Kwa maneno ya siku hizi ni
kwamba Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Fredrick Werema
'amelikoroga na kulinywa mwenyewe', baada ya jana kutoa kauli ya kuudhi
alipomtaka mbunge kutoka Zanzibar akaulize swali lake visiwani humo,
iliyosababisha baadhi ya wabunge kususia Bunge na kutoka.
Kauli iliyoonyesha kuwagawa wabunge
katika mafungu mawili; wa bara na Zanzibar, ilimlazimu Jaji Werema
baadaye kusimama bungeni na kuwaangukia akiwaomba radhi waliokerwa na
kauli yake na pia kuliomba radhi Bunge, Spika wake, Anne Makinda na
wananchi.
Kuondoka kwa wabunge hao kulitokana na
mwongozo wa Spika ulioombwa na Mbunge wa Ole (CUF), Rajabu Mbarouk
Mohamed kutokana na majibu Jaji Werema kwa mbunge wa Mkanyageni (CUF),
Habibu Mnyaa aliyekuwa ameomba ufafanuzi wakati Bunge lilipokaa kama
kamati ya kupitisha vifungu vya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya
Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2014/15. Mnyaa alisema Wizara ya Katiba na
Sheria ni muhimu lakini imekuwa ndiyo ya kwanza kuvunja sheria na haki
za binadamu na akataka ufafanuzi.
Hata hivyo, aliposimama kujibu swali
hilo, Jaji Werema alimwambia Mnyaa kuwa mambo mengine akaulize Zanzibar
na siyo katika Bunge la Jamhuri kwa kuwa si kila kitu kitaulizwa ndani
ya Bunge hilo. "Alichokizungumza Mnyaa ni sahihi
lakini hapa si mahali pake, namshauri kuwa akaulize huko Zanzibar kwenye
vikao vyao hapa sisi hatuna majibu," alisema Werema. Tafadhari Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz
Mara baada ya Bunge kurejea, Mbarouk aliomba mwongozo wa Spika akitaka ufafanuzi wa kauli hiyo kwamba ilikuwa ya kibaguzi. "Mheshimiwa Spika, huu ni ubaguzi na haupaswi kufanywa na mtu msomi kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali," alisema Mbarouk. Alisema ubaguzi huo umewabagua wabunge
ambao wamekula kiapo cha kulitumikia Bunge la Jamhuri ya Muungano na
unaonyesha namna ambavyo Wazanzibari wanabaguliwa.
"Mheshimiwa Spika, yanapofanyika mambo
kama hayo na wewe mwenyewe uko hapa unaona ni sawa na kubariki jambo
hilo, huu ni ubaguzi unaoufanya wewe kwa kuwa lilifanyika ukiona bila
hata ya kukemea," alisema Mbarouk. Hata hivyo, Spika alipinga na kusema:
"Hakuna mwongozo wowote kwa kuwa hata wewe umevunja sheria kwani hata
nilipokuambia kaa chini umeendelea kuzungumza, tunaendelea.... Katibu
(akimtaka Katibu wa Bunge kutoa mwelekeo wa shughuli iliyokuwa inafuata
ambayo ilikuwa Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi)."
Baada ya kauli ya Spika, wabunge wa
Zanzibar walihamasishana na kuamua kutoka nje kwa wakati mmoja na huku
wenzao wa upinzani wakiendelea kutafakari cha kufanya. Wakati huo,
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe alikuwa akisoma hotuba
yake. Muda mfupi baadaye, wabunge wa Chadema
na NCCR Mageuzi nao walitoka na katika viti vya upinzani, alibaki John
Cheyo wa UDP peke yake.
Baada ya kutoka
Akizungumza nje ya Viwanja vya Bunge,
Mbarouk alisema wametoka kwa sababu Spika na Jaji Werema wamewadharau.
"Hatutarejea ndani ya Bunge hadi hapo watakapotuomba radhi, wasipotuomba
radhi hatutarejea bungeni," alisema Mbarouk. Hata hivyo, wakiwa nje ya Ukumbi wa
Bunge, mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed aliwafuata na
kuwaeleza kuwa amezungumza na Werema na amekubali kuomba radhi kwa
wabunge na Watanzania.
"Ndugu zangu nimeongea na Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, amekubali kuomba radhi," alisema Hamad Rashid jambo
ambalo liliungwa mkono na wabunge wa CUF waliokuwa wamekaa katika
makundi katika Viwanja vya Bunge. Hata hivyo, wabunge hao baada ya muda
wa dakika 15, walikwenda katika kikao cha dharura kwenye Ukumbi wa Kambi
ya Upinzani ambako pamoja na mambo mengine, walijadiliana kusudio la
kumuona Spika Makinda kumweleza mambo yasiyowaridhisha.
Werema aomba radhi
Muda mfupi kabla ya Bunge kuahirishwa,
Jaji Werema alisimama na kusema: "Kwa imani yangu, ninaamini kila
binadamu ana nyongo, isipokuwa watu wawili... Yesu Kristo na Mtume
Muhammad (SAW), ndiyo pekee ambao hawakuwa na nyongo. Naomba maneno
yangu yafutwe katika kumbukumbu za Bunge hili.
"Mimi ni Jaji kwa taaluma na kwa
nafasi yangu nimekosea kwa kutoa maneno hayo. Nimetambua kosa langu na
naomba radhi... kwanza kwako Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rajab Mbarouk,
Mheshimiwa Injinia Habib Mnyaa, Bunge hili na Watanzania kwa jumla."
KULIKOROGA
"Alichokizungumza Mnyaa ni sahihi
lakini hapa si mahali pake, namshauri kuwa akaulize huko Zanzibar kwenye
vikao vyao hapa sisi hatuna majibu."
KULINYWA
"Mimi ni Jaji kwa taaluma na kwa
nafasi yangu nimekosea kwa kutoa maneno hayo. Nimetambua kosa langu na
naomba radhi... kwanza kwako Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rajab Mbarouk,
Mheshimiwa Injinia Habib Mnyaa, Bunge hili na Watanzania kwa jumla. Tafadhari Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment