Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Msangi (katikati) akiwasihi Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (kushoto) na Mbunge wa Nkasi, Ali Kessy wasigombane kwenye Viwanja vya Bunge, mjini Dodoma jana.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo jana alipangua hoja zilizotolewa na Kamati ya Hesabu za
Serikali (PAC), kuhusu ufisadi uliofanyika katika Akaunti ya Tegeta
Escrow na kuacha wananchi njia panda kwa kutokuelewa nani anasema ukweli
kati yake na kamati hiyo, inayoongozwa na Zitto Kabwe.
Juzi, kamati hiyo ya Zitto iliwasilisha ripoti
yake kuwa imethibitisha kuwa Profesa Muhongo amekuwa mara kwa mara
akilipotosha Bunge na Taifa kwa ujumla kwamba ndani ya fedha hizo
hakukuwa na fedha za umma.
Kamati hiyo ilieleza kuwa imebaini kuwa Profesa
Muhongo ndiye aliyekuwa dalali mkuu aliyewakutanisha Singh Sethi na
James Rugemalira tena katika ofisi ya umma na pengine hilo ndilo
lilikuwa sababu ya upotoshaji.
Akiwasilisha taarifa ya Serikali kuhusu hoja hiyo,
Profesa Muhongo alianza kupangua hoja moja baada ya nyingine ingawa
katika mjadala wa baadaye, zilihojiwa na wachangiaji wengine waliohoji
uhalali wa vielelezo alivyotoa. Asante
kwa kutembelea blog hii na endelea kuwa nasi siku zote, kuwa wa kwanza
kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya
neno Jambo Tz
Kutaifisha mitambo
Jana, alieleza kuwa pendekezo la Kamati ya PAC
kutaka mitambo ya IPTL itaifishwe si sawa kwa kuwa kulingana na mkataba
wa PPA kati ya Tanesco na IPTL, majukumu ya IPTL yalikuwa ni kujenga,
kumiliki na kuendesha (Build, Own and Operate – BOO). Hivyo, kutaifisha
mtambo huo ni kukiuka makubaliano katika mkataba wa PPA wa Mei 26, 1995.
“Ukiukwaji wa aina hii ukitokea unaweza kuingiza
Serikali katika mgogoro mkubwa ikiwa ni pamoja na kushtakiwa kwenye
Mahakama za kibiashara za kimataifa. Aidha, utaifishaji wa miradi ya
uwekezaji binafsi itakuwa ni njia ya kufukuza wawekezaji.”
Gharama za uwekezaji
Kuhusu taarifa ya kamati ya PAC kwamba mwaka 2004
Tanesco ilifungua shauri katika Kituo cha Kimataifa cha Utatuzi wa
Migogoro ya Kiuwekezaji (ICSID 2) kupinga kiasi kikubwa cha tozo ya
gharama za uwekezaji, Profesa Muhongo alisema suala hilo si kweli.
Alifafanua kuwa Tanesco haijawahi kufungua shauri
lolote ICSID ya London au Mahakama yoyote dhidi ya Benki ya Standard
Charterd kupinga kiasi kikubwa cha Capacity Charge kama inavyoelezwa na
PAC.
“Shauri la ICSID 2 lilifunguliwa Oktoba 31, 2010
na Standard Chatered Bank Hong Kong (SCBHK) kwa ajili ya kudai malipo ya
deni ililonunua kutokana na mkopo uliotolewa na mabenki ya ushirika ya
Malaysia kwa IPTL. Wahusika katika shauri hilo la ICSID 2 ni SCBHK na
Tanesco na wala siyo Tanesco na IPTL.”
Alisema Februari 12, ICSID ilitoa uamuzi kuhusiana
na shauri la SCBHK na Tanesco na kuwashauri wakae kukokotoa upya malipo
ya Capacity Charge. Hata hivyo, ilikuwa vigumu kwa pande hizo
kutekeleza uamuzi huo kutokana na pande hizo kutokuwa na mkataba wa
kibiashara baina yao.
Na Mwananchi
“Vilevile, kupitia shauri la madai Na. 60/2014, lililofunguliwa
na IPTL katika Mahakama Kuu ya Tanzania Aprili 4, ilizuia utekelezaji wa
maelekezo hayo,” alisema.
Uwekezaji wa Sh50,000
Profesa Muhongo alisema kuhusu madai ya PAC kuwa
mtaji wa uwekezaji katika mtambo wa IPTL ni Sh50,000 na kwamba huo ndiyo
ungetumika kukokotoa gharama za uwekezaji ili kulipa tozo ndogo kuliko
ilivyo sasa, maelezo hayo siyo sahihi.
