Na Daniel Mbega
UHALIFU nchini Tanzania umekuwepo kwa miaka mingi, lakini katika miaka ya karibuni umeonekana kushika kasi kuliko ilivyowahi kutokea, kiasi cha kutishia amani kwa Watanzania kuhusu usalama wa maisha na mali zao.
Kati ya Januari 2005 hadi Januari 2006 kulikuwepo na matukio ya uhalifu na ujambazi wa kutumia silaha ambapo kiasi cha Shs. 16,782,172,419 kiliporwa katika benki kadhaa za maduka ya kubadilishia fedha nchini.
Takwimu zinaeleza kwamba jumla ya wahalifu 46, wakiwemo raia 12 wa Kenya, walikamatwa katika kipindi hicho wakihusishwa na matukio mbalimbali ya uhalifu.
Baada ya hapo ikafuatia kasheshe kubwa
ndani ya Jeshi la Polisi, sekeseke ambalo lilifanya iibuliwe orodha ya
maofisa 20 wa jeshi hilo ambao wanashirikiana na majambazi katika wizi
huo.
Lakini wakati huo zilikuja taarifa
mfululizo zikiwatuhumu askari kadhaa ndani ya jeshi hilo ambao wanadaiwa
kujihusisha na vitendo vya uhalifu, huku wakiwa wamechuma mali nyingi
ambazo haijulikani namna walivyozipata kulinganisha na mishahara yao.
Kama nilivyotangulia kusema, vitendo
vya uhalifu hapa nchini vimekuwepo kwa miaka mingi, na kwa kumbukumbu
zangu vitendo hivi vilianza kushika kasi mwanzoni mwa miaka ya 1980.
Vitendo hivi vya uhalifu si ujambazi
tu, bali ni pamoja na uhujumu uchumi, magendo pamoja na wizi wa
maofisini. Uhujumu uchumi huu ndio uliomfanya Waziri Mkuu wa wakati ule,
hayati Edward Moringe Sokoine, akasimama kidete kukabiliana na
wafanyabiashara na watu wote waliokuwa wakijihusisha na magendo mwanzoni
mwa miaka hiyo ya 1980.
Wapo wengi waliokumbwa na kimbunga cha
Sokoine, na wengi wao walikuwa watumishi wa umma, katika Chama na hata
serikali, ambao ama walishiriki moja kwa moja au waliwatumia jamaa zao
katika harakati zao za kuvuna wasichopanda.
Sokoine alikuwa sahihi, kwa sababu
hali ilikuwa mbaya katika kipindi hicho, kipindi ambacho binafsi siwezi
kukisahau kwa sababu bidhaa zote muhimu ziliadimika kiasi kwamba wengine
wakaona kulikuwa na afadhali wakati wa mkoloni kuliko kipindi hicho.
Maduka ya kaya, ambayo yalichipua kila
sehemu Tanzania, kuanzia mijini mpaka vijijini, yalikuwa hayana vitu
vile muhimu kama sukari, sabuni, na kadhalika. Watu wachache, tena wale
waliokuwa watumishi wa umma, walishirikiana na baadhi ya wafanyabiashara
kuuza vitu vilivyostahili kuletwa kwenye maduka hayo. Kilikuwa kipindi
cha ulanguzi!
Nakumbuka tulikuwa tukiweka foleni ya
mawe kwa kusubiri sukari ambayo ilikuwa inakuja baada ya mwezi au miezi
miwili, na hata ilipokuja tukalazimishwa kununua kilo moja moja tu
ambayo pia iliambatana na kulazimishwa kununua jembe la mkono 'Chapa
Jogoo'!
Ni mateso haya ya wananchi ambayo
yalimfanya Waziri Mkuu Sokoine aingilie kati na kuanza kupambana na
wahujumu uchumi na wafanya magendo, hasa baada ya kugundulika kwamba
bidhaa hizo zilikuwa zikiuzwa usiku na kwa usiri mkubwa. Waliohusika ni
wale wale waliokuwa na dhima ya kuwatumikia wananchi.
