MKURUGENZI wa Mashitaka (DPP), Eliezer Feleshi, amesema haoni mantiki yoyote au uhalali wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), kumshitaki Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Alisema hayo janai wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari, baada ya kufungwa kwa mkutano wa siku tatu wa mawakili wa Serikali wafawidhi, wakuu wa upelelezi wa mikoa na vikosi vingine vya Polisi Alisema kauli aliyotoa Pinda bungeni, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu kuhusu Polisi kutumia nguvu kwa wananchi, ililenga wanaokaidi kukamatwa na kufikishwa mbele ya sheria na si kupiga na kuua kama ilivyotafsiriwa na wengi.
“Sijapata taarifa kwa maandishi juu ya azma ya kumshitaki Waziri Mkuu, lakini Pinda hajavunja sheria kwa kauli yake aliyotoa,” alisema. Alisema kwa jinsi alivyosikia maelezo ya Waziri Mkuu bungeni, kama LHRC wanamshitaki kwa jinai Waziri Mkuu, haoni uhalali wa mashitaka hayo.
Usahihi wa Pinda Alisema Waziri Mkuu alieleza hatua zinazochukuliwa dhidi ya mvunja sheria, na kufafanua kuwa Mtanzania yeyote ana haki kwa mujibu wa sheria, lakini pia ana wajibu, ndiyo maana vipo vyombo na kila chombo kimepewa mamlaka na wajibu wa kutekeleza. Alifafanua, kwamba kilichoongelewa ni dhana ya mkusanyiko ambayo ni haki kwa mujibu wa Katiba, ikiwemo uhuru wa kukutana, kutoa mawazo na kufanya mawasiliano.