Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta akisisitiza jambo juzi,
baada ya mkutano wa Kamati ya Maridhiano uliofanyika jijini Dar es
Salaam.
Wakati Bunge
Maalumu la Katiba likiazimia kuzifanyia marekebisho kanuni zake ili
kuwabana wajumbe wa Bunge hilo ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), viongozi wa kundi hilo wamesema hawatishwi na uamuzi
huo na kwamba wataendelea kususia vikao hivyo.
Kikao kilichokuwa kiwe cha mashauriano
kilichoitishwa juzi na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta
kiliazimia kuzifanya marekebisho baadhi kanuni za uendeshaji kwa lengo
la kusimamia nidhamu wajumbe wake, hatua inayotafsiriwa kwamba
inawalenga Ukawa.
Jana Sitta akizungumza na Mwananchi Jumamosi
alisema mabadiliko yanayokusudiwa kufanywa yatahusisha masuala ya
nidhamu, yakiwamo fujo na utoro, mambo ambayo hivi sasa hayawezi
kudhibitiwa moja kwa moja na mwenyekiti wa Bunge hilo.
Sitta alikuwa akitoa ufafanuzi wa taarifa
iliyotolewa na ofisi yake jana na kusomwa mbele ya waandishi wa habari
na Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad, ikieleza maazimio ya
kikao ya usuluhishi alichokuwa amekiitisha kwa ajili ya kutanzua mzozo
unaotishia kukwama kwa mchakato wa Katiba Mpya.
Hata hivyo, Ukawa unaoundwa na wajumbe wa Bunge
Maalumu kutoka Vyama vya Chadema, NCCR Mageuzi, CUF na baadhi ya wajumbe
kutoka Kundi la 201 walioteuliwa na Rais, walisusia kikao hicho na
kusababisha uamuzi uliofikiwa kuwa wa upande mmoja. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz