Katika hotuba yake ya mwanzo ya Krismasi, Papa Francis amezungumza mjini Rome juu ya maeneo ya vita duniani.
Alitoa wito kwa pande zote zilizohusika na vita vya Syria ziruhusu msaada kufika kwa wanyonge.
Alisema:
"Maisha mengi yamevunjika katika vita vya Syria na kuchochea chuki na kulipiza kisasi.
Wacha tuendelee kumuomba Mungu
awaepushe wapendwa watu wa Syria na maafa zaidi, na kuziwezesha pande
zilizohusika na vita kumaliza ghasia na kuruhusu msaada ufike kwa wale
wanaouhitaji"
Papa Francis piya alitoa wito kwa
mapigano kusitishwa Sudan Kusini na aliwaomba viongozi wa kimataifa
kushughulikia zaidi yanayotokea Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo alisema
mara nyingi haitiwi maanani.
Akizungumza juu ya mamia ya wakimbizi
kutoka Eritrea waliozama karibu na kisiwa cha Utaliana cha Lampedusa
mwezi Oktoba, alieleza wasiwasi wake kuhusu wale wanaohatarisha kila
kitu ili kutafuta maisha bora.
Piya alizungumzia swala la ukatili majumbani, akitetea wanawake wanaopigwa.