Jeshi la Polisi mkoani Mtwara limemkamata mbunge wa Mtwara Mjini (CCM), Hasnain Murji likimtuhumu kuchochea vurugu za kupinga mradi wa bomba la gesi kutoka mkoani humo kwenda jijini Dar es Salaam.
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Msemaji wa Jeshi la polisi nchini, Advera Senso zinaeleza kuwa Murji alikamatwa jana jioni nyumbani kwake maeneo ya Shangani mjini Mtwara.
Kukamatwa kwa mbunge huyo kunakuja ikiwa zimepita siku tano tangu viongozi wanne wa vyama vya upinzani mkoani Mtwara, kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara, Juni 4, mwaka huu wakikabiliwa na mashtaka matatu ikiwamo kula njama, kufanya uchochezi na kuamsha hisia mbaya kwa wakazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Washtakiwa hao ni Katani Ahmed Katani (33) na Saidi Kulaga (45) wa CUF, Hassan Uledi (35) wa NCCR Mageuzi na Hamza Licheta (51) wa TLP, wote wakazi wa Mtwara.
Taarifa zaidi zilieleza kuwa baada ya polisi kumkamata mbunge huyo, walifanya upekuzi katika nyumba yake kwa saa kadhaa na baada ya kujiridhisha walikwenda kupekua na ofisi yake.
“Amekamatwa kwenye saa 11:00 jioni, hata hati ya kukamatwa kwake imeeleza kuwa anatuhumiwa kuchochea vurugu za kupinga gesi inayopatikana mkoani Mtwara kwenda Dar es Salaam,” alisema Katibu wa Mbunge huyo, Meckland Millanzi.