Kocha wa timu ya soka ya Taifa ya Taifa Stars, Charles Mkwasa.
KOCHA mpya wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa amewataka mashabiki wa Simba kutomzomea pindi watakapomuona kwenye mazoezi au mechi, kwa vile atakuwa pale kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya wachezaji wake wa timu ya taifa.
Akizungumza Dar es Salaam juzi, Mkwasa alisema mashabiki wanatakiwa kufahamu kuwa yeye ni kocha wa taifa, hivyo atakuwa akitembelea katika mechi za timu mbalimbali kuangalia wachezaji na maendeleo ya wale wanaocheza timu ya taifa.
“Mashabiki wa Simba mnaponiona kwenye mechi zenu msinikimbize kwa mawe mkadhani kuwa nimekuja kwa ajili ya Yanga, nitakuwa na utaratibu wa kutembelea timu kuangalia wachezaji, mnajua kazi ya kocha wa taifa ndio hiyo,” alisema Mkwasa ambaye pia ni Kocha Msaidizi wa Yanga.
Kujihami kwa Mkwasa ni kutokana na tabia iliyopo kwa mashabiki hasa wa Yanga na Simba, pindi wanapoona kiongozi wa Yanga au Simba anakwenda kwenye mechi zao hufanya vurugu.
Alisema atakuwa anachagua wachezaji wenye uwezo na ambao wanatumika katika timu zao, na kwamba iwapo kuna baadhi watakuwa wanacheza timu ya taifa na wakabainika viwango vyao vimeshuka watapigwa chini.
Alisema atakuwa akichagua wachezaji kwa kuangalia uwezo wake bila kubagua na sio timu, na kwamba wachezaji wanatakiwa kujituma.
Mkwasa alipewa jukumu la kuinoa Stars baada ya aliyekuwepo Mart Nooij kutimuliwa kwa kufanya vibaya katika michuano ya kimataifa.
Benchi la ufundi la Taifa Stars kwa sasa linasimamiwa na makocha wazalendo chini ya Mkwasa, msaidizi wake Hemed Morocco na mshauri wa timu Abdallah Kibadeni.
Kitendo cha timu ya Taifa kupewa kocha mzalendo sio cha kwanza, miaka ya nyuma aliwahi kuchukuliwa kocha wa Simba, James Singalaza.
No comments:
Post a Comment