Marekani imetoa ripoti inayozungumzia usafirishaji wa binadamu ya mwaka 2013, huku ikiitaja Tanzania kuwa kinara wa kunyanyasa wasichana, kuwatumikisha katika ngono na usafirishaji wa binadamu.
Ripoti hiyo iliyotolewa na idara ya nchi hiyo inayohusika na diplomasia (US Department of State, Diplomacy in Action), pia inaitaja Tanzania kuwa ni kitovu cha njia ya kusafirisha wanawake, watoto na wanaume ambao hutumikishwa kwenye kazi za mashambani na biashara ya ngono.
Ripoti
hiyo iliyozinduliwa Julai mwaka huu na Waziri wa Mambo ya Nje wa
Marekani, Seneta John Kerry inaweka bayana kwamba biashara ya
usafirishaji wa binadamu hufanywa na baadhi ya ndugu na marafiki ambao
hutoa ahadi kwa wahusika kwamba wanakwenda kuwasomesha au kuwatafutia
ajira nzuri mijini.
"Unyonyaji
wa wasichana wadogo na utumikishaji majumbani ndilo tatizo
linaloongoza, ingawa kesi za watoto kusafirishwa kwa ajili ya biashara
ya ngono katika mpaka wa Tanzania na Kenya zinaongezeka. Pia, wasichana
wananyonywa kwenye maeneo ya utalii," inasema sehemu ya ripoti hiyo.