Alisema ukweli ni kwamba kutokana na uamuzi ya
ICSID 1 ya Julai 12, 2001, gharama za ujenzi wa mtambo wa Tegeta ni Dola
za Marekani 127.2 milioni kama ilivyoelezwa na taarifa ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Profesa Muhongo alisema katika taarifa hiyo, pia
imeelezwa kuwa ilikubalika kuwa uwiano wa deni na mtaji utakuwa 70:30
ikiwa na maana kwamba, deni ni Dola za Marekani 89.04 milioni na mtaji
ni Dola za Marekani 38.16 milioni na kwamba uamuzi huo haujabadilishwa
na Mahakama yoyote au mtu yeyote.
“Tunakubaliana kwamba fedha iliyopokewa kutoka
mabenki ya ushirika ya Malaysia kama mkopo ni Dola za Marekani 85.86
milioni ambazo kati ya Dola za Marekani 105 milioni zilizokuwa
zimeidhinishwa,” alisema na kuongeza:
“Swali la kujiuliza je, mtambo huo ulikamilikaje
kwa gharama ya Dola za Marekani 85.86 milioni, huku gharama halisi ya
ujenzi wa mtambo wa Tegeta ikawa Dola za Marekani 127.2 milioni?
Alisema ni dhahiri kwamba kuna matumizi ya zaidi
ya Dola za Marekani 38.16 milioni ambazo pia zimetumika kwenye uwekezaji
na kwamba Kamati ya PAC haikuonyesha fedha hizo kuwa sehemu ya
uwekezaji.
PAP na umiliki wa hisa saba
Profesa Muhongo alisema kuwa kwa mujibu wa taarifa
za Brela za Desemba 31, 2013, uhamishaji wa hisa saba za Mechmar katika
IPTL kwenda PAP ulisajiliwa hapa nchini. Kwa maana hiyo, PAP ni mmiliki
wa asilimia 70 za IPTL.
Alisema Kamati ya PAC imeeleza kuwa PAP siyo
mmiliki halali wa hisa saba za Mechmar katika IPTL lakini kamati
imethibitisha kwamba nyaraka za mauziano kati ya Mechmer na Piper Link
zilipokewa na Harbinder Singh Sethi ambaye pia ndiye mmiliki wa PAP.
“Kwa uthibitisho huo, kamati inakubali kuwa hisa za Mechmer katika IPTL zinamilikiwa na PAP,” alisema Profesa Muhongo.
Akana kuwa dalali
Profesa Muhongo alisema taarifa ya Kamati ya PAC
kwamba yeye ndiye aliyekuwa dalali mkuu aliyewakutanisha Harbinder Sethi
na James Rugemalira siyo sahihi kuwa tangu Novemba 9, 2011, Rita
iliitisha mkutano na kuwakutanisha wadau wote wa IPTL wakati yeye
alikuwa hajateuliwa kwenye wadhifa huo.
“Mimi kama ni dalali, udalali wangu ni kupeleka
umeme vijijini. Mimi kama ni dalali udalali wangu ni kusaidia wachimbaji
wadogo wa madini na kupeleka Watanzania kusoma masters (shahada ya
pili) duniani kote.”
Serikali kutokuchukua tahadhari
Waziri alisema Kamati ya PAC, imeeleza kuwa
Serikali haikuchukua tahadhari ya kutosha dhidi ya madai mengine
yanayoweza kujitokeza kabla ya kutolewa kwa fedha kutoka akaunti ya
escrow kitu ambacho alidai si kweli.
Profesa Muhongo alisema kinga iliyochukuliwa
inakidhi matakwa ya kisheria na imezingatia athari yoyote ambayo
ingeweza kutokea baadaye kutokana na kutolewa kwa fedha katika akaunti
ya escrow.
“Kwa hiyo, siyo kweli kwamba Serikali haikuchukua tahadhari kama ilivyodaiwa na PAC.”
Madai ya Sh321 bilioni
Profesa Muhongo alisema hoja ya PAC kwamba
imejiridhisha kuwa madai ya Tanesco ya Sh321 bilioni yana uhalali japo
usahihi wake utapatikana baada ya kutekelezwa kwa uamuzi wa ICSID 2 na
Tanesco na IPTL kukubaliana kiwango sahihi cha Capacity Charge haina
nguvu.
“Madai ya kwamba Tanesco inaidai IPTL Sh321
bilioni msingi wake ni dhana kwamba mtaji wa IPTL ni Dola za Marekani
100, sawa na Sh50,000 kwa wakati huo. Dhana hii ilipuuza ukweli kwamba
Dola za Marekani 38.16 milioni ziliwekezwa kwenye mradi wa Tegeta,”
alisema.
Profesa Muhongo alisema Bodi ya Tanesco imekana
kuyatambua madai hayo ya Sh321 bilioni... “Kimsingi hata vitabu vya
hesabu vya Tanesco ambavyo vimekuwa vikikaguliwa na CAG, havionyeshi
kuwapo kwa deni hilo.” Asante
kwa kutembelea blog hii na endelea kuwa nasi siku zote, kuwa wa kwanza
kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya
neno Jambo Tz
Na Mwananchi
No comments:
Post a Comment