Ujambazi katika kipindi hicho cha
Sokoine ulichomoza kwa kasi ya ajabu, na hii ilitokana na ukweli kwamba,
kulikuwa na watu wengi waliokuwa na silaha. Watu hawa walivamia benki
na kuteka nyara magari ya abiria kwa ya mizigo, kisha kuchota mali
ambazo hawakuzichuma.
Watu hawa, kwa asilimia kubwa,
walikuwa ni wale askari walioshiriki katika Vita ya Kagera, vita pekee
ambayo Tanzania huru imewahi kupigana. Baada ya kumtoa Dikteta Nduli Idi
Amini Dada na kumfukuza kabisa Uganda, askari hawa, mashujaa wetu,
baadhi yao walirejea makwao wakiwa na silaha pamoja na magwanda ya
jeshi. Hawakuyarejesha kwenye kambi zao, nadhani kwa sababu ya furaha
iliyokuwepo wakati huo na hakuna aliyewatilia shaka.
Kila mmoja aliwasifu mashujaa hao kwa
kumng'oa madarakani Amini, na inawezekana hata makamanda wa jeshi
wakajisahau kuwataka askari hao warejeshe silaha, ingawa wapo waungwana
ambao walizirejesha.
Hawa ambao hawakuzirejesha, hatimaye
wakaamua kabisa kuachana na jeshi na kuingia uraiani, na wengine kwa
tamaa zao ama kuona kwamba wao binafsi hawakunufaika na ushindi huo,
wakaamua kutumia silaha hizo na magwanda kwa njia haramu ya kujipatia
mali. Wakaanza kushiriki vitendo vya ujambazi wa kutumia silaha.
Alhaji Ally Hassan Mwinyi alipoingia
madarakani mwaka 1985 kwa kauli mbiu yake ya 'Fagio la Chuma', aliwagusa
zaidi wafanyakazi na viongozi wazembe, lakini kamwe hakuwagusa
majambazi kwa kudhani kwamba walikuwa wamekimbia! Lakini kumbe umafia
ulikuwa umeingia nchini.
Hakuna mtu asiyelijua neno 'MAFIA'
hapa Tanzania. Hata mtoto mdogo ukimuuliza anaweza akakwambia kwamba mtu
akisema 'Mafia' ana maana gani. Sikatai kwamba yawezekana wapo
wasioijua maana halisi ya neno hili wala asili yake.
Labda nidokeze kidogo asili na fasili
ya neno hili. Mafia ni kifupi cha maneno 'Morte alla Francia Italia
anela'katika lugha ya Kitaliano yakiwa na maana; 'Kifo kwa Mfaransa ni
kilio kwa Mtaliano'. Wengine wanaitafsili Mafia kama: 'Mazzini autorizza
furti, incendi, avvelenament' yakimaanisha kwamba 'Mazzini anaruhusu
wizi, unyang'anyi, mauaji ya sumu!' Mazzini ndiye aliyekuwa bosi wa
Mafia, ambao asili yao hasa ni katika visiwa vya Sicily nchini Italia,
ambapo historia inaonyesha kwamba kundi hili liliundwa zamani sana
katika mwaka 1282 baada ya kuwatimua Wafaransa waliokuwa wakikikali
kisiwa hicho. Lengo lao kubwa lilikuwa kutetea maslahi yao.
Hata hivyo, miaka mingi baadaye
wanachama wa kundi hili wakaanza kujihusisha na vitendo vya uhalifu kama
wizi, ujambazi, mauaji ya kutisha, na hata kuhujumu siasa na uchumi wa
nchi mbalimbali.
Mpaka leo hii, Mafia bado wapo na wana
wanachama wao karibu katika kila nchi ulimwenguni kote, kwani
wanajihusisha na ujambazi, uuzaji na usafirishaji wa dawa za kulevya,
utekaji nyara wa magari ya mishahara na hata viongozi na watu maarufu
kwa lengo la kujipatia fedha. Mauaji kwao ni kitu cha kawaida, na karibu
wote wamekula yamini kutotoa siri nje hata kama watalazimika kufa.
