Arusha. Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) Kanda ya Kaskazini, kimetangaza mgogoro na Mkuu wa Mkoa wa
Arusha, Magessa Mulongo na Kamanda wa Polisi Wilaya ya Arusha (OCD),
Gilles Bilabaye .
Hatua hiyo inatokana na kile kinachodai
walitumia lugha na kauli za matusi dhidi ya wanachama na wafuasi wa
chama hicho, kwenye harakati za kuzuia maandamano yaliyoitishwa
kumshinikiza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa
ajiuzulu.
Akisoma tamko la chama hicho kwa
waandishi wa habari jana, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alisema
viongozi hao waliwaita vijana wafuasi wa Chadema kuwa ni wahuni, wavuta
bangi na wanywa viroba.
Pia, wanadaiwa kuwaita wafuasi hao kuwa
hawana kazi za maana, ndiyo maana wanakubali kushiriki maandamano
yanayoitishwa na chama hicho.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, viongozi hao
wanadaiwa kutoa kauli hizo Jumamosi na Jumapili iliyopita wakiwa katika
harakati za kukabiliana na tishio la maandamano yaliyotangazwa na
Chadema, kabla ya kuahirishwa baada ya makubaliano kati ya Mwenyekiti wa
chama hicho, Freeman Mbowe na Mkuu wa Polisi nchini, Said Mwema.
Wakati Magessa akisema alitimiza wajibu
na majukumu yake ya kazi kuhakikisha maandamano hayo hayafanyiki, OCD
aligoma kuzungumzia tuhuma dhidi yake akisema mwenye mamlaka ya suala
lolote linalohusu polisi ni Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha,
Lebaratus Sabas alisema hawezi kuzungumzia tuhuma dhidi ya OCD wake, kwa
sababu hakusikiza maneno hayo yakitamkwa.
Januari 5, 2011 Chadema waliandaa
maandamano kupinga uchaguzi uliomweka madarakani Meya wa Arusha,
Gaudence Lyimo matokeo yake watu watatu waliuawa na polisi.