HOTUBA
YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHE. EZEKIAH DIBOGO
WENJE (MB) KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA MAMBO YA
NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014
1.0 UTANGULIZI
Mheshimiwa
Spika, katika hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
katika bajeti ya wizara hii mwaka 2012/13, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inayoongozwa na CHADEMA ilibaini mapungufu mengi ya kiutendaji
na kiuwajibikaji katika wizara hii, na hivyo kuitaka Serikali kufanya
mambo yafuatayo ili kuboresha utendaji na ufanisi:
1. Kuziwezesha balozi zetu nje kwa kuzitengea fedha za kutosha ili ziweze kufanya kazi kwa ufanisi
2.
Kutoa idadi ya majengo ya balozi zetu nje (nyumba za mabalozi, nyumba
za maafisa wa balozi na ofisi za balozi) kwa mchanganuo wa idadi ya
nyumba katika nchi na kama nyumba hizo zina hati miliki au la.
3.
Kutoa taarifa ya namna kila ubalozi ulivyotekeleza sera ya Diplomasia
ya uchumi kwa kuzingatia kwamba balozi nyingi ziko hoi kifedha kiasi cha
kwamba waambata wa kiuchumi wanakosa fedha za kusafiri kutoka sehemu
moja hadi nyingine kwa ajili ya upelelezi wa masuala ya kiuchumi.
4.
Kulikarabati jengo la ubalozi wa Tanzania huko Msumbiji lililokuwa
limechakaa kwa kutofanyiwa ukarabati tangu 1975 ingawa jengo hilo
tulipewa bure na Serikali ya Msumbiji chini ya FRELIMO.
5.
Kujenga kitega uchumi katika kiwanja cha Tanzania kilichopo Dubai na
kukiendeleza kiwanja namba 19 tulichopewa bure na Serikali ya Uingereza
kilichopo Uingereza (Central London) ambavyo vimekuwa maficho ya wezi
kwa kutoendelezwa kwa muda mrefu na kusababisha Serikali za nchi hizo
kutaka kutaifisha viwanja hivyo.
7.
Kukarabati jengo la ubalozi wetu nchini China ambalo lilikuwa na nyufa
na kuvuja nyakati za mvua, na kununua samani na vifaa vya ofisi kama
mashine za nukushi na za kurudufu ambazo zilikuwa hazipo,
8.
Kununua magari mapya ya ofisi ya ubalozi wetu nchini China kwa kuwa
magari matatu yaliyokuwepoyalikuwa yameshapitiliza muda wa miaka 10
ambao kwa mujibu wa sheria za China hayapaswi kutumika tena,
9.
Kupeleka mwambata wa kiuchumi (economic attaché) nchini China ili
kufuatilia fursa mbalimbali za kiuchumi katika kutekeleza diplomasia ya
uchumi kutokana na mahusiano makubwa ya kibiashara kati ya nchi yetu na
China
10.
Kuwawekea zuio wahusika wa kashfa ya rada kuwa viongozi wa shughuli za
kiserekali ili walau kuonesha uwajibikaji wa kimaadili (moral
accountability) baada ya kushindwa kuwawajibisha kisheria, ili kuondoa
dhana iliyojengeka miongoni mwa jamii kwamba dola imetekwa na mafisadi.
11.
Kuchunguza na kuwachukulia hatua watanzania (wafanyabiashara na
wanasiasa) waliotorosha kiasi kikubwa cha fedha za nchi yetu (zaidi ya
shilingi bilioni 315) na kuzificha katika mabenki ya uswisi
12. Kutoa mchanganuo wa jinsi fedha za rushwa ya rada (chenji ya rada) zilivyotumika
13.
Kueleza bayana faida za kiuchumi tunazopata kama taifa kwa kushirikiana
na jumuiya mbalimbali za kimataifa ili kuthibitisha kwamba mashirikiano
hayo hayatumiki kupora rasilimali za nchi yetu kwa hila ya “uwekezaji”
Mheshimiwa
Spika, kabla sijajielekeza kwenye mambo mahsusi kwa kipindi hiki cha
bajeti ya 2013/2014, napenda kuchukua nafasi hii kwa niaba ya Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA, kuitaka Serikali
kutoa majibu mbele ya Bunge hili tukufu, kwamba imetekeleza kwa kiwango
gani masuala yaliyoorodheshwa hapo juu, tuliyoitaka iyatekeleze (moja
baada ya jingine) kwa mwaka wa fedha unaomalizika wa 2012/2013?
1.1 Upotevu wa Fedha za Safari za Rais, Shilingi bilioni 3.5
Mheshimiwa
Spika, katika hotuba yangu ya mwaka 2012/2013 nilihoji kuhusu serikali
Kuchunguza na kuchukua hatua kwa waliohusika na upotevu wa shilingi
bilioni 3.5 kwa ajili ya safari “hewa” za Rais nje ya nchi, ili waweze
kubainika na kuchukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria zetu.
