RAIS wa
zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela (95), jana aliondolewa hospitali
na kurejeshwa nyumbani ambako ataendelea na matibabu ya maradhi ya
mapafu. Hata hivyo, taarifa ya Serikali ya Afrika Kusini imesema uamuzi
huo hauna maana kwamba Mandela amepata nafuu kwa vile hali yake bado ni
mbaya na wakati mwingine hudorora zaidi.
Taarifa
hiyo imeongeza timu ya madaktari wa Mandela inaamini ataendelea kupata
matibabu katika makazi yake mjini Houghton kwa kiwango sawa na anayopata
akiwa hospitalini mjini Pretoria.
Tangazo hilo limekuja siku moja tu baada ya maofisa wa serikali kukanusha ripoti kuwa shujaa huyo wa taifa hilo, alisharuhusiwa.
Mshindi
huyo wa tuzo ya amani ya Nobel aliyekuwa amelazwa hospitali tangu Juni
8, mwaka huu anaheshimiwa duniani kwa kuongoza mapambano dhidi ya
utawala wa kibaguzi wa wazungu wachache na kuhubiri upatanisho na
maridhiano na jamii za weupe pamoja na kufungwa miaka 27 jela.
"Timu ya
madaktari imetuhakikishia kuwa Mandela atapokea matibabu kwa sawa na
anachopata hospitalini mjini Pretoria atakapokuwa katika makazi yake ya
Houghton," taarifa ya Ofisi ya Rais ilisema.
"Lakini ikibidi, atarejeshwa hospitali," taarifa hiyo ilisema na kuongeza kwamba inamtakia Mandela afya njema.
Nyumba ya Mandela imerekebishwa kwa ajili ya kumruhusu kupata matibabu ya mgonjwa mahututi akiwa hapo.
Wachambuzi
wa mambo wanasema kuruhusiwa kwa Mandela hakumaanishi mtu aliyepata
nafuu bali kumhamisha kutoka wodi ya hospitali kwenda wodi
iliyotengenezwa maalumu ya nyumbani kwa matakwa ya familia yake.
Hata
hivyo, wanasema inachotia moyo ni kwamba madaktari wake wamesema Mandela
yuko imara kuweza kuhimili safari ya kilomita 55 kutoka hospitalini
kwenda nyumbani kwake.
No comments:
Post a Comment