Serikali imepandisha maradufu ada kwa wanafunzi wanaosomea ualimu kwenye vyuo vya ualimu nchini kuanzia muhula ujao wa masomo. Ada hizo kwa wale wa ngazi za cheti na stashahada
ambazo zimeongezwa kwa karibu mara mbili au zaidi ya zile zilizokuwa
zikilipwa awali. Uamuzi huo ambao huenda ukawaathiri zaidi wanafunzi
ambao waliona ualimu kama kimbilio, unaelezwa na baadhi ya wadau
wakiwamo walimu, wanafunzi na hata wakufunzi wa baadhi ya vyuo nchini
kuwa ni wa ghafla.
Kwa mujibu wa baadhi ya wakufunzi, uamuzi huo
umetolewa kupitia waraka wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na
unatarajiwa kuanza kutekelezwa muhula wa pili wa masomo utakaoanza Julai
2, mwaka huu.
Kabla ya kupandishwa kwa ada hizo, wanafunzi
wanaosomea ualimu kwa ngazi ya cheti walikuwa wakilipa Sh200,000, lakini
sasa watalazimika kulipa Sh300,000, ikiwa ni ongezeko la asilimia 50. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Kwa wale wanaochukua stashahada watalazimika
kulipa Sh400,000 kwa masomo ya Sanaa na Sh600,000 kwa masomo ya Sayansi
kutoka Sh200, 000 za awali.
Mhasibu wa Chuo cha Ualimu cha Mtwara, aliyekataa
kutaja jina lake kwa kuwa siyo msemaji wa chuo hicho, alithibitisha
kupokea waraka wa Serikali unaowataka kupandisha ada, lakini alisisitiza
kuwa Mkuu wa Chuo ndiye angeweza kufafanua zaidi kuhusu ongezeko hilo.
“Taarifa hizo ni za kweli ada imepanda, kama
umezipata kutoka wizarani hivyo ndivyo ilivyo kwa hiyo huna sababu ya
kupata taarifa zaidi kutoka kwetu,” alisema mhasibu huyo.
Awali, habari zilizolifikia gazeti hili zilieleza
kuwa Serikali imefikia uamuzi huo kutokana na uhaba wa fedha na ugumu wa
kuviendesha vyuo hivyo.
Habari zinasema kwa muda mrefu sasa, Serikali
imekuwa ikidaiwa na wazabuni fedha nyingi, jambo ambalo limeathiri pia
uendeshaji wa vyuo vikiwamo vya ualimu.
Baadhi ya wakufunzi wameeleza kuwa fedha za ada
sehemu yake itatumika kutatua matatizo ya uhaba wa fedha ambao umekuwa
ukiwakabili na hivyo kuathiri utoaji wa huduma zikiwamo za vyakula.
Wizara ya Elimu
Msemaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
Ntambi Bunyazu alisema viwango vilivyoongezwa siyo vikubwa
ikilinganishwa na hali ya ugumu wa maisha ilivyo sasa nchini.
“Unamweka mtu mwaka mzima anakula, analala, anasoma…kweli unaona
hiyo ada hiyo ni kubwa? Bado siyo kubwa kiasi cha kushtua watu,”
alisema Bunyazu.
Aidha, Bunyazu alisema kuwa wanafunzi watakaopata
daraja la kwanza katika masomo ya Sayansi na Hisabati na kuingia katika
vyuo vya ualimu vya Serikali watasomeshwa bure na wale watakaopata
daraja la pili na la tatu watapewa mkopo.
Wengine wazungumza
Meneja wa Utafiti na Uchambuzi wa Sera wa Shirika
la HakiElimu, Godfrey Boniventura akizungumzia suala hilo jana, alisema
kuwa siyo kweli kwamba serikali haina fedha za kutosha ndiyo maana
inaongeza ada, ila inadhani kuwa idadi ya walimu waliopo inatosha.
“Serikali imeamua kupandisha ada kwa kudhani kuwa
walimu waliopo wanatosha, lakini ikumbuke kuwa kuna walimu wengi wazee
wanaostaafu kila mwaka, wengine hawaripoti shuleni, hivyo tunahitaji
kuwa na benki ya walimu,” alisema Boniventura. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Na Mwananchi
Na Mwananchi
No comments:
Post a Comment