RAIS Dk. John Magufuli, amesema kama atashindwa kutumbua majipu dhidi
ya wazembe na wabadhirifu serikalini, hana sababu ya kuendelea kushika
wadhifa huo.
Amesema endapo hali hiyo ikitokea ni bora arudi nyumbani kwake
akalale, kwa sababu lengo lake la kuwapatia wananchi Tanzania mpya,
litakuwa halijatimia.
Rais Dk. Magufuli aliyasema hayo jana, wakati wa hafla ya kuweka jiwe
la msingi la ujenzi wa barabara ya Arusha-Holili yenye urefu wa
kilometa 234.3, itakayogharimu Sh bilioni 209.3
“Ndugu zangu kazi hii ni ngumu, wapo watu ambao hawataki mimi na
Serikali yangu kuwatumbua, nitapambana hadi nihakikishe ninafanikiwa.
“Na iwapo nitashindwa hakuna sababu ya mimi kuendelea kuwa Rais wa nchi hii, ni bora nirudi nyumbani kwangu kulala,” alisema. Like page yetu ya facebook Jambo Tz
Dk. Magufuli alisema amejitoa sadaka kwa ajili ya Watanzania na hivyo
amewakumbusha wananchi waendelee kumwombea kwa Mungu, ili akamilishe
kazi hiyo ngumu.
Alisema amekuwa akipata vikwazo wakati wa kutumbua majipu, katika
hatua mbalimbali anazochukua dhidi ya watumishi wa umma wanaotumia
vibaya madaraka yao.
“Tanzania ilikuwa imegeuka kuwa shamba la bibi, ilikuwa nchi ya ovyo
kweli kweli, nimejitosa kuwa sadaka ya Watanzania, nihakikishe kuwa
nitawavusha kutoka katika lindi kubwa la umasikini linalowakabili
wananchi wa pato la chini,” alisema.
Rais Dk. Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC), amewataka wakuu wenzake wa nchi wananchama wa jumuiya
hiyo kuhakikisha wanatimiza wajibu waliokabidhiwa na wananchi ili
kuwasaidia kutoka kwenye umasikini.
Alisema umefika wakati viongozi wa nchi wanachama kuamka na kufanya
kazi kwa bidii kwa lengo la kuwanufaisha wanachi wao ambao wengi
wanateseka na umasikini, wakati nchi zao zimejaliwa rasilimali nyingi
ikiwemo madini, mbuga za wanyama, gesi asilia, mafuta,misitu na ardhi
nzuri kwa ajili ya kilimo.
Alisema barabara hiyo ikikamilika, itaharakisha maendeleo ya wananchi
wa nchi wanachama katika nyanja za kilimo, biashara, viwanda na
usafirishaji. Like page yetu ya facebook Jambo Tz
“Tutakapokamilisha barabara hii, tutaendelea na ujenzi wa barabara
zitakazounganisha nchi zote za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki,
tuunganishe Tanzania na Rwanda na Burundi, tuunganishe Tanzania na
Uganda na hatimaye mtandao wa barabara uziunganishe nchi zote sita”
alisema Rais Dk. Magufuli.
Alisema kati ya fedha hizo, Sh bilioni 190 zimetolewa na Benki ya
Maendeleo ya Afrika (ADB) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la
Japan (JICA), huku kiasi cha Sh bilioni 19.4 zikitolewa kwa pamoja kati
ya Serikali ya Tanzania na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.
“Lengo la nchi zetu ni kujitegemea, ndiyo maana kwa kiasi tunatumia
fedha zetu za ndani, hatutaki tabia ya kuombaomba kwa vile tunazo
rasilimali za kutosha, tukizitumia vizuri tutajitegemea” alisisitiza
Rais Magufuli.
SUDAN KUSINI
Kuhusu hatua ya kuikaribisha Sudan Kusini kuwa mwanachma wa jumuiya
hiyo, alisema nchi hiyo imekaribishwa baada ya pande hasimu zilizokuwa
zikigombana kupatana na kumaliza vita ya wenyewe kwa wenyewe.
“Nchi ya Sudan Kusini ni nchi tajiri sana, ina zaidi ya aina 22 za
madini na vito vya thamani, inaongoza kuwa na mifugo mingi katika
jumuiya yetu, uroho wa madaraka waliokuwa nao viongozi umechangia
wanachi wa nchi hiyo kuwa masikini na mimi nawaambia kuwa lazima
watambue madaraka yanatoka kwa Mungu” aliasa Rais Magufuli.
RAIS KENYATA
Kwa upande wake Rais wa Kenya, Uhuru Kenyata, alisema umefika wakati
kwa nchi za jumuiya hiyo kuondoa vikwazo vyote katika mipaka ya nchi zao
ili kurahisisha biashara zinazofanywa na wananchi wa nchi hizo .
Aliwataka viongozi wenzake kuweka mkakati wa pamoja wa kuanzisha
viwanda vipya na vya kisasa ili kuachana na vile vilivyoachwa na
wakoloni na kutoa ajira kwa vijana ambao wengi wamesoma na wanakimbilia
nchi za nje kwenda kutafuta kazi. Like page yetu ya facebook Jambo Tz
“Hatuna haja ya kuagiza nguo za mitumba kutoka nje ya nchi zetu,
hatuna haja ya kuagiza samani za ndani, magari, pamoja na bidhaa zingine
ambazo kwa mali ghafi tulizonazo tunaweza kuzitengeneza” alisema Rais
Kenyata.
Amesema kuna haja ya nchi za Afrika ya Mashariki kusimamia uchumi
wake na kuachana na tabia ya kuajiri wazungu na kwamba kama wazungu
wanataka kuja Afrika waje kwa ajili ya utalii na si kuja kutuletea nguo
na magari.
RAIS MUSEVENI
Naye Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alisema nchi hizo zinakosa
maendeleo pamoja na kuwa na rasilimali nyingi kutokana na wananchi wengi
kukosa huduma muhimu za afya na elimu.
“Tunao wajibu wa kusimamia na kuwaelimisha wananchi wetu ili waweze
kutumia ardhi nzuri kwa kilimo cha kisasa kitakachowezesha kuzalisha
chakula na ziada kwa ajili ya biashara na kukuza uchumi wa watu wetu.
“Barabara hii ikikamilika itanufaisha wananchi wetu , watasafirisha
mazao yao kutoka hapa Arusha kwenda Taveta na Mombasa huko Kenya,
itumieni vizuri pindi itakapokamilika” alisema.
Baadhi ya viongozi na wawakilishi kutoka nchi mbalimbali
waliohudhuria hafla hiyo, ni pamoja na Balozi wa Japan nchini Tanzania,
Masaharo Yoshida, Makamu wa Pili wa Rais wa Burundi, Dk. Joseph Butore,
Makamu wa Pili wa Rais wa Sudan Kusini, James Igga, Mwakilishi wa Rais
wa Rwanda, Valentine Rwegabure na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed
Shein. Like page yetu ya facebook Jambo Tz
Na Mtanzania
No comments:
Post a Comment