HUWEZI kutawala miili ya watu ukaacha mioyo yao. Ndiyo, mjumbe hauawi, ni kauli ya hekima ya tangu enzi za wahenga wetu.
Leo ni
mwaka mmoja tangu mwandishi wa habari na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama
cha Wandishi wa Habari mkoani Iringa,Daud Mwangosi kuawa.
Ilikuwa
ni Jumapili ya Septemba 2, 2012. Hakika, siku ile itabaki katika
kumbukumbu za Watanzania kwa mamilioni. Ni kwa kufikiwa na taarifa za
kutisha za mauaji ya mwandishi wa habari. Haya yanaingia katika historia
kuwa ni mauaji ya kwanza kwa mwandishi wa habari kufanyika hadharani
tangu nchi hii ipate Uhuru. Wengi watakuja kukumbuka walikuwa wapi na
walifanya nini siku walipopata taarifa hizo za kutisha. Binafsi, taarifa
ile ya mauaji ya Daud Mwangosi siku ile ya Jumapili ya huzuni kwa Taifa
ilinikuta nikiwa Iringa Mjini. N umbali wa mwendo wa saa moja kwa gari
kufika eneo la tukio, Nyololo, Mufindi.
Jioni
ile nilikuwa nikifundisha soka ya watoto. Mara baada ya kupata taarifa
zile kwa simu, nilisitisha mazoezi yale ya watoto. Nikawapa taarifa
zile. Nilipowaambia kuwa nimepata taarifa sasa hivi kuwa mwandishi wa
habari ameuawa Mafinga, mtoto mmoja akaniangalia na kuniuliza; “
Kwanini?”
Ndiyo, swali la mtoto yule ndilo umma wa Watanzania unapaswa uendelee kujiuliza hata leo; KWA NINI?
Mwandishi
wa habari ni mjumbe katika jamii. Anapokuwa akifanya kazi yake hapaswi
kuwa na hofu ya kudhuriwa kwa kukusudia na waliopata mafunzo ya kutumia
silaha. Ndivyo ilivyo kwa watumishi wa Msalaba Mwekundu, wanapokuwa
kazini kwenye maeneo hata ya vita.
Askari
asiyejua kutofautisha kati ya mwanahabari aliyeshika kamera, mtu wa
Msalaba Mwekundu aliyeshika mkoba wa Huduma ya Kwanza na raia
anayefanya vurugu au adui aliyeshika silaha vitani, huyo hawezi kuwa ni
askari makini.
Na
hakika, kama Taifa, tunafanya makosa kuamini, kuwa nchi yetu ni ya
amani kwa vile wananchi wetu hawagombani. Kama watu hawagombani kuwa na
maana nchi ni ya amani yaweza kuwa tafsiri potofu ya maana nzima ya
amani. Maana, kama watu hawagombani mahali pasipo na haki, usawa na
uadilifu wa viongozi; mahali palipojaa dhuluma,unyanyasaji na maovu
mengine wanayotendewa au wanaotendeana wanajamii, basi, amani hiyo
itakuwa ni ya muda tu.
Maana,
kwa watu wenye kuishi kwenye mazingira hayo bila kugombana wala kutokea
uvunjifu wa amani, hiyo itakuwa na maana ifuatayo; ama watu hao
hawaelewi kuwa wanaishi katika mazingira hayo ya dhuluma na maovu
mengine wanayotendewa au kutendeana, au wamejawa na hofu.
Hivyo
basi, kwa hilo la mwisho, itakuwa ni amani iliyojengeka katika misingi
ya hofu. Na hofu hiyo haiwezi kuwa ya kudumu. Kuna siku mwanadamu
hufikia ukomo wa kuhofia. Ukimwandama sana mjusi, mwisho hugeuka nyoka!
Ndipo hapo tunapoona nchi zinalipuka na watu kuchinjana.
