Rais Jakaya Kikwete
*Asema hatawatetea wauza ‘unga’*Ashangazwa na kiwango cha uongo
RAIS Jakaya Kikwete, amesema anashangazwa na kiwango cha uongo cha baadhi ya wanasiasa ambao hakuwataja majina, kuwa wamekuwa wakizusha madai kuwa Rais aliteua wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, bila kuongozwa na mapendekezo ya wadau mbalimbali waliopendekeza majina hayo. Alisema bado anaendelea kuamini mchakato wa Katiba mpya utafikia mwisho wake mwaka 2014 na hivyo kuiwezesha Tanzania kufanya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, chini ya Katiba mpya.
Alisema hana tatizo na watu wanaopinga sera za serikali ama hata kumpinga yeye binafsi, bali tatizo lake ni wanasiasa na wanaharakati wanaochochea ghasia, fujo na uvunjifu wa amani.
Rais Kikwete, aliyasema hayo juzi, mjini San Rafael, California, nchini Marekani, wakati alipokutana na kuzungumza na jumuia ya Watanzania waishio katika Jimbo la California.
Katika hotuba yake, ambayo alizungumzia mambo mbalimbali, Rais Kikwete aligusia mjadala wa karibuni bungeni kuhusu mchakato wa Katiba mpya na kusema kuwa alishangazwa na madai kuwa yeye kama Rais, hakuongozwa na mapendekezo ya wadau wakati anateua Tume ya Katiba.
“Watu wote niliowateua walipendekezwa na wadau mbalimbali, zikiwamo taasisi za dini. Yule Mama Maria Kashonda alipendekezwa na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Mama Mwantumu Malale alipendekeza na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA). Kila kundi ambalo lilipendekeza watu limepata mjumbe katika tume hiyo, wakiwemo walemavu ambao naambiwa nimewasahau,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
Kuhusu kama Tanzania itaweza kupata Katiba mpya kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Rais Kikwete alisema: “Ningependa sana na kwa kweli ni matarajio yangu makubwa, tuweze kumaliza mchakato wetu mwaka 2014 na tuweza kuwa na Katiba Mpya ili iongoze Uchaguzi Mkuu wetu wa mwaka 2015. Mchakato wetu unakwenda vizuri na wala siyo lazima tuhangaike na Katiba kwa miaka mingi. Muhimu ni ushirikishwaji wa kila mmoja wetu.”
Akizungumzia tabia za wanasiasa wa Tanzania kwa jumla, hasa wale wanaochochea chuki na ghasia, Rais Kikwete aliwaambia Watanzania hao:
“Sina tatizo na wanasiasa ama wanaharakati kupinga sera za Serikali yangu. Hili ni suala la nguvu ya hoja na tunao uwezo mkubwa sana wa kutetea sera zetu. Na wala sina tatizo na watu kunipinga mimi binafsi. Kinachonipa taabu mimi ni pale wanasiasa na wanaharakati wanapochochea ghasia na kuleta fujo. Kama mtu anataka kuongoza Tanzania si asubiri hadi atakapochaguliwa?”
Aliongeza Rais Kikwete: “Hivi unapochochea ghasia, fujo na chuki na kweli mambo hayo yakatokea na nchi ikateketea, utaongoza nchi ya namna gani? Utaongoza magofu na majivu yatakayobakia baada ya nchi kuteketea?”
Kuhusu mjadala wa karibuni kuhusu kama Rais awe na madaraka ya kuteua wajumbe 166 wa nyongeza ili kuingia katika Bunge la Katiba kujadili Rasimu ya Katiba Mpya, Rais Kikwete amesema kuwa yeye hana tabu kama itabidi ateua basi atateua, lakini kama siyo lazima yeye hana tabu. MTANZANIA
No comments:
Post a Comment