Watu sita kati ya 12
wanaotuhumiwa kwa uchochezi na kuvunja chumba cha kuhifadhia maiti
katika Kituo cha Afya Kaigara wilayani hapa, jana wamepata dhamana baada
ya kutimiza masharti ya mahakama.
Mwendesha mashtaka wa polisi, Cleophace Waane
Maatu aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni pamoja na Georgina Angelo,
Triphory Joseph, Georgia Triphory, Shafii Abdul, Venanti Benard na
Shamim Yusuph.
Aliiambia mahakama kuwa mnamo Juni 16, mwaka huu
watuhumiwa hao walifanya uchochezi na kuvunja chumba cha maiti cha kituo
hicho na baadaye kutoa mwili wa binti aliyedaiwa kufariki na
kunyofolewa viungo vya mwili.
Maatu alisema mtuhumiwa wa kwanza ni shangazi wa
marehemu, Georgina Angelo aliyekuwa ametoroka na kukamatwa na polisi kwa
kuhusika na uchochezi kwenye mazishi ya binti huyo katika Kijiji cha
Bukono wilayani hapa.
Alisema Triphory Joseph na mkewe Georgia ambao ni
wazazi wa binti aliyefariki akifanya kazi za ndani mkoani Arusha na
Georgina Angelo wanatuhumiwa kwa uchochezi wa kuvunja mochwari ya kituo
hicho.
Alisema katika vurugu hizo, pia siku hiyo saa
11:00 jioni walivamia shamba la Valentina Maxmilian na kukatakata
migomba pamoja na mazao mengineyo kisha kuchoma nyumba mbili, vitu vyote
vikiwa na thamani ya Sh20 milioni.
Watuhumiwa wengine sita hawakutimiza masharti ya dhamana na kesi hiyo itatajwa tena Julai 10, mwaka huu.
Kesi hiyo imevuta hisia za wengi kufuatia kifo cha binti huyo kuzua sintofahamu. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz