Serikali ya mapinduzi Zanzibar imewaagiza Wahariri wa Gazeti la Mwananchi kuomba radhi Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (ZURA) ndani ya saa 24 kuanzia saa 9:00 Alasiri ya jana Septemba 28, 2017.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa naNaibu Mkurugenzi Idara ya Habari (MAELEZO) Zanzibar, Dk. Juma Mohammed Salum ambapo amesema iwapo wahusika hawatafanya hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya gazeti hilo la Mwananchi.
Hatua hiyo imekuja baada ya Serikali kudai gazeti hilo la Mwananchi linalochapishwa na kampuni ya Mwananchi Communications Limited Septemba 27, 2017 kuchapisha makala katika Ukurasa wake wa 16 yenye kichwa cha habari kisemacho “Siri ya nini Zabuni ya Mafuta Zanzibar”?
Salum amefafanua kuwa makala hiyo licha ya kujenga picha kwamba hakuna uwazi katika Zabuni ya uletaji Mafuta Zanzibar,msingi na maudhuhi ya Makala yenyewe kwa ujumla ni upotoshaji wa makusudi kwa nia ya kuipaka matope Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Taarifa hiyo pia licha ya kuwataka wahariri wa gazeti hilo kuomba radhi pia imefafanua ukweli wa mambo yalivyo kwa sasa ambapo Serikali, kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) tayari imeanzisha mfumo mpya wa uletaji Mafuta Zanzibar tangu Septemba Mosi, 2017.