwalimu anasema “Viongozi wa kiserikali wana wajibu mkubwa wa kuwafahamisha wananchi nini serikali inafanya na kwa sababu gain”
Tofauti kabisa hali ilivyo sasa, hali inayopelekea minung’uniko na malumbano yanayo husisha hata ugawaji wa tenda za serikali. Labda tuangalie mfano mmoja tu wa Mkataba wa Buzwagi ambao ulikuwa ni maarufu kama ‘Mkataba wa Karamagi’ kati ya Waziri wa Nishati na Madini Nazir Karamagi na Kampuni ya Barrik Gold Mine. Mkataba huu ulikuwa ni siri kubwa baina ya Barrik na Waziri tu, hali iliyopelekea Mbunge Zitto Kabwe kusimamishwa shughuli za bunge kwa miezi minne baada ya yeye kuhoji uhalali na uharaka wa utiaji saini mkataba huo uliosainiwa hotelini [Churchil Hotel] mjini London Uingereza.
Hivi nchi yetu itakuwa kituko mpaka lini? Mbona hatuoni viongozi wanaoleta tija na maendeleo.
Nakumbuka Rais Thabo Mbeki wa Afika Kusini alitudharau sana alipokuwa katika moja ya ziara zake hapa nchini, alisema wakati biashara ya Tanzanite inatoa dola milioni 500 kwa mwaka duniani, Tanzania nchi pekee duniani yenye madini hayo inapata dola 80 tu. Rais Mbeki alitukejeli kwa kusema hakuna sababu ya kumtafutamchawi wakati sheria ya uchimbaji madini tumeitunga wenyewe inayoruhusu wageni waondoke na asilimia kubwa ya madini hayo na sisi kuambulia mashimo.
Hali hii inanipa shaka hasa nikichunguza upeo wa kufikiri wa hawa viongozi wetu, ndipo ninapokumbuka usemi wa Waziri mstaafu Arcado Mtagazwa [CCM] alioutoa bungeni mwaka 1993, alisema “Tutakapokufa vizazi vijavyo vitafukua makaburi yetu ili vione vichwa vyetu viongozi vilikuwa na ubongo wa aina gain kwa sababu yaelekea hatufikiri sawasawa”.
Kauli hii ililazimika kutolewa baada ya kuona kwamba baadhi ya maamuzi yanayofikiwa na serikali yetu hayana maslahi kwa taifa na ni ubinafsi.


10. RUSHWA

Katiba ya CCM katika ahadi yake ya nne [4] ina sema “rushwa ni adui wa haki, sitatoa rushwa wala kupokea rushwa”. Jambo la rushwa pia Mzee wetu mpendwa Mwl Nyerere alilikemea vikali enzi za uhai wake kwani alijua wazi kuwa rushwa ni kikwazo cha maendeleo ya umma katika kila Taifa.
Leo hi inchi yetu imegubikwa na rushwa na hata kuhalalishwa na kuitwa ‘takrima’ ili tu kukidhi matakwa na mahitaji ya ‘mahafidhina’. Viongozi wa serikali, viongozi katika taasisi mbalimbali wameweka mbele rushwa kama msingi wa kushibisha matumbo yao. 
Baya zaidi hata viongozi wa CCM chama pekee kilicho asisiwa na Baba wa Taifa Mwl Nyerere wamezisahau kabisa falsafa zake na chuki yake dhidi ya rushwa na hata katika Chaguzi mbalimbali za Chama Cha mapinduzi zilizofanyika siku chache zilizopita tumeweza kusikia kama sio kushuhudia vitendo vya rushwa vikifanyika waziwazi katika chaguzi hizo jambo ambalo licha ya kushindwa kutumia mamlaka aliyonayo katika kuviasaidia vyombo husika kuchukua hatua za kisheria amebaki akilalamika na kushtaki kwa wananchi kuhusiana na vitendo hivyo vichafu vinavyotendeka ndani ya CCM, Serikali na hata katika sekta nyinginezo nyingi nchini.
 Nakumbuka Mh Kabuye [Mb-TLP] aliwahi kuwashutumu bungeni kuwa anauhakika wabunge wote waliingia kwa rushwa, wabunge hao walioshutumiwa walimtaka Kabuye afute kauli naye alisema “ kwa kulazimishwa nafuta kauli”. Walimlazimisha lakini hoja yake ilibaki kuwa ni ya msingi.


11. UCHU WA MADARAKA

Mwl Nyerere ni miongoni mwa viongozi wachache sana duniani waliokosa kuwa na uchu wa madaraka. Ni miaka 24 sasa tangu Mwl ang’atuke madarakani kwa hiari yake akiwa kama rais wa awamu ya kwanza wa nchi yetu na ni miaka 22 tangu aachie uongozi wa CCM kama Mwenyekiti wa chama. Ndipo alipoamua kwa hiari yake kurejea Butihama na kuendeleza kilimo.
Uroho wa madaraka leo hii umekithiri, viongozi wengi wanaendelea kung’ang’ania madaraka bila kujali uzee walionao. Mahafidhina hawa wamezoea kusema ‘vijana ni taifa la kesho’ ili wao wazee waendelee kuhujumu mali za nchi yetu. Na unafiki wao ni pale wanaposema ‘vijana ni nguvu kazi ya taifa’, sentensi hizi mbili kimantiki zinakinzana. Mbaya zaidi na kinachouma ni pale unapoona watoto wa vigogo au viongozi wa Serikali wakiwa ndio kama warithi wa nafasi za wazazi wao ndani ya CCM na hata Serikali ya CCM. Hili linaweza kujithibitisha wazi iwapo utaamua kufuatilia kwa undani idadi ya watoto wa vigogo na Viongozi waliomo ndani ya CCM sambamba na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi [CCM]

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...