Wadau wa habari nchini wametangaza
msimamo wa kutotangaza wala kuandika habari zinazomhusu Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenela Mukangara pamoja na
Mkurugenzi wa Idara ya Habari(Maelezo), Assah Mwambene kama sehemu ya
kupinga mwenendo wa serikali wa kuvifungia vyombo vya habari.
Wadau hao kutoka taasisi mbalimbali za
habari wamesema kuwa pamoja na kilio cha muda mrefu cha kuitaka
serikali kufuta Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, lakini hakuna jambo
lolote lililofanyika mbali ya kuendelea kuviandama vyombo hivyo.
Katika taarifa yao, wadau hao wamesema
pia wamesikitishwa na tabia iliyoonyeshwa na Dk Mukangara na Mwambene
kuchukua uamuzi wa kuyafungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania bila
kuyasikiliza na kupotosha umma juu ya jambo hilo.
"Kwa msingi huo, wadau tumeamua kwamba
tutasitisha kuandika, kutangaza na kupiga picha shughuli zozote
zitakazowahusisha au kuratibiwa na Dk Mukangara na Mwambene hadi hapo
itakapotangazwa vinginevyo. Adhabu hiyo inaanza mara moja kuanzia leo,"
imesema sehemu ya taarifa hiyo.