Mheshimiwa
Spika, fedha hizi ni nyingi sana na hasa ikikukumbukwa kuwa mwaka jana
2012 wapo mawaziri ambao walichukuliwa hatua na Bunge hili kutokana na
upotevu ama madhaifu yaliyofanyika kwenye wizara zao, wapo ambao
walihukumiwa kutokana na kupotea kwa Twiga kwenye wizara zao, wapo
waliohukumiwa kutokana na udhaifu katika kusimamia wizara zao na taasisi
zilizoko chini yao.
Kambi
rasmi ya upinzani, inahoji iweje leo waziri aliyeshindwa kusimamia
wizara yake na kusababisha upotevu wa fedha hizi mpaka leo bado yupo,
wakati wapo mawaziri wengine walioshughulikiwa kutokana na udhaifu
walioonyesha kwenye kusimamia wizara zao, au ndio kusema kuwa Serikali
hii ya CCM inafanya upendeleo na kuonea baadhi ya mawaziri na kuwaacha
wengine? “This clearly indicates the “double standard” nature of this
Government in the performance of its functions”
1.2. Kuanzishwa kwa Ubalozi Mdogo Guangzhou -China
Mheshimiwa
Spika, mwaka jana Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilipendekeza kuwa
serikali ianzishe ubalozi mdogo katika Jiji la Guangzhou kwa ajili ya
kurahisisha biashara kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na wale wa
China. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inatambua kuwa serikali
imelifanyia kazi wazo hili na imeamua kuanzisha ubalozi mdogo katika mji
huo ,ila tunataka kujua ni lini ubalozi huu utazinduliwa rasmi, kupata
watendaji na vitendea kazi ili uweze kuanza kufanya kazi .
2.0 DIPLOMASIA YA UCHUMI
Mheshimiwa
Spika, moja ya matarajio ya ushirikiano wa kimataifa ni kuweza
kutafuta, na kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi zinazoweza
kupatikana katika mashirikiano hayo ili kama Taifa, tuweze kujikwamua
kiuchumi na kujitegemea.
Mheshimiwa
Spika, kinyume na matarajio hayo mazuri, sasa nchi yetu imegeuzwa kuwa
kitega uchumi cha nchi zilizoendelea kwa kisingizio cha “ushirikiano wa
kimataifa” chini ya mwavuli wa “uwekezaji”. Matokeo ya ushirikiano huu
wa kinyonyaji (exploitative relationship) ni kwamba kiwango cha
umasikini katika nchi yetu kimeongezeka na hivyo kuifanya nchi yetu kuwa
tegemezi zaidi kuliko ilivyokuwa hapo kabla.
Mheshimiwa
Spika, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikerwa na unyonyaji na
unyanyasaji uliokuwa ukifanywa na wakoloni, hali iliyompelekea kusema
maneno yafuatayo:
“Tumeonewa
kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha, tumepuuzwa kiasi cha
kutosha. Unyonge wetu ndiyo uliotufanya tuonewe, tunyonywe na kupuuzwa.
Sasa tunataka kufanya mapinduzi”
Mheshimiwa
Spika, baada uhuru, Mwalimu akaanzisha siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.
Ujamaa ulilenga kujenga umoja wa kitaifa na umoja wa bara la Afrika
dhidi ya unyonyaji wa kibeberu, wakati kujitegemea kulimaanisha kujenga
uchumi endelevu ili kulijengea taifa heshima na nguvu ya maamuzi mbele
ya mataifa mengine, na kuliepusha taifa na fedheha ya kuombaomba.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imesikitishwa sana na kitendo cha
Serikali kulidanganya taifa, kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010
kwamba: “Katika kipindi cha miaka mitano 2010 -2015, Serikali ya Chama
cha Mapinduzi itatekeleza Sera ya Diplomasia ya Uchumi” wakati Ibara ya
98 (i) ya Ilani hiyohiyo ya CCM inasema kwamba Serikali ya CCM
itaendelea kushinikiza nchi tajiri kutekeleza ahadi yao ya kutenga
asilimia 0.7 ya pato la taifa la nchi zao kwa ajili ya misaada kwa nchi
masikini”.
Mheshimiwa
Spika, ikumbukwe kwamba ahadi hii ya asilimia 0.7 ya pato la taifa la
nchi tajiri ambayo Serikali ya CCM inakodolea macho ni fedha za walipa
kodi wa nchi hizo kama ambavyo wananchi wetu wanavyolipa kodi. Aidha ni
aibu kwa Serikali hii ya CCM kuchukua ahadi za wahisani na kuziweka
kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM kama ahadi kwa wananchi ili kubembelezea
kura.
Mheshimiwa
Spika, kutokana na uvivu wa kufikiri na kubuni mbinu za kuikwamua nchi
hii na umasikini, Serikali hii ya CCM sasa hivi imeachana kabisa na sera
ya kujitegemea, ambayo Mwalimu kupitia Azimio la Arusha alisema kwamba “
… Hakika ni ujinga na upumbavu zaidi kwetu sisi, kufikiri kwamba
tutaondokana na umasikini wetu kwa misaada ya fedha kutoka nje kuliko
rasilimali zetu wenyewe”
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza bunge hili,
kama inatekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa kutegemea ahadi ya misaada ya
fedha kutoka kwa wahisani na kama hilo ndio suluhisho la matatizo
yanayokumba uchumi wetu kama taifa kwamba tutaweza kuendelea kwa
kutegemea hisani na fadhila za wafadhili huku tukishindwa kuzitumia
rasilimali zetu kwa ajili ya kujikomboa kiuchumi.
