Wednesday, July 12, 2017

DIWANI MWINGINE WA CHADEMA ARUSHA, AJIUZULU LEO







Hali si shwari tena ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini, baada ya diwani mwingine wa chama hicho, Japhet Jackson kuandika barua ya kujiuzulu udiwani na kujiunga na CCM.

Diwani huyo ni wa saba kujiuzulu ndani ya mwezi mmoja, katika Jimbo la Arumeru Mashariki na Jimbo la Arusha mjini, majimbo ambayo wabunge wake ni Joshua Nassari na Godbless Lema.

Jackson amewasilisha barua leo mchana ya kuhama Chadema kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru, Christopher Kazeri na kueleza anamuunga mkono Rais John Magufuli.


Katika barua hiyo, Jackson ameeleza kuwa ameamua kujiondoa Chadema, baada ya kujiridhisha kuwa kazi ambazo walipanga kufanya kama upinzani sasa zote zinafanywa na Rais John Magufuli hivyo ameamua kumuunga mkono wazi wazi.

Akizungumza na Mwananchi leo, Kazeri amekiri kupokea barua ya diwani huyo kujiuzulu na kueleza kuwa tayari alikuwa anaendelea na taratibu kupeleka barua rasmi Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

"Muda huu naandika barua ya kuitaarifu tume ya uchaguzi, amekuja huyo Diwani hapa yeye mwenye amenikabidhi barua kwa mkono," amesema.

Diwani huyu sasa ni wa sita kujiuzulu katika Jimbo la Arumeru Mashariki na katika uchaguzi uliopita Chadema, ilishinda viti 25 vya udiwani na CCM iliambulia kiti kimoja.

Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari amesema, mchezo mchafu unaochezwa kuwashawishi madiwani kuhama haumpi shida kwani kabla ya uchaguzi wa mwaka 2015, alikuwa mbunge na madiwani wawili tu.

"Wasifikiri kuwaondoa madiwani wetu wanaimaliza nguvu Chadema, mimi nilishinda ubunge kwa mara ya kwanza nikiliwa na madiwani wawili tu na nina imani bado wananchi wanaimani na chama changu" alisema.

Nassari alisema tayari wamebaini wafadhili wa zoezi la kuhamisha madiwani, kwani madiwani wanne waliojiuzulu wanatoka kamati ya ardhi, ambayo imekumbwa na tuhuma za kubadili mihutasari katika migogoro ya ardhi.

Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Aman Golugwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Arusha, jana hakupatikana kuelezea hatua ambazo chama hicho kitachukuwa kutokana na kuhamwa na madiwani kwa madai kwamba alikuwa katika kikao.

Hata hivyo juzi Golugwa alieleza kuwa, alikuwa katika jimbo la Hai, Kilimanjaro, ambapo kulikuwa na njama za kushawishi madiwani kuhama na kabla ya hapo alikuwa Jimbo la Monduli ambapo napo kuna mkakati wa kushawishiwa madiwani kuondoka Chadema.

"Hatuwezi kumzuia ambaye anataka kuondoka, tena nadhani wamechelewa, waende tu lakini ipo siku watajibu dhambi hii ya usaliti," alisema.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...