Hawa ndio Mafia ambao tumezowea kuwarejea tunapozungumzia matukio mbalimbali ya ajabu yanayowahusu watu fulani.
Ni kwa mantiki hiyo basi nimelazimika
kuandika makala haya nikisema Mafia wako ndani ya Tanzania na ndio
wakijihusisha na vitendo vya uhalifu. Hii ni kwa sababu Mafia hawa
miongoni mwao wako serikalini, ndani ya vyama vya siasa, wafanyabiashara
na watumishi wa idara nyingine nyingi nyeti.
Wengine wapo hata katika vyombo vya sheria, mathalani Bunge, Mahakama na hata kwenye majeshi.
Itakumbukwa kwamba, Rais Mwinyi
alipotoa 'ruksa' kwa kila kitu, ujambazi ukafumuka kama sisimizi.
Ulifumuka pamoja na biashara nyingi ambazo kabla ya hapo hazikufikiriwa,
ikiwemo biashara ya dawa za kulevya pamoja na utumiaji wake. Pia
uuazaji wa nyara za serikali kama pembe za ndovu na faru, ngozi za
wanyama pamoja na madini!
Mambo yote haya yasingeweza kufanikiwa
kwa mtu wa kawaida. Jambazi wa kawaida hawezi kuota kwamba benki fulani
kuna fedha mahali fulani halafu akaja na wenzake na kuiba kwa kutumia
muda usiozidi nusu saa. Lazima atakuwa ameshirikiana na watu fulani
ambao wanaifahamu ratiba na ramani halisi ya mahali husika.
Kwa maana nyingine, lazima kuwe na
mtandao madhubuti, kama ambavyo tumeyashuhudia matukio mengi ya wizi
katika benki, maduka ya kubadilishia fedha za kigeni, kwenye majumba na
hata kwenye maduka ya wafanyabiashara wakubwa.
Ni mtandao huu ambao tunaweza kuuita
uko katika kundi la Mafia, ambao umefanya mpaka maofisa wa jeshi la
polisi wahusishwe moja kwa moja, kwani hawa wanawafahamu majambazi.
Taarifa zinaonyesha kwamba, katika
baadhi ya matukio, wakati mwingine majambazi huwa wakiwapigia simu
baadhi ya polisi, kuwaeleza kwamba wanakwenda kufanya tukio mahali
fulani, hivyo wasishangae. Na katika hali ya kushangaza, hata polisi wa
doria huwa hawapangwi katika eneo husika na wakubwa zao kwa hofu kwamba
wanaweza kuwatibulia.
Kila wakifanya tukio, lazima baadaye
kwa siri wawapelekee wazee 'mzigo' katika kujisafishia njia kwamba hata
siku nyingine wanaweza kulindwa. Kwa maana nyingine, maofisa hawa
wanawafahamu fika wahalifu na wanawajua kama reale kwa ya pili! Ina
maana hata leo hii wakibanwa, lazima watawataja majambazi wote wa nchi
nzima.
Inavyoonyesha ni kwamba, mtandao wa
uhalifu umeenea sana kama ule wa Mafia, kwani siyo ajabu kukuta
majambazi wa Tanzania wakaenda kufanya uhalifu wao Kenya, na wale wa
Kenya wakaja Tanzania.
Polisi pia wanawafahamu hata wale
majambazi wa kigeni kama kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambao
hujificha katika nyumba za wageni hapa jijini.
Zaidi polisi wanafahamu hata uingiaji
wa silaha zinazotumika katika uhalifu huo, mbali ya kwamba hata wenyewe
huwa wanawakodisha majambazi silaha zao.
Nakumbuka miaka kadhaa iliyopita
nilikuwa natokea Dodoma. Muda mfupi kabla sijaondoka nikiwa nimekata
tikiti yangu, bwana mdogo mmoja anayenifahamu akaniita pembeni na
kunielekeza kwa kijana mmoja mdogo tu kama yeye, yapata kama miaka 22
hivi.
