Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Magufuli.
RAIS Dk. John Magufuli amesema anapochukua hatua yeye si kichaa, si dikteta, si shetani wala si mnyama, ila ni mpole, lakini amefika mahali lazima afanye hivyo kwani ndani ya Serikali yanafanyika mambo ya ajabu.
Kauli hiyo aliitoa jana jijini Dar es Salaam katika kilele cha Siku ya Sheria nchini, alipokuwa mgeni rasmi kwa mara ya kwanza katika uzinduzi wa Mwaka wa Mahakama tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisifu kazi kubwa inayofanywa na Idara ya Mahakama, huku akitangaza uamuzi wa gharama za kurusha matangazo ya moja kwa moja ya Bunge zaidi ya Sh bilioni nne ni bora zikawasaidia wananchi.
“Ninapochukua hatua mimi si mnyama, si dikteta, si shetani, ni mpole kweli, lakini inafika mahali lazima nifanye, yanayofanyika serikalini ni mambo ya ajabu sana, nataka kutoa sadaka yangu, inawezekana hata nikifa naweza kuwa rais wa malaika,” alisema.
Alipongeza kazi kubwa inayofanywa na mahakama huku akibaki kujiuliza kwanini katika maadhimisho ya siku yao hawarushi matangazo yao moja kwa moja kupitia luninga.
“Mnafanya kazi kubwa, nilipofika niliuliza kwanini hii siku yenu hamrushi ‘live’, nikajibiwa fedha za kurusha ‘live’ zinapelekwa kuwahudumia wananchi.
“Kipindi kimoja kurusha ‘live’ kwa wiki mbili inatumika zaidi ya Sh bilioni nne, ni vizuri kuzikata hizo fedha zinazopelekwa kurusha ‘live’ zikapelekwa katika kesi za ubunge zinazohitaji shilingi bilioni tatu kusikilizwa hadi kumalizika kwake,” alisema.
Alisema mahakama ilikuwa inapewa bajeti ya Sh bilioni 41, lakini mwaka 2015/2016 ilishuka wakatakiwa kupewa Sh bilioni 12 ambazo hadi sasa hawajapewa.
“Kiongozi lazima ufikirie wapi pa kupeleka fedha na wapi pa kunyima, watu wa mahakama mnafanya kazi ya Mungu, nawaahidi ndani ya siku tano nitakuwa nimewapa Sh bilioni 12 zote.
“Sina tatizo la masilahi ya wafanyakazi wa mahakama, katika bajeti ya mwaka huu nitawapa fedha nyingi kuliko bajeti zote zilizopita, fedha zipo,” alisema.
MAHAKIMU KUTUMBULIWA
Rais Magufuli alisema anamwagiza Jaji Mkuu kuwachukulia hatua mahakimu 502 ambao hawakufikia malengo ya kumaliza kesi 250-260 kwa mwaka. Walimaliza kesi chini ya 100.
“Mahakimu ambao hawajafikia kumaliza kesi 260 hayo ndiyo majipu yako Jaji Mkuu, unatakiwa kuyatumbua, wewe uliniapisha hata mimi, leo unapitisha agizo mwingine anapinga.
“Unatoa siku saba sasa sijui ndiyo watamaliza kutoa hizo hukumu, nakuagiza wachukulie hatua, tusipochukua hatua hakuna kitakachofanyika.
“Walioshindwa kufikia lengo unawabakiza wa nini, wasomi wako wengi, hata ukitangaza leo watajitokeza, niruhusu mimi nitangaze, sitaki kuingilia mahakama,” alisema.
MABILIONI YA NIDA
Akizungumzia hatua yake kwa watendaji wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), alisema ilipewa Sh bilioni 176.6, lakini vitambulisho vilivyotengenezwa havifiki hata milioni mbili na havina sahihi wakati vitambulisho vya kupigia kura fedha iliyotolewa haizidi Sh bilioni 70, lakini vina sahihi za wapigakura wote wa Tanzania ambao ni milioni 23,253,982.
“Utaona ugumu wa kuongoza, nchi inatawaliwa na madudu ya kila aina, wapo watu wanacheza na fedha wanavyotaka wakati wapo watu masikini sana, wengine wanataka bodi zao wakakae Ulaya.
“Hapo ndipo tulipofikia, wengine wanalipwa mshahara kwa mwezi Sh milioni 35, naomba mniombee kabla ya kunihukumu, toeni hukumu kwa haki kwa hawa wanaotaka kuifikisha nchi pabaya, toeni hukumu zao haraka,” alisema.
KESI ZA WAKWEPA KODI
Rais Magufuli alisema kuna kesi 442 za kukwepa kodi ambazo zingeamuliwa Serikali ingepata Sh trilioni moja, ambayo ingeweza kununua ndege zaidi ya sita.
Alimuomba Jaji Mkuu kuzimaliza kesi 442 na kama zikimalizika fedha hizo Sh trilioni moja ataipa Idara ya Mahakama Sh bilioni 259 na Sh bilioni 750 zilizobakia zitanunuliwa ndege sita na wafanyafakazi 250 ATCL waliopo sasa wataondolewa.
Akizungumzia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, alisema kuna kesi 26 za watu waliokutwa na nyara za Serikali, ambazo zipo zaidi ya miaka mitano hazijaamuliwa kwa sababu upelelezi bado.
“Polisi wapo, DPP yupo, upelelezi unaendelea kila siku, hapo unaona tatizo lilipo, DPP upo unapeleleza nini au unatafuta rushwa?” alisema.
Alisema suala la kuanzishwa kwa mahakama ya mafisadi ya wahujumu uchumi halihitaji kwenda bungeni kufanya mabadiliko, lifanywe haraka, mahakama ianze kwani nchi inachezewa.
Pamoja na hali hiyo Rais Magufuli alikubali kupokea maombi yote yaliyotolewa na mahakama na kuyazingatia kwani lazima ayaunge mkono ikiwamo kukubali watumishi wa Idara ya Mahakama wasome na kupatiwa mikopo na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
“Nimeamua nchi iende na itaenda, anayefikiria ataikwamisha atakwama yeye, nategemea zaidi mahakama katika kufanikisha hilo,” alisema.
JAJI MKUU
Awali Jaji Mkuu Mohamed Othman Chande, alisema baada ya Uchaguzi Mkuu zimeibuka kesi 221 kupinga matokeo ambapo kati ya hizo za udiwani ni 175.
“Februari 22 mwaka huu kesi za ubunge zinaanza kusikilizwa ambapo zinahitaji Sh bilioni tatu ili zisikilizwe na kutolewa uamuzi, wananchi wanahitaji kujua nani mbunge wao,” alisema.
Alisema wananchi wanasubiri kwa hamu Mahakama ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, lakini wanawahakikishia itaanza kazi mwaka huu.
Jaji Chande alisema kesi zitasikilizwa na majaji wazoefu na rufani zitawekewa njia maalumu kumalizika haraka.
TLS NA AG
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Charles Rwechungura, alisema chama hicho kitamsaidia Rais Magufuli kuhakikisha anaendelea kupambana na mafisadi kwa kuzingatia misingi ya sheria.
Alisema sheria inayounda TLS imepitwa na wakati na inatakiwa kufanyiwa mabadiliko, hivyo walishawasilisha maombi ya kubadili sheria.
Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) akiwakilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga, alisema mahakama ndiyo yenye mamlaka na kauli ya mwisho katika utoaji hukumu.
No comments:
Post a Comment