kurugenzi wa Mashtaka ya Umma Zanzibar,(DPP) Ibrahim Mzee Ibrahim
Barua hizo pamoja na taarifa za kikao kilichofanyika Aprili 4 mwaka huu kujadili jalada la uchunguzi wa kesi hiyo inadaiwa kiliwahusisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Othman Masoud Othman, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Ibrahim Mzee Ibrahim, Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa na Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai na Upelelezi, (DDCI) Yusuph Ilembo.
Wakili wa upande wa utetezi Abdallah Juma Mohamed alitoa taarifa hizo wakati akipinga hoja ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Abdallah Issa Mgongo, baada ya kuiomba Mahakama Kuu kuahirisha shauri la kesi hiyo kwa madai upelelezi bado haujakamilika.
Wakili huyo alisema kwamba amefanikiwa kupata barua yenye kumbukumbu namba BUB/P89/VOLV/54 ya Machi 25 mwaka huu, ambayo imeandikwa na Inspekta wa Jeshi la Polisi Suleiman Suleiman kwenda kwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Mjini Magharibi ambayo ilikuwa ikimtaka mkuu wa upelelezi kulipitia kwa kina jalada la uchunguzi na kumtaarifu kuwa mtuhumiwa amehojiwa na ametambuliwa katika gwaride maalum.
Alisema barua hiyo iliyokuwa na kichwa cha habari 'Kuua kwa makusudi Padri Evarist Mushi’ baadae jalada hilo lilipelekwa kwa Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar kabla ya kuwasilishwa katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Ibrahim Mzee Ibrahim.
Wakili Abdallah Juma Mohamed alisema kwa mujibu wa barua hiyo ambayo nakala yake aliikabidhi mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Mkusa Isaac Sepetu, Inspekta Suleiman alisema amewasilisha jalada hilo kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani kwa mtuhumiwa huyo.
Alisema kwamba kwa mujibu wa uchunguzi wake, Machi 26 mwaka huu, majumuisho ya ushahidi wote uliopatikana yalifanyika na jalada la kesi kupelekwa kwa DPP, ambapo Aprili 4 Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanizbar, Yusuph Ilembo alikula kiapo mbele ya Mrajis wa Mahakama Kuu cha kuthibitisha kukamilika kwa uchunguzi wa jalada la kesi hiyo.
Alisema kimsingi hakubaliani na hoja ya mteja wake kuendelea kubaki mahabusu hasa kwa kuzingatia Machi 25, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Mwanakwerekwe Janeth Sekiola alipokea ombi la Jeshi la Polisi la kuomba kuongezewa muda wa kuendelea kumhoji mtuhumiwa na kutoa kibali hicho.
Wakili huyo alisema kitendo cha mteja wake kuendelea kubakia mahabusu kutokana na ushahidi wa kesi hiyo kutokamilika, kinakwenda kinyume na kifungu cha 14(1)(2) cha katiba ya Zanzibar kinachozungumzia haki ya mtu kuwa huru na kuishi kama mtu huru.
Hata hivyo, Mwanasheria wa Serikali, Abdallah Issa Mgongo alipinga hoja hizo na kuieleza mahakama kuwa kesi ya msingi haiwezi kuanza kusikilizwa kabla ya kukamilika kwa ushahidi, kwa vile Jamhuri ni watu na upande wa mashtaka ili kuhakikisha haki ya kisheria inatendeka mahakamani.
"Mheshimiwa Jaji, DPP hana nia ya kumkandamiza wala kumuonea mshtakiwa, lengo letu ni kuhakikisha upelelezi unajitosheleza na kuuleta mbele ya mahakama yako, ili uweze kuusikiliza na kuutolea uamuzi" alisema Abdallah Issa Mgongo.
Kwa upande wake, Jaji Mkusa Isaac Sepetu aliliahirisha shauri hilo hadi Mei 21 mwaka huu, ambapo atatoa maamuzi kuhusu hoja zilizowasilishwa na pande zote mbili, ikiwemo suala la mtuhumiwa huyo kuachiwa huru kutokana na upande wa mashataka kuchelewa kuwasilisha ushahidi mahakamani.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment