Mambo yanayomtokea kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA) ni kama mchezo wa kuigiza.
Jana, Lissu alianza siku kwa furaha baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu kumuona hana kesi ya kujibu, lakini dakika chache baadaye polisi walimkamata tena, kumhoji na kumuachia kwa dhamana.
Licha ya kashikashi hizo mahakamani na kituo cha polisi, Lissu ameonyesha kuwa na sakata jingine katika uchaguzi wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) baada ya kudai kuwa kuna mkakati unasukwa na baadhi ya mawakili wenzake kutaka kumkwamisha asigombee urais wa chama hicho.
Baada ya kuachiwa huru, Lissu alikamatwa na polisi akiwa Mahakama ya Kisutu na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi, lakini haikueleweka sababu za kukamatwa kwake.
Lissu alikutana na polisi hao saa 4:00 asubuhi na akaambiwa kuwa anahitajika kituoni, mbunge huyo aliomba aendeshe gari lake mwenyewe ambalo alikuwa nalo Kisutu.
Wakili wake, Fredrick Kihwelo alisema: “Polisi walikubaliana naye na kuingia kwenye gari lake na kuelekea kituoni hapo na walipofika walikaa muda kisha wakaelezwa kuwa, anadaiwa kutoa matamshi yanayoweza kusababisha matatizo ya kidini.”
Alisema Lissu alidaiwa kutoa matamshi hayo akiwa mkoani Dodoma, hivyo baada ya mahojiano aliachiwa kwa dhamana na kutakiwa kuripoti kituoni hapo Machi 13.
Chanzo: Mwananchi.
No comments:
Post a Comment