Dar
es Salaam. Licha ya ujumbe wa Rais wa Marekani, Barrack Obama
kutarajiwa kufikia katika hoteli kubwa zenye hadhi wakati kiongozi huyo
atakapowasili nchini Julai Mosi mwaka huu, Ikulu ya Marekani imetoa
tahadhari ya vyakula ambavyo hawatakiwi kuvigusa wakiwa nchini ikiwa ni
pamoja na kutumia maji ya bomba.
Mbali na tahadhari hiyo,
ziara hiyo ya Obama itakuwa na ulinzi mkubwa ambao pengine haujawahi
kutokea katika historia ya viongozi wa nje wanaotembelea Tanzania kwani
utahusisha idadi kubwa ya magari, ndege za kijeshi na meli kubwa ya
kivita ambazo zitakuwa zikifanya doria karibu na pwani ya Tanzania.
Tahadhari
za matumizi ya chakula, maji na nyinginezo zimetolewa katika nchi zote
tatu za Afrika ambazo Obama atatembelea, kila moja kwa jinsi
Wamarekani hao wanavyoitathmini.
Rais Obama atatembelea nchi za Tanzania, Senegal na Afrika Kusini.
Ulinzi
Vyombo
vya usalama vya Marekani vimejipanga kuhakikisha ziara ya kiongozi
huyo haivurugwi kwa namna yoyote ile. Tayari ndege za jeshi zilizobeba
magari ya akiba 56, yakiwemo 14 aina ya ‘Cadillac One’ maalumu kwa
ajili ya kiongozi huyo, yamewasili katika nchi hizo tatu za Afrika
atakazotembelea.