NYUMA ya habari ya mfanyabiashara tajiri wa Kariakoo jijini, Costa Shirima (47), anayedaiwa kujirusha kutoka ghorofa ya tisa katika Hoteli ya Concord iliyopo Kariakoo Mtaa wa Mchikichini, Dar es Salaam na kufariki dunia, kuna siri ambayo Ijumaa Wikienda limeelezwa.
Wananchi wakiwa eneo alipodondoka marehemu Costa Shirima.
Habari za kina kutoka hotelini hapo zilieleza kuwa Shirima alikuwa asafiri kwa ndege ya saa 10:00 jioni, Ijumaa iliyopita kuelekea nchini China kufuata bidhaa za maduka yake.
ALIMILIKI MADUKA KADHAA
Uchunguzi wa Ijumaa Wikienda ulibaini kwamba Shirima ambaye alithibitishwa kufariki dunia baada ya kukimbizwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar, alikuwa akimiliki maduka kadhaa ya urembo wa akina mama yaliyopo jirani na hoteli hiyo ya Concord.
Taarifa zaidi zilidai kuwa marehemu mara kwa mara alikuwa akipendelea kula katika hoteli hiyo na siku ya tukio inadaiwa kuwa aliwaeleza watu kuwa anapanda juu ya hoteli hiyo kupunga upepo.
Ilidaiwa kuwa jamaa zake walipomhoji kulikoni kwenda kupunga upepo mchana wote huo, Shirima alisema kuwa alihisi hewa nzito mahali alipokuwa.
Mwili wa Costa Shirima baada ya kujirusha kutoka ghorofa ya tisa katika Hoteli ya Concord iliyopo Kariakoo Mtaa wa Mchikichini, jijini Dar.
MHUDUMU AFICHUA MANENO YA MWISHO
Madai zaidi yalishushwa na mhudumu mmoja wa hoteli hiyo aliyeomba hifadhi ya jina kuwa jamaa huyo alipoingia mahali hapo, alitaka kupatiwa chumba cha kupumzika lakini alipopelekwa kwenye vyumba vya ghorofa ya kwanza alikataa hadi alipofika ya tisa na kuanza kupunga upepo.
Mhudumu huyo alidai kuwa alikuwa akimsikia Shirima akiongea peke yake akisema “Haiwezekani… haiwezekani kabisa…” na baadaye alipokea simu ya kiganjani ambayo alisikika akibishana na mtu wa upande wa pili.