Serikali imeyafungia kutochapishwa
Magazeti ya MWANANCHI na MTANZANIA kuanzia 27 Septemba, 2013 kutokana na
mwenendo wa magazeti hayo kuandika habari na makala za uchochezi na
uhasama kwa nia ya kusababisha wananchi wakose imani kwa vyombo vya dola
hivyo kuhatarisha amani na mshikamano ulipo nchini.
Gazeti la MWANANCHI limefungiwa
kutochapishwa kwa siku kumi na nne (14) kuanzia 27 Septemba, 2013.
Adhabu hii imetangazwa kwa Tangazo la Serikali (Government Notice) Namba
333 la tarehe 27 Septemba, 2013.
Gazeti la MWANANCHI limepewa adhabu hiyo kutokana na hivi karibuni kuchapisha habari zenye mwelekeo wa
uchochezi na uvunjifu wa amani, mfano
tarehe 17 Julai, 2013 katika toleo Namba 4774 ilichapisha habari isemayo
"MISHAHARA MIPYA SERIKALINI 2013" kwa kuchapisha waraka uliozuiliwa kwa
matumizi ya vyombo vya habari waraka huo ulikuwa wa Siri haukupaswa
kuchapishwa Magazetini.
Aidha, katika toleo la Jumamosi,
tarehe 17 Agosti, 2013 lilichapisha habari yenye kichwa kisemacho
"WAISLAM WASALI CHINI YA ULINZI MKALI" habari hiyo ilikolezwe na picha
ya mbwa mkali mwenye hasira.