Aidha,
Kambi Rasmi ya Upinzani imejiridhisha kwamba kauli mbiu ya ‘Diplomasia
ya Uchumi’ imeendelea kubakia kama ilivyo kauli mbiu ya ‘Kilimo Kwanza’
ambayo imebakia kutamkwa na viongozi bila kuwa na mkakati wa utekelezaji
wala vigezo vya kupima kiwango cha utekelezaji wake.
3.0. VYAMA VYA SIASA NA MISAADA KUTOKA NJE YA NCHI.
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa ‘United
Nations University’(UNU-WIDER) ya mwezi Aprili 2012 iliyoandaliwa na
Aili Mari Tripp ilionyesha kuwa misaada ya wahisani kutoka nje katika
mabadiliko ya kisiasa Tanzania ‘Donor Assistance and Political Reform in
Tanzania’, inaonyesha kuwa Tanzania imepokea misaada kutoka nje yenye
thamani ya dola za kimarekani bilioni 26.85 toka mwaka 1990-2010.
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa ripoti hiyo ni kuwa Tanzania ni nchi inayoongoza
kusini mwa jangwa la Sahara kwa kupokea misaada mingi kutoka nje ya nchi
na hasa kutoka mataifa ya Ulaya na taasisi za nchi za Uingereza,
Marekani, Ujerumani, Uholanzi, Norway, Canada, Sweden, na taasisi kama
Benki ya Dunia, IMF ,UNDP ,UNICEF na mengineyo.
Pamoja
na misaada yote hiyo, bado tumeendelea kuwa nchi maskini sana duniani
pamoja na kuwa na rasilimali lukuki ambazo tumepewa na Mungu ila
tunashindwa kuzitumia kwa manufaa ya watanzania na badala yake
tumeendelea kudanganywa na vimisaada vidogo vidogo na kubadilishana na
rasilimali zetu kama madini, misitu ,wanyama nk kwa ajili ya misaada
hiyo.
Mheshimiwa
Spika, pamoja na misaada hiyo kwa serikali hii ya CCM bado vyama vya
siasa vimekuwa na mahusiano na baadhi ya vyama vingine vya siasa katika
mataifa ya magharibi na vimekuwa vikipokea misaada ya aina mbalimbali
kama fedha , nyenzo na mengineyo kadiri ya makubaliano na mirengo ya
kiitikadi ya vyama husika.Pamoja na ukweli huo bado vipo vyama vya siasa
vinavyopotosha umma kuhusiana na misaada vinayopokea kutoka nje ya nchi
na vyama hivi vimekuwa mstari wa mbele kueneza propaganda za uongo kuwa
vyenyewe havipokei misaada kutoka nchi za magharibi.
Mheshimiwa
Spika, CCM wao ‘wanajiita’ kuwa wapo mrengo wa kijamaa/kikomunisti na
wamekuwa wakipokea misaada mingi sana ya fedha na nyenzo kutoka Umoja wa
Vyama vya Kikomunisti Ulimwenguni ‘Socialist International’ kutoka
katika nchi kama za Ujerumani kupitia SDP ,Uingereza kupitia chama cha
Labour,China kupitia chama cha Kikomunist ,Marekani kupitia chama cha
Democrats. Pamoja na misaada ya kifedha na kiufundi ambayo CCM imekuwa
ikipata kutoka nje wamekuwa hawatangazi hadharani hata mara moja
kuhusiana na kiasi ambacho wamekuwa wakipokea na hivyo kila kitu kwao
imekuwa ni siri kuu ya viongozi wao.
Mheshimiwa
Spika, kwa upande wa chama cha CUF, kutokana na itikadi zake za mrengo
wa Kiliberali ambazo miongoni mwa misingi yake mikuu ni pamoja na
“kupigania haki za ndoa ya jinsia moja, usagaji na ushoga”. Hii ni kwa
mujibu wa tangazo lao kwenye mtandao wao wa umoja wa maliberali
ulimwenguni, likiungwa mkono na Waziri wa Haki na Usawa wa Uingereza,
Lynn Featherstone kutoka chama cha Liberal Democrats wakati chama hicho(www.liberal-international.org)
kilipokuwa kinapitisha azimio la kuruhusu ndoa za jinsia moja kama haki
ya mtu mmoja mmoja, wanashirikiana na vyama kama vile LPC ya Canada,
Det Radikale Venstre cha Norway, FDP cha Ujerumani, Israel Liberal Group
cha Israel,PDS cha Senegal na Liberal Democrats cha Uingereza.
