Siku mbili baada ya Rais wa Sudan
kuiomba Marekani kumpa Visa ya kusafiri nchini humo kuhudhuria mkutano
wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, wito umetolewa kwa
taifa hilo kumkamata Bashir na kumkamabidhi kwa mahakama ya ICC.
Mkutano huo utafanyika wiki ijayo.
Ombi hilo limetolewa na ICC kwa
Marekani na kuitaka impe Visa Bashir na kisha kumkamata na kumkabidhi
kwa mahakama hiyo pindi tu atakapotua nchini humo.
Bashir anatakikana na mahakama ya ICC
kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya binadamu na pia kuamuru mauaji ya halaiki
katika jimbo la Darfur.
Marekani ilisema kuwa ilipokea ombi la
Bashir kutaka Visa na kulitaja ombi hilo kama la kuudhi na kejeli kubwa
kwa taifa hilo. Ilimtaka Bashir kwanza kujikabidhi kwa mahakamya ICC
kabla ya kutaka kuingia Marekani.
Hata hivyo Marekani sio mwanachama wa
mahakama ya ICC na kwa hivyo , kisheria sio lazima itimize matakwa ya
mahakama hiyo juu ya Bashir.
Marekani imekuwa katika msitari wa
mbele kutaka Bashir akamatwe kwa madai ya uhalifu dhidi yake ili
akabiliwa na sheria za kimataifa
Shirika la habari la Reuters lilisema
kua mahakama imeshauri Marekani kumkamata Bashir na kumkabidhi kwa ICC
ikiwa ataingia nchini humo.
Vibali viwili vya kumkamata Bashir vilitolewa mwaka 2009 na 2010 kwa madai ya uhalifu dhidi ya binadamu.
Hata hivyo Sudan imepuuza hatua ya ICC
kumtaka Bashir kwa makosa ya Darfur wakisema kuwa madai hayo
yameongezwa chumvi, na nchi hiyo imekataa kuitambua mahakama hiyo
ikisema kuwa ni sehemu ya njama ya nchi za magharibi dhidi ya Afrika.