RAIS
Jakaya Kikwete
amezipiga ‘kijembe’ klabu kongwe hapa nchini, Simba na Yanga, kutokuwa
na maendeleo kisoka na kuiacha Azam FC, ikiwapiga kumbo kila idara huku
wao wakiendekeza ushirikina mbele na migogoro.
Kikwete aliyasema hayo jana,
wakati akiweka jiwe la msingi la klabu ya Azam iliyoko Chamazi nje
kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Rais
aliipongeza Azam kwa hatua ambayo imefikia, licha ya kuwa na uchanga
katika soka na kuzipita klabu za Simba na Yanga.
Alisema endapo Azam inataka kupiga hatua na
kuifikisha nchi mbali kwa kulitangaza jina la Tanzania, ifanye mambo
yake bila kuzifuata timu kongwe na kudai kuwa itafika mbali kitaifa na
kimataifa pia.
“Naamini mna uwezo wa kufika mbali katika
ulimwengu
wa soka, ila msiwe karibu na hizi timu, mtajikuta mnaishia hapahapa;
wao mechi mechi moja wanatolewa,” alisema Kikwete na kuwafanya watu
walioshuhudia hafla hiyo kuvunjika mbavu.
Aidha Kikwete alisema
kutokana na mafanikio ambayo Azam wameyapata hadi sasa, ikiwemo uwanja
na mambo mengine, imeonekana kama wao ndio vigogo na kusababisha
kuogopwa na jamaa ambao wanajifanya wakubwa.
Alikwenda mbali zaidi na kuwataka Azam, kuacha
kufuata vivuli vya hizo timu na kujisimamia wenyewe, kwa kuwa timu
mbili kongwe zina wanachama wanaopiga kura kwa kuhongwa, sambamba na
kutumia muda mwingi kulumbana, wakati hawana kitu wanachoingiza katika
timu.
Alisema
timu kubwa
zikiambiwa kutumia Uwanja wa Chamazi, zinaanza kuleta maneno ya ajabu
na kuongeza kuwa ushirikina haufai katika soka, cha muhimu ni kucheza
mpira na sio kazi ya kuandaa kamati za ufundi na kushindwa kutazama
benchi la ufundi ili kujenga timu.
“Ingekuwa mpira ni
ushirikina, basi Afrika tungekuwa mabingwa kila mwaka, kama timu inaona
uchawi dili, basi ikusanye wachawi wote dunia nzima ikae nao klabuni
kwao tuone!” aliongeza Kikwete.
Aliwataka
Azam endapo watakuwa na shida yoyote, wasisite kumjulisha na kudai
kuwa ombi lao la kupunguziwa VAT katika bidhaa zao za kisoka,
atawasiliana na wahusika ili aweze kulipatia ufumbuzi.
Naye Mkurugenzi wa Azam,
Yusuph Bakhressa, alishukuru sana kupata nafasi ya Rais kuzindua mradi
wao maalumu, ambao lengo lake ni kukuza na kuendeleza mpira wa miguu
nchini.
Alisema hadi sasa wametumia sh bilioni 3 katika mradi huo.
Katika hafla hiyo, Rais
aliambatana na mkewe Mama Salma Kikwete, Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, Mkuu wa Mkoa Dar es
Salaam, Mecky Saidi Sadick, na viongozi mbalimbali.
No comments:
Post a Comment