Hii ni
nchi yetu. Katika tofauti zetu hizi za kiitikadi tusifike mahali
tukashindwa kuongea kama Watanzania kwa kutanguliza maslahi ya Tanzania.
Kuna umma uliopo na unaokuja. Umma unaotegemea sana busara katika
uongozi wetu. Tuanze sasa kujenga utamaduni wa kuitumikia nchi yetu kwa
kufanya na kuamua yale yenye maslahi kwa Tanzania. Hivi vyama vya siasa
vipo leo na kesho havipo. Vinakuja na kuondoka, lakini Tanzania kama
nchi itakuwapo daima.
Tusifike
mahali tukabaki tunawaangalia wanasiasa wetu, kwa maslahi yao binafsi,
ya makundi yao na vyama vyao, wakashinikiza au kuelekeza yale yenye
kuchochea machafuko makubwa ya kijamii. Ni wajibu wa viongozi wa kisiasa
kutanguliza busara katika kila maamuzi wayafanyao.
Na
tunafanyaje pale tunapowaona viongozi wa kisiasa na watendaji wakifanya
maamuzi yasiyo na busara na kusababisha Watanzania wenzetu kupoteza
uhai na hata kuchochea machafuko?
Jibu; Kama Watanzania wazawa na wazalendo wa nchi hii, tuna wajibu wa kuyalaani matendo yao maovu.
Na
katika nchi zetu hizi, ni kazi rahisi sana kuanzisha vurugu na kujenga
mazingira ya chuki na uhasama, lakini, ni kazi kubwa sana kumaliza
vurugu na kuondosha mazingira hayo ya chuki na uhasama. Na nchi yetu
kamwe haiwezi kupiga hatua za maana za maendeleo katikati ya mazingira
ya vurugu, chuki na uhasama, uwe wa vyama vya siasa au wanajamii.
Kihistoria,
Watanzania tumeishi kwa amani na upendo bila kuwa na chuki na uhasama
miongoni mwetu unaotokana na tofauti zetu za kidini na kikabila.
Tunaziona sasa, dalili za baadhi ya wanasiasa, kwa malengo ya kisiasa,
kutaka kupandikiza miongoni mwetu uhasama na chuki kwa kutumia tofauti
zetu za kidini na kikabila, tofauti zetu za kiitikadi. Wanafanya hivyo
mara ile wanaposhindwa kujenga hoja za kisiasa kwenye majukwaa ya
kisiasa. Hawa ni watu hatari sana kwa maslahi ya taifa letu.
Katika
nchi zetu hizi, ni wanasiasa wa aina hii ambao, katika kufanikisha
malengo yao, huwa tayari hata kuwalipa vijana wasio na ajira na
kuwavutisha bangi ili washiriki vurugu za kisiasa, kidini na kikabila.
Tumeyaona hayo Liberia, Ivory Coast na hata katika nchi jirani na kwetu.
Tusipokuwa makini, yako karibu kupisha hodi kwenye nchi yetu, kama si tayari kuwa yameshaingia ndani ya nchi yetu.
Hii ni
nchi yetu. Tutafanya makosa makubwa kuwaachia viongozi wa kisiasa
pekee, jukumu la kulinda maslahi ya nchi yetu. Tunapita sasa katika
kipindi kigumu tangu tupate Uhuru. Dunia
imebadilika, na nchi yetu inapitia kwenye kipindi cha mabadiliko.
Hakuna mtu au chama cha siasa kinachoweza kuyazuia mabadiliko haya.
Kufanya hivyo ni kutuletea machafuko na kuvunja amani yetu. Tuna jukumu
la kufanya tunayoweza, na kwa kutanguliza busara, kuipitisha salama nchi
yetu katika kipindi hiki cha mabadiliko.
Maana,
tukiingia kwenye machafuko, basi, hakutakuwa na mshindi, maana, sote
tutashindwa. Na kifo cha Daudi Mwangosi kinatutaka tuyatafakari haya.
Maggid,
Iringa.
No comments:
Post a Comment