Kutokana
na umoja huo, CUF wamekuwa wakipata msaada wa kifedha na nyenzo
nyingine mbalimbali kutoka kwa vyama hivyo vya mrengo wa Kiliberali na
msaada wa mwisho ni hivi majuzi mwezi Machi 2013 waliposaini makubaliano
na chama cha Kiliberali kutoka Norway.
Mheshimiwa
Spika, kwa upande wa CHADEMA, wapo kwenye Umoja wa Vyama vya
Kidemokrasia Ulimwenguni (International Democratic Union - IDU). Huu ni
umoja wa vyama ambavyo vipo kwenye mrengo wa kati na ambavyo msingi wake
mkuu ni pamoja na kuwa na familia, kama taasisi muhimu katika jamii,
ikimaanisha kwamba: “tunapinga vitendo vyote vya ushoga na usagaji”.
Tunatetea demokrasia, haki za binadamu na kupambana na ufisadi katika
serikali. Vyama wanachama wa umoja huu ni pamoja na Conservative Party
cha UK, CPP cha Norway, Republican cha Marekani na vingine vinavyofuata
mrengo huo.
Mheshimiwa
Spika, Kambi rasmi ya upinzani Bungeni, inavitaka vyama vyote ambavyo
vimekuwa na mahusiano na vyama vya nje viweke wazi mikataba yao na
malengo ya mahusiano hayo ikiwa ni pamoja na misaada ambayo vimekuwa
vikipokea kutoka kwenye nchi hizo .
4.0 MPANGO WA KUJITATHIMINI KIUTAWALA BORA (APRM)
Mheshimiwa
Spika, itakumbukwa kuwa mnamo mwezi Januari, 2013 ulifanyika mkutano wa
20 wa wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa
,Ethiopia na ni katika mkutano huo Mhe. Rais Kikwete aliwasilisha
taarifa ya nchi yetu kuhusu kujitathimini katika utawala bora kwenye
mpango wa nchi zinazojitathimini katika utawala bora (APRM).
Mheshimiwa Spika, baada ya taarifa hiyo (randama uk.15) nchi yetu ilitakiwa kutafutia ufumbuzi changamoto zifuatazo;
i. Migogoro baina ya wakulima na wafugaji
ii. Imani za kishirikiana (uchawi)
iii. Kuhakikisha kuwa manufaa ya kukua kwa uchumi yanawafikia wananchi
iv. Kutoa elimu kwa umma kuhusu mipango na sera za serikali
Mheshimiwa
Spika, changamoto hizi ambazo nyingine zinatia aibu taifa letu mbele ya
mataifa mengine kama vile sisi kuonekana ni wachawi na hivyo kutakiwa
kuchukua hatua dhidi ya uchawi !ni fedheha na aibu kubwa kwa taifa letu .
Aidha
, Kambi rasmi ya upinzani Bungeni inataka kujua serikali na wizara
imechukua hatua gani mpaka sasa katika kukabiliana na changamoto hizi na
hasa tatizo la wakulima na wafugaji na kuhakikisha kuwa manufaa ya
kukua kwa uchumi wetu yanawanufaisha wananchi na sio kuwanufaisha baadhi
ya viongozi na mafisadi wachache.
5.0 MLIPUKO WA BOMU ARUSHA NA BARAZA LA USALAMA LA UMOJA WA MATAIFA.
Mheshimiwa
Spika, mwaka huu tarehe 05 Mei, Kanisa Katoliki Parokia ya Olasiti huko
Arusha lililipuliwa kwa bomu. Tukio hili lilitokea wakati akiwepo
balozi wa Vatican Nchini na ambaye ndio alikuwa mgeni wa heshima kwenye
tukio la kuzindua Parokia hiyo.
Mheshimiwa
Spika, mara baada ya tukio hilo, Balozi wa Vatican nchini aliwasilisha
taarifa hiyo kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuonyesha
kuwa Tanzania sio nchi salama sana kutembelewa na wageni na kama
wakitembelea basi wanapaswa kuchukua tahadhari kubwa kwa kipindi chote
watakapokuwa hapa nchini.
Mheshimiwa
Spika, Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kujua nini kauli ya
serikali kuhusiana na tukio hili na hasa kuhusiana na taarifa za hali ya
usalama wa nchi yetu na wageni zilizowasilishwa kwenye Baraza la
usalama la Umoja wa Mataifa .
6.0 SAFARI ZA VIONGOZI NJE NA MISAFARA MIKUBWA
Mheshimiwa
Spika, tangu mwaka 2011/2012 Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa
ikihoji suala la misafara ya Viongozi wa kitaifa kuwa mikubwa kutokana
na kuambatana na watu wengi ambao wengine wanakuwa hawana hata majukumu
ya msingi ya kufanya wakati wa ziara hizo huku wakiliongezea taifa
gharama kubwa ya kuwasafirisha na na kulipia malazi yao na starehe zao.
