MARAIS KUINGIA KWA KADI MAZISHI YA MANDELA...!!!
TISHIO
la vitendo vya kigaidi vinavyotokea kwenye maeneo mbalimbali hapa
duniani, vimeifanya Serikali ya Afrika Kusini, kutoa kadi kwa marais na
viongozi watakaohudhuria mazishi ya baba wa taifa hilo, Nelson Mandela.
Mandela aliyefariki Desemba 5, atazikwa Desemba 15 kijijini kwake Qunu, eneo alilolichagua kabla ya mauti yake.
Kwa mujibu wa vyombo mbalimbali vya kimataifa, usalama katika miji ya
Afrika Kusini, unatarajiwa kuimarishwa zaidi kuliko hata ule unaotumika
kwa marais wa Marekani wanapofanya ziara kwenye mataifa mbalimbali.
Taarifa hizo zinabainisha kutokana na idadi kubwa ya watu kuhudhuria
mazishi hayo, utawala wa nchi hiyo umebuni mbinu hiyo ya utoaji kadi kwa
watu watakaokuwa eneo la maziko wakiamini itasaidia kuimarisha ulinzi.
Mazishi hayo yanatarajiwa kuvunja rekodi ambapo yanalinganishwa na
yale ya Papa John Paul II mwaka 2005, ambayo yalihudhuriwa na wafalme
watano, malkia sita wa falme mbalimbali na marais wapatao 70 na mawaziri
kadhaa, wakiwamo wafuasi wake zaidi ya milioni mbili.
Ratiba ya kutoa heshma za mwisho yatangazwa
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana na Serikali ya Afrika Kusini,
mwili wa Mandela utawekwa katika jengo la serikali kwa muda wa siku
tatu, kutoa fursa kwa wananchi kutoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi
waliyempenda.
Meya wa jiji la Cape Town, Patricia de Lille, alisema ibada ya
kumuaga Mandela itafanyika Jumanne kwenye uwanja wa mpira mjini
Johannesburg.
Jana maelfu ya raia wa Afrika kusini kutoka matabaka yote na rika
zote walishiriki katika ibada ya pamoja ya dini mbalimbali, ambayo
ilifanyika mjini Cape Town mahali ambako Mandela alitoa hotuba yake ya
kwanza baada ya kuachiwa huru kutoka jela. Chanzo: TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment