Msemaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Erick Komba
*******
Msemaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Erick Komba, alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo ambazo zilianza baada ya kumalizika kwa mechi ya soka kati ya timu ya JKT Maramba na Maramba City inayoundwa na wakazi wa kijiji hicho.
Komba alisema viongozi wa JKT kikosi cha Maramba wapo katika harakati za kutafuta chanzo cha vurugu hizo na kwamba hakuna athari iliyotokea wala wananchi kujeruhiwa katika mapambano hayo.
Hata hivyo, NIPASHE ambayo ilifika kijijini hapo ilipata taarifa kutoka kwa viongozi wa kata na kijiji kwamba wapo watu 15 waliojeruhiwa ambao baadhi yao wamelazwa katika Kituo cha Afya Maramba na wengine katika Hospitali ya Mkoa Bombo.
Uchunguzi wa gazeti hili kijijini hapo umebaini kuwa askari wa JKT waliamua kutembeza mkong’oto baada ya mmoja wa askari hao kudaiwa kuvunjwa mguu na lawama zikaelekezwa kwa wakazi wa kijiji hicho.
Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Edu Steven (31) ambaye amelazwa katika kituo cha afya kutokana na kupigwa, alisema vurugu hizo zilianza baada ya kumalizika kwa mechi ambayo matokeo yake yalikwenda sare ya kutofungana.
Steven alisema baadaye wakazi wa kijiji hicho walikwenda katika baa moja ijulikanayo kama Obama kwa ajili ya kucheza disko na ndipo askari wa JKT walipokwenda eneo hilo na kuanza kutembeza mkong’oto ovyo kwa kila aliyekuwapo hapo.
Mganga Mfawidhi wa kituo cha Afya Maramba, Dk. Shughusha Mwambo, alisema alipokea majeruhi 15 ambao baadhi yao walitibiwa na kuruhusiwa na wawili wamelazwa katika kituo hicho na mwingine Hospitali ya Bombo.
Watu waliojeruhiwa ni Asha Mdoe, Fatuma Kassimu, Hassan Salimu, Mwajuma Rashid, Edward Mtumbatu, Mohamed Salim, Peter Samweli, Eddo Jumanne, Zephania Makaranga, Muhudi Daudi, Yahaya Said, Juma Msagati, Hussein Mgaya na Hadija Richard.
Diwani wa Kata ya Maramba, Said Mjasambu, alisema alifika katika kituo cha afya saa 8:00 usiku na kukuta hali bado ni tete na askari hao walikuwa wakizingira kwenye eneo la kituo.
Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Mboni Mgaza, aliwaomba wananchi kuwa watulivu wakati suala hilo linatafutiwa ufumbuzi na kuwaagiza polisi kuimarisha ulinzi katika kijiji hicho.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment