Mwenyekiti Wa Makampuni ya IPP Reginald Mengi
MWENYEKITI wa Makampuni ya IPP, Reginald
Mengi amesema Watanzania wengi wanazidi kuwa masikini kwa sababu
hawazitumii fursa za utajiri uliopo nchini, hivyo kutaka vijana kuona
kwa macho fursa hizo ili waweze kujikwamua kutoka kwenye dimbwi hilo la
umasikini.
Akizungumza wakati wa kutoa zawadi kwa
washindi watatu wa shindano la nini kifanyike kuzalisha ajira nyingi
hapa nchini aliloanzisha Mwenyekiti huyo wa IPP, Mengi alisema baada ya
Watanzania kupofushwa kuwa nchi yao ni masikini, wengi walibweteka na
kushindwa kuchangamkia fursa zilizopo hali ambayo imeifikisha nchi hapa
ilipo.
Alisema jambo la msingi kwa vijana wa
Tanzania ni kuibua mawazo ya shughuli gani atafanya badala ya kukimbilia
namna ya kupata mitaji, kwani wengi ambao wamekimbilia kutafuta mitaji
wamejikuta wanaipata mitaji hiyo, lakini wakashindwa namna ya kuitumia.
Washindi katika shindano hilo ambalo
limeanzishwa na Mengi lijulikanalo kama Tweet Bora ni Lilian Wilson wa
Chuo Kikuu cha Ardhi aliyepata Sh milioni moja, Susan Senga ambaye ni
mfanyabiashara ndogo alipata Sh 500,000 na Ombeni Kaaya ambaye ni
mjasiriamali kutoka Nzega, Tabora aliyekabidhiwa Sh 300,000.
Katika maoni yao, Lilian alipendekeza
kuwa ili kuondoa tatizo la ajira wajasiriamali waliofanikiwa na Serikali
waanzishe mifuko ya kuwekeza mitaji kwenye biashara za vijana zenye
uwezekano wa kukua haraka badala ya kutegemea mikopo ya benki au taasisi
za fedha.
Susan Senga yeye alipendekeza kuanzishwe
vipindi maalumu kutoa elimu ya ujasiriamali ya kuwawezesha vijana
kuwatoa katika fikra ya kuishi kutegemea ajira ili kujiairi.
Kwa upande wake, Ombeni Kaaya katika
maoni yake alisema tafiti wanazofanya wanafunzi wa elimu ya juu mwaka wa
mwisho zihusu jinsi watakavyojiajiri katika fani zao kwani itasaidia
wengi wajiajiri.
Naye Dk Donath Olomi wa Taasisi ya
Management and Entrepreneurship Development ambao ndio wanaoteua
washindi, alisema katika shindano la mwezi huu jumla ya maoni 979
yalipokewa na watachagua washindi watatu kutoka katika maoni hayo.Chanzo Mwananchi Online
No comments:
Post a Comment