Thursday, May 16, 2013

CCM YAWAPONGEZA VIONGOZI WA DINI


   Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi iliyokutana jana Mjini Dodoma imeipongeza serikali kwa hatua inayoendelea kuchukua katika kuchunguza chanzo cha tukio la mlipuko wa Bomu uliotokea Kanisani Jijini Arusha.
Bomu hilo lilirushwa Mei Tano mwaka huu wakati wa uzinduzi wa Kanisa la Romani Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Parokia ya Olisiti na kusababisha vifo vya watu watatu na majeruhi kadhaa.
Akizungumza leo Jijini Dar es salaam Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi NAPE NNAUYE ameeleza kuwa taarifa hiyo ya serikali iliwasilishwa jana katika kikao hicho na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dokta EMMANUEL NCHIMBI .
Kufuatia tukio hilo, Kamati Kuu imelaani na imeitaka serikali kuharakisha uchunguzi pamoja na kuongeza kasi ya uchunguzi wa suala hilo sanjari na kutafuta mzizi wa matukio hayo pamoja na kutoa taarifa mara kwa mara kuhusu maendeleo ya uchunguzi wa tukio hilo.

Hata hivyo Kamati Kuu imewapongeza viongozi wa Madhehebu ya Dini nchini kwa kuweza kuwaelekeza waumini wao kuhusu mlipuko huo na kuweza kusimamia amani na utulivu tangu kutokea kwa tukio hilo.
Pia Kamati Kuu imewataka viongozi wa kisiasa nchini kuliachia Jeshi la Polisi liendelee na kazi ya upelelezi wa tukio hilo.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi-CCM, Rais JAKAYA KIKWETE wiki ijayo anatarajia kukutana na Wabunge wote wa CCM Mjini Dodoma katika kikao cha kazi. Kikao hicho kitakuwa ni cha siku Mbili kuanzia Mei 18 na 19 mwaka huu. Katika kikao hicho, Wabunge watatumia fursa hiyo kutoa maoni yao kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010/2015 katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika Majimbo yao ya Uchaguzi.
NAPE amefafanua kuwa Chama Cha Mapinduzi kimekuwa na utaratibu wa kukutana na Wabunge wa Chama hicho ili kujadili masuala yanayohusu nchi likiwemo suala la utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ambalo ndio Dira ya maendeleo ya wananchi.
Pia amesisitiza kuwa kuitishwa kwa kikao hicho hakuna uhusiano na suala la aina yoyote ya kuwawajibisha Wabunge wa CCM kinidhamu bali ni mkutano wa kawaida na wa kazi.
Mara baada ya kikao hicho cha Wabunge wa CCM, Kamati Kuu ya CCM itakutana kwa siku Mbili Mjini Dodoma kuanzia Mei 20 hadi 21 mwaka huu.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...