"Unamuona yule," alisema kijana huyo akinionyesha kwa kidole kijana huyo ambaye alikuwa mbali kidogo.
Nikamjibu ndiyo nimeomuona. Kisha
akasema, "Basi brother, kama unahitaji bastola, rifle au SMG mwambie tu.
Ameingia jana na anazo kama saba hivi!"
Nilinyamaza kidogo nikitafakari kabla
sijamuuliza kijana wangu huyu alijuaje. Akaniambia kwamba kijana huyo
mgeni alimwendea asubuhi hiyo na kumshauri amtafutie wateja wa 'bidhaa'
zake.
"Hata wewe kama unataka sema, bastola
anauza shilingi 500,000 tu na unaweza kurudisha fedha zako katika
kipindi kifupi sana pamoja na faida," akaniambia kijana huyu.
"Nitarudishaje?" nikamuuliza swali kwa
mtego. Yeye akajibu haraka haraka kwa kusema ninaweza kuikodisha kwa
'watu wa kazi'! Nilimkazia macho halafu nikamuuliza kwamba niwakodishe
majambazi, wakaue na kuiba, kisha ndipo waniletee silaha yangu na fedha?
Yeye akajibu haraka haraka kwamba ndivyo alivyomaanisha.
"Kama polisi wanakodisha SMG kwa
majambazi na wanachuma fedha, wewe unaogopa nini? Kwani wewe ndiwe
unayeingia vitani?" akaniuliza.
Lakini nikamwonya kamwe asijidanganye
kuingia katika biashara hiyo. Jambazi anayekwenda kuiba na kuua, na yule
anayemkodisha silaha, wote ni majambazi tu!
Kilichonishangaza zaidi ni kwamba,
kijana yule inasemekana silaha hizo alikuwa anazinunua kwenye kambi za
wakimbizi huko Ngara. Lakini nikajiuliza, anaweza kusafiri kutoka Ngara
hadi Dodoma, na pengine hata Morogoro au Arusha, bila kukamatwa na
polisi?
"Wewe brother utafikiri siyo msomi?
Kuna kitu kinachoshindikana mbele ya fedha? Polisi wenyewe wakati
mwingine huwa wanawasindikiza majambazi, sembuse mtu kupita na silaha!"
kijana yule akasema katika namna ya kunizodoa.
Huyu ni miongoni mwa watu wengi
wanaofanya biashara hiyo ya silaha, na kwamba wanashiriki moja kwa moja
kwenye ujambazi na ndiyo maana uhalifu unazidi kumea kila siku. Na hii
inatokana na mtandao wao waliouweka mpaka serikalini.
Wapo viongozi wengine wa serikali
wanaoshiriki katika uuzaji wa nyara za serikali, wapo wanaoshiriki
katika biashara za dawa za kulevya, kama wale wabunge kadhaa ambao
waliibuka tu ghafla kutoka vijiweni na kuwa na mali nyingi katika
kipindi kifupi.
Hawa nao wameingia kwenye chombo cha
kutunga sheria ili waweze kutunga sheria zinazowapa unafuu wahalifu
wengi kote nchini. Wahalifu hawa wameingia serikalini ili kuficha maovu
yao, japo ni miongoni mwa majambazi sugu waliokuwa wakitafutwa na
polisi.
Wapo wafanyabiashara wanaodaiwa kuwa
majambazi na wamekuwa mstari wa mbele kuvisaidia vyama vya siasa fedha
za kampeni na mambo mengine kadha wa kadha, ili tu kuficha maovu yao.
Pengine nimalizie kwa kusema, vyombo
vya ulinzi na usalama vinapaswa kutekeleza wajibu wao kikamilifu katika
kupambana na mtandao huu mpana wa Mafia hapa nchini. Kinyume cha hapo,
wananchi wanaweza kuchoshwa na vitendo hivi, na kwa hakika, mnyonge
anaposema 'sasa yatosha' madhara yake huwa ni makubwa, kwani huwa hajali
nini kitakachotokea! <MWISHO>.
No comments:
Post a Comment