Aidha
, tumekuwa tukipendekeza na kushauri kuwa sasa ni wakati muafaka kwa
Rais wa nchi kuamua kutuma wasaidizi wake kwenye baadhi ya ziara za nje
kama wanavyofanya viongozi wengine wa nchi jirani kama Rais Kagame wa
Rwanda na hata Mwai Kibaki, Rais mstaafu wa Kenya alivyokuwa anafanya
akiwa Rais, kwani kwa kufanya hivyo atapunguza msururu wa maafisa na
viongozi mbalimbali wa kuambatana naye. Tunashauri tena kuwa rais awe
anatuma wasaidizi wake kwenye ziara za kawaida na yeye awe na jukumu la
kushiriki kwenye ziara rasmi za kiserikali ‘State Visits’ na mikutano
maalum ya Kimataifa kama UN na AU.
Hivyo
basi Kambi rasmi ya Upinzani inashauri mambo yafuatayo yafanyike ili
kupunguza gharama hizi kubwa za kuwasafirisha viongozi na misafara
isiyokuwa na tija kama ifuatavyo;
i.
Serikali itengeneze kanuni za kuthibiti idadi ya maafisa na watu ambao
watakuwa wakiambatana na Rais kwenye ziara za nje (idadi ya wajumbe
kwenye misafara iwe wazi na ijulikane)
ii.
Pawepo na kanuni za kuainisha kuwa ni nani watapaswa kupanda ndege
daraja la kwanza na wale wenye haki ya kulala kwenye hoteli za daraja la
kwanza wajulikane.
6.1. Idara ya Protocol na Mabilioni ya Fedha za Safari za Nje.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2011/2012 fungu 221100 ‘travel out of
country’zilitumika shilingi 36,121,942,870.00 kwa ajili ya safari za nje
ya nchi kwa viongozi wakuu. Katika mwaka wa fedha uliopita wa 2012/2013
kifungu 1010 ambacho ni kwa ajili ya protocol walitengewa shilingi
8,372,581,824 na fedha ambazo zilikuwa zimepokelewa na wizara mpaka
mwezi Februari 2013 zilikuwa jumla ya shilingi 26,081,860,727.16!
(randama uk.4)jedwali la 2 na zilitumika kwa ajili ya kugharamia safari
za viongozi nje ya nchi.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013 Bunge lilikuwa limetenga na
kuidhinisha kiasi cha shilingi 8,372,581,824 kwa ajili ya kifungu hiki
cha Protocol ‘travel out of Country’kwa mujibu wa kitabu cha matumizi ya
kawaida juzuu ya pili (volume II). Jambo la kushangaza ni kwamba,
wizara iliieleza kamati na Bunge hili kuwa walishatumia zaidi ya bilioni
26.081 kutokana na fedha walizokuwa wamejitengea wenyewe wizara ambazo
hazikuidhinishwa na Bunge kiasi cha bilioni 29.404
Mheshimiwa
Spika, Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA, inataka
maelezo ya kina kuhusiana na mamlaka ya wizara hii kwenda kutenga na
kutumia fedha nyingi kuliko zilizokuwa zimeidhinishwa na Bunge hili na
zilikuwa fedha kwa ajili ya safari za kwenda nje ya nchi, ni nani aliipa
wizara mamlaka hiyo na kiburi hicho kiasi cha kupuuza maamuzi ya Bunge
hili tukufu.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka huu wa fedha 2013/2014 kitengo hiki cha Protocol
kimetengewa jumla ya shilingi 15,155,377,400.00 kwa ajili ya matumizi
mengineyo ,ambazo katika mchanganuo wake kwenye kifungu 1010 kifungu
kidogo cha 221100 ‘travel out of Country’ zimetengwa shilingi
9,381,328,850.00 kwa ajili ya kugharamia safari za kikazi za viongozi wa
Kitaifa nje ya nchi.
Aidha,
katika kifungu kidogo cha 220700 ‘rental expenses’ zimeombwa jumla ya
shilingi 2,925,445,000.00 kwa ajili ya kukodisha ndege ,magari na kumbi
za mikutano kwa ajili ya viongozi wa kitaifa.
Kambi
rasmi ya Upinzani Bungeni, haikubaliani na kamwe haitakubaliana na
ufujaji huu wa fedha za walipakodi maskini wa Tanzania . Tunamtaka
waziri atoe maelezo ya kina kwa watanzania ni kwanini nchi maskini kama
yetu tutumie fedha nyingi kiasi hicho kwa ajili ya safari za viongozi
nje ya nchi? Aidha , hatukubaliani na kitendo cha kutenga fedha kwa
ajili ya kukodi ndege wakati Rais ana ndege yake ambayo ilinunuliwa na
mabilioni ya fedha za watanzania.
Ikumbukwe
kwamba ndege hii ya Rais ilinunuliwa kwa mbwembwe nyingi kiasi kwamba
Waziri wa Fedha wa wakati huo Ndugu Bazili Mramba alisema watanzania
wafunge mkanda, hata kama watakula majani, lazima ndege ya Rais
inunuliwe. Watanzania hawa wamekula majani sasa kiasi cha kutosha, bado
tena Serikali inaendelea kuwanyonya ili ipate pesa za kukodisha ndege
wakati Rais ana ndege? Hivi Serikali sasa inataka watanzania wale mawe
ndio ijue kwamba watu wamefunga mkanda kiasi cha kutosha?
