WABUNGE wanachama wa Chama cha Kupambana na Ukimwi (TAPAC), wiki iliyopita walikutana na kujadiliana mambo mbalimbali na mashoga katika mkutano wa mwaka wa chama hicho uliofanyika kwa muda wa siku tatu mjini Dodoma. Katika mkutano huo, baadhi ya wabunge walionyesha wasiwasi wa taifa kupata rais shoga katika miaka ijayo kutokana na ongezeko la mashoga hapa nchini.
Mbali na wasiwasi ulioonyeshwa na wabunge, mashoga waliokuwa wakihudhuria mkutano huo, walilalamikia vitendo vya unyanyasaji wanavyofanyiwa na wanajamii wenzao na kudai watambulike na wapatiwe huduma za msingi za kibinadamu.
Akizungumza katika mkutano huo uliomalizika jana, Mbunge wa Nkasi, Ally Kessy (CCM), alitahadharisha uwezekano wa nchi kupata rais shoga katika miaka ijayo, iwapo hatua za makusudi za kudhibiti hali hiyo hazitachukuliwa.
“Tabia ya kuwapeleka watoto kwenye shule za mabweni wangali wadogo wa umri wa miaka hadi miwili, itatuletea matatizo baadaye.
“Katika shule nyingi za bweni vitendo vichafu vinafanyika, vikiwamo vya ushoga. Katika vyuo vikuu hivi sasa kuna mashoga wasiopungua 40,000. Hii ni hatari, tusipojihadhari tutakuwa na rais shoga katika miaka ijayo,” alisema Kessy huku akishangiliwa na wabunge.
Mbunge huyo alitaka elimu dhidi ya ushoga na athari zake ienezwe nchini kupitia vyombo vya habari na nyumba za ibada.