Mkuu Mpya wa Jeshi la Polisi, Inspekta
Jenerali, Ernest Mangu ameanza kazi kwa kutangaza mabadiliko ya mfumo
wa jeshi hilo huku akiunda vitengo vipya kwa lengo kuongeza ufanisi
katika kukabiliana na uhalifu.
Katika mabadiliko hayo, IGP Mangu
amesema polisi wameanzisha kamisheni mpya tano ambazo ni Intelijensia,
Utawala, Fedha na Ugavi, Upelelezi, Uchunguzi wa Kisayansi wa Kesi za
Jinai na Polisi Jamii.
Mfumo huo mpya wa polisi ndiyo
uliowezesha kuundwa kwa nafasi mpya ya Naibu IGP, ambayo mteule wake wa
kwanza ni Abdulrahman Kaniki ambaye kabla ya hapo alikuwa Kamishna wa
Uchunguzi wa Sayansi wa Makosa ya Jinai. Nafasi hiyo sasa inakaimiwa na
watu waliokuwa chini yake.
Viongozi wengine katika safu hiyo ni
Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Issaya Mngulu, Kamishna wa
Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja, Kamishna wa Fedha na Ugavi,
Clodwig Mtweve, Kamishna wa Utawala, Thobiasi Andengenye na Kamishna wa
Polisi Jamii, Mussa Ali Mussa. Naibu Kamishna wa Polisi, Diwani Athuman
yeye anakaimu nafasi ya Kamisheni ya Intelijensia.
Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like page ya facebook ya Jambo Tz