6.2 Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje
Mheshimiwa
Spika, mwaka 2012 Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje Ulinzi na
Usalama, ilifanya ziara kwenye balozi takribani zote na iliona matatizo
yanayozikumba balozi zetu huko na ilikuwa matumaini yetu kuwa baada, ya
ziara ile ya kamati ingehakikisha kuwa fedha zinaongezwa kwenye wizara
hii na hasa kwenye fungu la maendeleo ili tuweze kuboresha mazingira ya
balozi zetu. Kinyume na matumaini hayo, ni kwamba hakuna jitihada
zilizofanyika kuongoeza bajeti ya wizara hasa katika fedha za
maeendeleo.
Mheshimimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka kamati ya Bunge ya
Ulinzi na usalama, kuishinikiza Serikali ili kuhakikisha kuwa katika
mwaka huu wa fedha wizara hii inaongezewa fedha kwa ajili ya kuboresha
mazingira ya balozi zetu , na hiyo ndio njia pekee ya kuonyesha kuwa
kamati haikuenda kufanya utalii bali ilienda kuona matatizo ya balozi
zetu na kuchukua hatua.
7.0 UFISADI KATIKA UNUNUZI WA JENGO LA OFISI NA MAKAZI KATIKA UBALOZI WA TANZANIA JIJINI PARIS – UFARANSA.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka huu wa fedha kwa mujibu wa randama ya wizara ni
kuwa mwaka huu wa fedha kiasi cha shilingi bilioni 28
(28,000,000,000.00) zimepangwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo na
kati ya hizo kiasi cha shilingi bilioni 24 na milioni 188
(24,188,000,000.00) ni kwa ajili ya ununuzi wa jengo la ofisi na makazi
ya balozi jijini Paris ,Ufaransa (randama uk 25) na kiasi cha shilingi
bilioni 3 na milioni 812 (3,812,000,000.00) ni kwa ajili ya gharama za
ukarabati wa majengo ya ofisi na makazi yaliyopo Ubalozi wa Tanzania
Maputo,Msumbiji.
Mheshimiwa
Spika, ukisoma randama ya wizara (uk.120) katika kasma 6391 ,kifungu
kidogo 411100 kiasi cha fedha kilichoombwa ni shilingi bilioni 23 na
milioni 900 (23,900,000,000) kwa ajili ya ununuzi wa jengo la ofisi na
makazi ya Balozi jijini Paris, Ufaransa na shilingi bilioni 3 namilioni
700 (3,700,000,000.00) kinaombwa kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya
ofisi na makazi yaliyopo ubalozi wa Tanzania Maputo,Msumbiji.
Hata
hivyo, katika mwaka huu wa fedha 2013/2014 kwenye kasma 6391 katika
fungu la Maendeleo (randama uk.120) wizara inaomba kutengewa kiasi cha
shilingi milioni 400 (400,000,000.00) (kifungu 221100 ) fedha ambazo
hazipo kwenye kitabu cha matumizi ya kawaida juzuu ya pili (volume II)
kwa ajili ya posho ya kujikimu na gharama za usafiri kwa ajili ya
kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Wizara, miradi yenyewe
ni miwili mmoja wa kununua nyumba Ufaransa na kukarabati jengo Msumbiji.
Mheshimiwa
Spika, mkanganyiko huu wa kimahesabu unatia mashaka makubwa sana
kuhusiana na dhamira ya serikali na wizara hii hasa fedha zinapotengwa
bila kufuata utaratibu wa kibajeti na bila kuingizwa kwenye vitabu vya
fedha na mafungu husika.
Kambi
rasmi ya Upinzani, inajiuliza tunapitisha mafungu yapi? Kwani kwenye
randama fedha zinatofautiana kwenye fungu moja la maendeleo baina ya
(ukurasa 25 na 120) , vilevile kwenye kitabu cha matumizi ya kawaida
hali ni tofauti kwenye fungu la travel out of the Country kwani sasa
wizara imejiongezea shilingi milioni mia nne kwa ajili ya kufuatilia
miradi miwili ambayo ni kununua jengo Paris na kukarabati Jengo la
ubalozi - Maputo,Msumbiji.
Mheshimiwa
Spika, utata wa fedha unaendelea kuonekana kwenye randama ya wizara
katika kiambatanisho Na.1 ‘utekelezaji wa ushauri na mapendekezo ya
kamati ya kudumu ya Bunge ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa’
katika ushauri/mapendekezo Na.5 kamati iliitaka ‘Wizara itoe mchanganuo
wa matumizi ya fedha za bajeti ya maendeleo zilizopokelewa kutoka hazina
katika mwaka wa fedha 2012/13’
Maelezo
ya wizara yalikuwa kama ifuatavyo; nanukuu randama ya wizara “katika
mwaka wa fedha 2012/2013 ,hadi kufikia mwezi Machi ,2013 wizara imepokea
kutoka Hazina kiasi cha shilingi 13,261,281,600.00 ambapo kati ya fedha
hizo kiasi cha shilingi 9,660,000,000.00 zimetumika kwa ajili ya
kulipia malipo ya awali ya ununuzi wa Jengo la Ofisi na Makazi ya Balozi
Paris,Ufaransa;shilingi 995,930,000.00 zimetumika kwa ajili ya
ukarabati wa jengo la serikali lililopo Maputo,Msumbiji ;shilingi
626,899,155.00 zimetumika kwa ajili ya ukomboaji wa vifaa vya ujenzi
bandarini vilivyotumika katika ujenzi wa kituo cha mikutano cha
kimataifa cha Julius Nyerere na safari ya kikazi ya wataalam katika
balozi za Maputo,Pretoria na Lusaka kwa ajili ya kazi ya upembuzi
yakinifu wa miradi ya maendeleo iliyopo katika Balozi hizo; na shilingi
1,978,452,485.20 bado hazijatumika na zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya
kulipia gharama za ukarabati wa jengo la Serikali lililopo Maputo’
Mheshimiwa
Spika, baada ya kufuatilia na kufanya tathimini ya kina kuhusiana na
majibu hayo ya wizara kuhusu fedha za maendeleo kwa ajili ya ukarabati
wa Jengo la Maputo na kununua Jengo la Ofisi na Makazi ya Balozi
Ufaransa na kukuta kuwa ni fedha nyingi sana kuliko uhalisia wenyewe ,
kwa mfano waziri anataka Bunge na taifa tuamini kuwa kufanya ukarabati
wa jengo moja la ofisi Maputo Msumbiji tunahitaji kutumia kiasi cha
shilingi 4,695,930,000.00 kwa kutumia fedha inayoombwa mwaka huu wa
fedha na zile ambazo tayari zilishalipwa katika mwaka wa fedha wa
2012/2013.
Aidha
wakati wizara inawasilisha majibu yake kwenye kamati ya kudumu ya Bunge
walisema kuwa (swali 12 uk.5) ‘kiasi cha fedha kilichotengwa kwa ajili
ya ukarabati wa majengo ya Serikali yaliyopo Maputo ni shilingi
3,812,000,000.00……kiasi hicho cha fedha kinatosheleza kukamilisha kazi
ya ukarabati wa majengo hayo ya Serikali yaliyopo Maputo, Msumbiji’
Aidha,
kununua jengo moja la ofisi na makazi katika Jiji la Paris Ufaransa
tunahitaji kutumia kiasi cha shilingi bilioni 33 na milioni 560
33,560,000,000.00.
Mheshimiwa
Spika, kwa majibu haya ya wizara ni kuwa tayari wizara imeshafanya
malipo ya shilingi bilioni 9.66 kama malipo ya awali kwa ajili ya
ununuzi wa jengo la ofisi na makazi huko Paris Ufaransa , na kuwa tayari
tumeshafanya malipo ya awali kiasi cha shilingi milioni 995.930 kwa
ajili ya ukarabati wa jengo la ubalozi huko Maputo,Msumbiji.
Mheshimiwa
Spika, hakika kiasi hiki ni kikubwa kupitiliza na hata utafiti na
tathimini ambayo ilifanywa na Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni ilionyesha
kuwa kununua jengo la ofisi katika jiji la Paris kwenye mji wa bei
ghali kama Co’te d’Azur (most expensive area in Paris) huwezi kutumia
fedha nyingi kiasi hicho kwa ajili ya manunuzi ya jengo la ofisi na
makazi.
Aidha,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tunakumbuka sakata la ununuzi wa jengo
la ubalozi lililomkumba balozi Prof.Mahalu huko Roma - Italia na
yaliyofuatia mpaka kesi na fedha zetu tulizoambiwa kuwa zimepotea
hazikuweza kurejeshwa baada ya Prof.Mahalu kushinda kesi hiyo
mahakamani.
Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kupata majibu kuhusiana na mambo yafuatayo;
i.
Ni eneo gani ambalo tumepata jengo la kununua kwa ajili ya ubalozi na
makazi ya balozi huko Paris, Ufaransa, na ni nyumba ya aina gani .
ii.
Je, Serikali inaweza kuonyesha mkataba wa manunuzi wa nyumba hizo
(Paris) kwa Bunge na tutalipa kiasi gani kununua jengo hilo?
iii. Ni nani au wakala gani wa serikali aliyefanya tathimini ya hayo majengo na kuamua kuwa tulipe kiasi hicho cha fedha?
iv. Ni kampuni gani iliyohusika katika kufanya makubaliano ya mauziano ya nyumba hizo na tunawalipa kamisheni ya shilingi ngapi?
v.
Nani, aliidhinisha kutumika kwa kiasi kikubwa hivyo kwa ajili ya
kununua jengo la Ubalozi na makazi huko Paris, je Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Mambo ya Nje, ilishirikishwa katika manunuzi haya?
vi. Ukarabati unaofanywa kwenye jengo la Maputo Msumbiji ni wa aina gani, au tunajenga upya nyumba hizo?
vii.
