SERIKALI
imeitaka kampuni ya New Habari 2006, kuacha kuchapisha gazeti la Rai
kila siku na kampuni ya Mwananchi kuacha kuchapisha gazeti la Mwananchi
kwenye mtandao.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari Malelezo,
Assah Mwamebene, alitoa onyo hilo ofisini kwake jana na kuongeza kuwa
ameziandikia barua kampuni hizo, zijieleze ni kwanini zinafanya hivyo.
“Tumeona gazeti la Mwananchi baada ya
kufungiwa, limeendelea kuchapishwa kwenye mtandano wa intaneti kinyume
na amri iliyotolewa. Vivyo hivyo kwa Rai ambayo ilikuwa ikichapishwa
mara moja kwa wiki, imeanza kutoka kila siku, tunawataka warejee ratiba
yao,” alisema.
Alisema endapo vyombo hivyo
havitatekeleza agizo hilo na kujieleza katika ofisi yao ifikapo kesho,
Serikali italazimika kuchukua hatua kali zaidi ikiwa ni pamoja na
kuongeza adhabu, ikiwemo kufungia kwa muda usiojulikana na kufutiwa
usajili wake.
“Umma ufahamu kuwa Serikali
haikukurupuka kufungia magazeti hayo, uamuzi ulifanywa baada ya kufuata
taratibu zote za msingi ikiwemo kuwasikiliza wahusika.
“Katika suala hili hatutarudi nyuma,
hata waje wanaharakati wa aina gani, lengo la Serikali ni kuhakikisha
maadili yanazingatiwa katika taaluma na hatutakuwa na mchezo katika
maslahi ya nchi,” alisema.
Gazeti la Mwananchi limefungiwa kwa muda
wa wiki mbili na Mtanzania, linalomilikiwa kampuni ya New Habari 2006,
limefungiwa kwa miezi mitatu kuanzia Septemba 27 mwaka huu kwa mujibu wa
Sheria ya Magazeti ya 1976 na kanuni zake za mwaka 1977.
Alipoulizwa Mhariri Mtendaji Mkuu wa New
Habari 2006 Ltd, Absalom Kibada, alidai wamefuata utaratibu kuchapa
gazeti la Rai kila siku, lililoanza kutoka baada ya kufungiwa gazeti la
Mtanzania, lililokuwa likitoka kila siku.
Alidai kuwa kampuni ya New Habari 2006
Ltd, ina kibali kilichotolewa mwaka 1994, hivyo alichofanya ni kumuarifu
Msajili mabadiliko ya ratiba ya utokaji wa gazeti hilo.
“Kampuni
yetu imerithi mambo yote ya wamiliki wa awali, mwaka 1994 msajili
aliruhusu Rai kutoka kila siku, na Jumatatu tulimuarifu Msajili kuhusu
kuanza ratiba hiyo, hivyo tumefuata utaratibu wote.
Hatua hii ya sasa ni kutaka kuiadhibu Rai kwa makosa ya Mtanzania,”
alidai. Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mwananchi Communications
Limited (MCL), Bakari Machumu hakupatikana kuzungumzia suala hilo baada
ya simu yake ya kiganjani kuita bila majibu.
SOURCE: HABARI LEO
No comments:
Post a Comment