Mkurugenzi
Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited, Tido Mhando (kushoto)
akimwangalia Mkurugenzi wa Kampuni ya Vodacom, Rene Meza alipokuwa
akijisajili katika huduma ya habari zilizotokea hivi punde (Breaking
News) kwenye hafla ya uzinduzi wa huduma hiyo Dar es Salaam, jana. Picha
na Silvan Kiwale
Kampuni ya
Vodacom Tanzania na Mwananchi Communications Limited (MCL), zimezindua
mradi wa kufikisha habari za punde (Breaking News) kwa jamii, kuanzia
leo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi
huo Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom, Rene Meza
alisema kwa kuanzia, wanatarajia wateja wasiopungua milioni kumi
kujiunga na huduma hiyo."Mtumiaji mtandao wa Vodacom ataunganishwa na huduma hii kwa kupeleka ujumbe wenye neno Habari kwenda namba 15569, kwa gharama ya Sh150 kwa siku, tunafurahia hatua hii kwani tuna hakika itatuimarisha sokoni," alisema Rene.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Tido Mhando alisema mradi huo umegharimu mwaka mmoja na nusu kuuandaa.
Mhando alisema mradi huo ni wa kitaifa na kimataifa, lengo ni kuwawezesha kupata habari yoyote kubwa, duniani na kuirusha papohapo kwa atakayekuwa amejiunga nao.
Huduma hiyo itatolewa kwa saa 24 na inalenga kufikia wateja wote wa Vodacom, ambao ni zaidi ya nusu ya watumiaji simu za kiganjani nchini, wanaokadiriwa kufikia milioni 28.
Mhando alibainisha kuwa lengo ni kudhibiti athari zinazotokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia kwa tasnia ya habari, kwani upashanaji habari umekuwa wenye kasi zaidi, huku magazeti yakisubiriwa kutoa uhakika na ufafanuzi kwa kina.
"Wateja wetu katika mradi huu watanufaika zaidi ya wengine, kwa kupata dokezo za habari zenye uhakika, kabla ya kupata undani wake katika magazeti yetu ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti," alisema Mhando.
Mkurugenzi huyo alisema kwa kiwango cha chini, watahakikisha mteja anapata habari za punde nyingi, kutoka ndani na nje ya nchi zisizopungua tatu na kuendelea bila ukomo.chanzo mwananchi
No comments:
Post a Comment