Ni kampuni gani ya ujenzi inayofanya ukarabati wa jengo letu huko
Msumbiji na mkataba wa ukarabati huo uko wapi, tungetaka uwekwe
hadharani.
Aidha
, kambi rasmi ya Upinzani Bungeni , inatoa hoja ya kumtaka Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya uchunguzi maalum
(Special Audit) kuhusiana na ununuzi wa majengo haya na ukarabati
unaofanyika kwenye jengo letu huko Maputo, Msumbiji, na kuona kama
thamani halisi ya fedha imezingatiwa , na kama sheria ya manunuzi ya
umma imefuatwa kikamilifu.
Mheshimiwa
Spika, Vile vile, tungetaka sehemu ya fedha hizi zitumike kwa ajili ya
kukarabati jengo letu la zamani la ubalozi lililopo Washngton ambalo kwa
sasa halitumiki baada ya kutekelezwa kwani likikarabatiwa litaweza
kuliongezea taifa mapato kutokana na matumizi ya kibiashara ya jengo
hilo.
8.0 MPANGO WA WIZARA WA KUTOA VISA KWENYE BALOZI TU
Mheshimiwa
Spika, mpango wa Wizara kutoa visa kwenye balozi tu haukubaliki. Kwa
Mujibu wa majibu ya wizara kwenye kamati ya kudumu ya Bunge ya Mambo ya
nje na ushirikiano wa kimataifa ilionyesha kuwa ili wizara iweze
kukusanya fedha za kutosha kwenye balozi zetu ni kwa kurudisha utaratibu
wa utoaji wa viza kufanywa na Balozi zetu tofauti na utaratibu
unaotumika hivi sasa ambapo wageni huweza kupatiwa viza pindi
wanapowasili katika vituo vya kuingilia nchini (viza on arrival).
Kambi
rasmi ya Upinzani Bungeni, haikubaliani na wazo hili la wizara kwani
badala ya kuongeza wageni kuja nchini litapunguza sana hasa ikizingatiwa
kuwa ni nchi chache sana ambako tuna ofisi za Balozi na pia kuna nchi
nyingine kama Marekani ambapo, kama mgeni yupo Carlifonia na anataka
kusafiri kuja Tanzania atalazimika kwanza kusafiri kwenda Washington
ambako ndiko kwenye ubalozi atafute visa na ndipo aweze kuja nchini.
Utaratibu huu utaongeza gharama kubwa za usafiri kwa wageni na watalii
na hivyo kulipotezea taifa mapato yataokanayo na utalii kwani wageni
watapungua.
Aidha,
tunaikumbusha wizara kuhusiana na Itifaki ya kuwa na“Single Tourist
Destination Protocol” na uwepo wa hati ya kusafiria na visa moja ya
utalii “Single Tourist Visas” kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki, hivyo kama sisi tukifanya huo uamuzi basi wenzetu Kenya
wataendelea kupata wageni wengi zaidi kutokana na visa ya pamoja na
wageni wataingia Tanzania kutokana na visa za Kenya chini ya Itifaki
hiyo.
8.1 Mkutano wa Mabalozi wa Mwaka 2013/2014
Mheshimiwa
Spika, wizara inahitaji kiasi cha shilingi bilioni 1 kwa ajili ya
kufanikisha mkutano wa mabalozi kwa mwaka wa fedha 2013/2014 , na wizara
iliwasilisha maombi ya fedha hizo Hazina kama sehemu ya kipaumbele
lakini hazikuweza kupatikana .
Kambi
rasmi ya upinzani Bungeni, inaitaka serikali kuiondoa aibu hii na
kutenga hizo fedha kwa ajili ya kufanikisha mkutano huo na tunapendekeza
kuwa katika fungu la protocol safari za nje ndipo fedha hizo zipunguzwe
na kutumika kwa ajili ya mkutano wa mabalozi wetu ili waweze kupeana
ushauri na uzoefu,ili kuboresha ufanisi wa majukumu yao.
8.2 Utaratibu wa Kupeleka Fedha kwenye Balozi
Mheshimiwa
Spika, kutokana na utaratibu wa kupeleka fedha kwenye balozi zetu kuwa
na mlolongo mrefu wa kwanza kutoka Hazina na kupelekwa Wizarani, ndipo
wizara isambaze fedha hizo kwenye balozi zetu mbalimbali umesababisha
fedha kuchelewa kufikishwa kwa wakati kwenye balozi zetu na hivyo
kusababisha usumbufu mkubwa na ucheleweshaji wa kazi kwenye balozi zetu.
Kambi
rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka serikali kubadilisha utaratibu huu
na hazina iwe inapeleka fedha hizo moja kwa moja kwenye balozi husika
badala ya kuzipitisha wizarani kama ilivyofanya kwenye fedha za
Halimashauri mbalimbali nchini ili kupunguza usumbufu huo.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya kambi rasmi ya Upinzani naomba kuwasilisha.
______________________________ __
Ezekiah Dibogo Wenje
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
NA
WAZIRI KIVULI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
CHANZO JAMII FORAM
CHANZO JAMII FORAM
No comments:
Post a Comment