Mkuu Mpya wa Jeshi la Polisi, Inspekta
Jenerali, Ernest Mangu ameanza kazi kwa kutangaza mabadiliko ya mfumo
wa jeshi hilo huku akiunda vitengo vipya kwa lengo kuongeza ufanisi
katika kukabiliana na uhalifu.
Katika mabadiliko hayo, IGP Mangu
amesema polisi wameanzisha kamisheni mpya tano ambazo ni Intelijensia,
Utawala, Fedha na Ugavi, Upelelezi, Uchunguzi wa Kisayansi wa Kesi za
Jinai na Polisi Jamii.
Mfumo huo mpya wa polisi ndiyo
uliowezesha kuundwa kwa nafasi mpya ya Naibu IGP, ambayo mteule wake wa
kwanza ni Abdulrahman Kaniki ambaye kabla ya hapo alikuwa Kamishna wa
Uchunguzi wa Sayansi wa Makosa ya Jinai. Nafasi hiyo sasa inakaimiwa na
watu waliokuwa chini yake.
Viongozi wengine katika safu hiyo ni
Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Issaya Mngulu, Kamishna wa
Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja, Kamishna wa Fedha na Ugavi,
Clodwig Mtweve, Kamishna wa Utawala, Thobiasi Andengenye na Kamishna wa
Polisi Jamii, Mussa Ali Mussa. Naibu Kamishna wa Polisi, Diwani Athuman
yeye anakaimu nafasi ya Kamisheni ya Intelijensia.
Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like page ya facebook ya Jambo Tz
Mabadiliko hayo yamekuja wakati
Tanzania ikikabiliwa na matukio ya uhalifu ambayo bado hayajapatiwa
ufumbuzi wa kiupelelezi, yakiwamo utekaji na utesaji wa watu, ulipuaji
mabomu, watu kumwagiwa tindikali, wizi kwa njia ya mitandao na mapigano
kati ya wakulima na wafugaji.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana, Mangu alisema amechukua hatua hiyo kutokana na changamoto ya
kukabiliana na aina mpya ya uhalifu ambao umekuwa ukijitokeza katika
siku za karibuni.
Alifafanua kuwa zamani kazi za Fedha na Ugavi zilikuwa zikifanywa na kitengo cha Utawala na Utumishi.
Mangu alieleza pia kuwa Kamisheni ya Uchunguzi wa Kisayansi ni kitengo kipya katika jeshi hilo.
Alisema mabadiliko hayo yamelenga kuliwezesha jeshi hilo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi katika mazingira ya sasa. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like page ya facebook ya Jambo Tz
"Jeshi limepanuliwa kidogo ili
kukabiliana na changamoto zilizopo na uteuzi huu ambao pia umefanya
kuwapo kwa Naibu IGP kwa mara ya kwanza una maana ya kuongeza ufanisi,"
alisema Mangu, akirejea hatua ya Rais Jakaya Kikwete kumteua Abdulrahman
Kaniki kushikilia nafasi hiyo mpya.
Alieleza kuwa wamepewa dhamana ya
kuliongoza jeshi hilo kutoka kwa mtangulizi wao, IGP Said Mwema huku
kiwango cha uhalifu kikiwa cha wastani na kuahidi kuupunguza maradufu.
Alisema wamepokea jeshi hilo tofauti na Mwema, ambaye alipopewa wadhifa huo 2006 kulikuwa na kiwango kikubwa cha uhalifu nchini.
"Tutajitahidi kubuni mbinu mpya za
kukabiliana na uhalifu kulingana na mazingira kwani uhalifu kila mwaka
unabadilika," aliongeza Mangu.
Kuchelewesha upelelezi
Mangu alikiri kuwapo kwa tatizo la
kuchelewa kwa upelelezi wa kesi zinazohusu uhalifu, ila alijitetea ni
kutokana na kujitokeza kwa uhalifu wa aina mpya.
"Tunalazimika kujipanga upya kukabili
vitendo vya uhalifu, pia katika masuala ya upelelezi," alisema na
kuongeza kuwa mkakati wao kwa sasa ni kuandaa vijana kwa ajili hiyo
kulingana na upatikanaji wa fedha kutoka serikalini.
"Tunatoa mafunzo kwa vijana jinsi ya kukabiliana na uhalifu mpya kama ule wizi kwa kutumia mtandao," alisisitiza Mangu.
Pia alizungumzia mapigano baina ya
wafugaji na wakulima, ambayo yametapakaa sehemu mbalimbali nchini kama
Ifakara, Kilombero na Kiteto.
Polisi na maadili
Mangu alibainisha kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa askari ambao watakiuka sheria na kanuni za jeshi hilo.
Alisema atajitahidi na timu yake
kuhakikisha hatua zinazofaa zinachukuliwa kwa askari watakaokiuka
misingi ya kazi zao na jeshi hilo litaendelea kuwaandaa askari wake
kulingana na wakati uliopo.
Pia alizungumzia suala la polisi
kutumia nguvu katika kukabiliana na uhalifu na kusema kwamba matumizi ya
nguvu itakuwa ni hatua ya mwisho na kwamba itafanyika pale tu watu
watakapokaidi amri halali.
"Matumizi ya nguvu ni hatua ya mwisho
kwa Jeshi la Polisi hivyo naomba ushirikiano kutoka kwa wananchi na
ninawaomba watii sheria bila shuruti," alisema na kuongeza kuwa yule
ambaye anadhani hakutendewa haki kuna njia za kufuata.
Alisema kama sheria ikifuatwa siyo
jambo rahisi kwa polisi kutumia nguvu, hivyo kuwataka wananchi kuendelea
kutii sheria bila shuruti.
No comments:
Post a Comment