Katibu Mkuu wa Chadema, Dk
Willibrod Slaa amesema endapo vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) vitashindwa kuafikiana katika kuachiana baadhi ya
majimbo kabla ya Uchaguzi Mkuu, watawaeleza wananchi kwa kuwa ndiyo
kiini cha kuanzishwa kwa umoja huo.
Dk Slaa alisema hayo jana kabla ya kumalizika kwa
vikao vya wakuu wa Ukawa ambao wamekubaliana kusimamisha mgombea mmoja
kuanzia ngazi ya urais, ubunge na udiwani na kwa siku mbili kuanzia
juzi, walikuwa wakijadili ufanikishwaji wa azimio hilo.
Dk Slaa alisema hadi sasa wameshakubaliana
kuachiana asilimia 95 ya majimbo yote na kwamba ana matumaini
watafanikisha, lakini akaonya kuwa ikishindikana, hawatasita kuwaeleza
wananchi. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Mkoani Dar es Salaam, Ukawa imeshafikia muafaka
katika majimbo mawili ya Kawe na Ubungo na kubakiza majimbo sita, wakati
majimbo matano ya mikoa mingine bado yanaupasua kichwa umoja huo wa
vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD.
“(Kuanzishwa kwa) Ukawa ilikuwa ni ombi la
Watanzania, ni sauti yao kwa hivyo taarifa zinazoendelea kutolewa siyo
sahihi,” alisema akirejea habari kuwa Ukawa, iliyoanzishwa wakati wa
Bunge la Katiba inaelekea kusambaratika kutokana na kushindwa kuafikiana
kwenye baadhi ya majimbo.
“Kama ikitokea tumeshindwa kufikia makubaliano
mwisho wa safari yetu, hakuna kitakachokuwa siri, tutawaeleza
Watanzania,” alisema Dk Slaa.
Hata hivyo, alisema mpaka sasa hakuna dalili
zozote za umoja huo kushindwa kuafikiana kwa sababu ya mvutano wa
majimbo hayo, kwani mpaka sasa wameshafanikiwa kuyagawana kwa asilimia
95 nchini kote.
Alipoulizwa itakuwaje kama hawatafikia muafaka
kwenye vikao hivyo vya siku mbili, Dk Slaa alisema bado kutakuwa na
nafasi ya kuendelea na majadiliano katika vikao vingine.
“Aliyekwambia tuna ratiba ya kumaliza leo (jana)
juu ya mgwanyo wa majimbo hayo ni nani? Hatuna ratiba maalumu kwa kuwa
tunapanga ratiba wenyewe,” alisema Dk Slaa, ambaye ni mmoja wa watu
wanaotajwa kugombea urais kwa tiketi ya Ukawa.
“Kuna mtu mwingine ambaye majadiliano yanapokuwa kwenye hali ya kuvutana, yeye anaona ni mpasuko. Sasa hilo ni tatizo kubwa.”
Habari za ndani kutoka katika vikao hivyo
zinaeleza kuwa uliibuka mvutano mkali kuhusu mgawanyo wa majimbo 17
yaliyobaki mpaka sasa.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi James Mbatia alisema haoni dalili zozote za Ukawa kutofanikiwa katika asilimia tano zilizobakia.
“Kama tumeshakubaliana kwa asilimia 95, iweje tushindwe
kuafikiana kwenye asilimia tano? Katika meza yoyote ya maridhiano,
mvutano hauepukiki. Tunachoangalia ni ‘give and take’. Ikishindikana
tutafuta tiba kwa sababu tunaijua,” alisema Mbatia ambaye anatajwa
kutaka kuwania ubunge wa Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro.
Kikao hicho kilianza juzi wakati wajumbe
walipopokea taarifa ya kamati mbili zilizokuwa zikifanya uchunguzi
kwenye majimbo sita ya Dar es Salaam na majimbo kumi na moja ya mikoani.
Juzi, wajumbe hao walifanikiwa kugawana majimbo
sita tu kati ya kumi na moja ya mikoani huku mengine yakibakia kwenye
mvutano kabla ya kuanza mjadala wa majimbo sita ya Mkoa wa Dar es
Salaam.
Kikao hicho kilihusisha wenyeviti, makatibu, wajumbe wa sekretarieti za vyama hivyo.
Chanzo hicho kilieleza kuwa moja ya majimbo ambayo
yalikuwa yanawakuna vichwa ni Serengeti ambako kigogo wa moja ya vyama
hivyo anataka kuwania ubunge wakati chama chake hakina nguvu. Mkoani Dar
es Salaam, mvutano katika majimbo sita unatokana na kila chama ndani ya
Ukawa kuamini kuwa kwa kutumia nguvu ya umoja huo, mgombea wake anaweza
kushinda.
“Kila chama kinahitaji kupata majimbo yaliyobakia
bila hata kujali vigezo, kwa mfano, NLD ilikuwa inahitaji majimbo mengi
lakini inaonekana kuwa na nguvu kwenye majimbo mawili tu ya Masasi na
Lulindi ya Mtwara,” alisema mpashaji habari wetu.
Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi alisema
katika mipango ya chama chake, waliomba kupewa majimbo 35 wanayoamini
kuwa wanaweza kufanya vizuri kwenye Uchaguzi Mkuu, lakini vyanzo vya
ndani vinaeleza kuwa chama hicho kimepangiwa majimbo mawili tu mpaka
sasa.
Alipoulizwa endapo hataweza kupata hata nusu ya
majimbo hayo, Dk Makaidi alisema, bado haiwezi kuwa sababu ya kujiondoa
ndani ya umoja huo.
“Siwezi kuondoka Ukawa nikikosa na pia siamini kama nitakosa majimbo, lazima yatapatikana tu,” alisema.
Kuhusu taarifa za kukabidhiwa majimbo mawili ya
Lulindi na Masasi, Dk Makaidi alisema pamoja na majimbo hayo, leo
(jana), walitarajia kuona hatima ya mgawo wa majimbo yote.
Mke wa Makaidi, Modesta Ponela ambaye mwaka 2010
aligombea ubunge wa Jimbo la Lulindi na kuibuka mshindi wa pili, alisema
jana kwamba yuko tayari kugombea tena jimbo hilo endapo Ukawa
itampitisha. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
No comments:
Post a Comment