Adai ndio chanzo cha kupigana bungeni Asema ndizo walizotumia kuzunguka na helkopta nchini. Aeleza yaliyotokea bungeni sio bahati mbaya, Chadema waliyapanga Ashukuru bunge kuendelea kuonyeshwa"live" ili wananchi waone ujinga wao.
Awatuhumu kuweka masilahi yao mbele badala ya nchi. Asisitiza CCM kuendelea kuheshimu uamuzi wa wananchi juu ya katiba. Aonyesha madai ya Chadema kitakwimu yasivyojali wakulima na wafanyakazi.
Katibu wa NEC ya CCM itikadi na Uenezi
amesema kinachowasumbua Chadema mpaka wanafanya yote waliyoyafanya hasa
ngumi na vurugu bungeni ni namna watakavyoeleza kwa waliowapa pesa za
kuvuruga mchakato wa katiba nchini kwani wanatakiwa kupeleka mrejesho
jinsi walivyofanikiwa na jinsi walivyotumia mabilioni hayo.
Nape ameyasema hayo kwenye mkutano
mkubwa wa hadhara mjini Kahama kwenye ziara ya karibu siku ishirini
kanda ya ziwa kwa mikoa mitatu yaani Shinyanga,Simiyu na Mara ya Katibu
Mkuu wa CCM Taifa Ndg. Abralhaman Kinana.
"Wenzetu hawa nasikia wamepewa
mabilioni toka nje kwa kisingizio cha kushiriki mchakato wa katiba, na
kama ilivyo kwa vibaraka wengine katika bara la Afrika lengo la mapesa
hayo sio kuwawezesha kushiriki bali kuanzisha fujo na vurugu ili
mchakato usimalizike salama iwe ajenda 2015 kwani kimsingi hawana ajenda
mpya" alisisitiza Nape.
Akielezea swala la pesa kutoka nje
Nape alisema mara tu baada ya rasimu ya kwanza kutoka Katibu Mkuu wa
Chadema alikwenda nje ya nchi na akakaa kwa muda na aliporudi tu, ndio
Chadema wakapanga kuanza kuzunguka na helkopta.
"Babu atwambie alifuata nini nje? Na
pesa za kuzunguka na misafara miwili tofauti ya helkopta walitoa wapi?
Na watwambie kama walisharudisha mrejesho kwa wafadhili wao" alisema
Nape
Nape aliendelea kusisitiza kuwa yote
yaliyotokea bungeni si mambo yaliyotokea kwa bahati mbaya isipokuwa ni
mambo yaliyopangwa na Chadema katika mkakati wa kutimiza moja ya malengo
yao.Alisema ilikua ni lazima watafute mahali pa kufanya kituko bungeni
ili iwe mjadala na ili wapate sababu na picha za kuonyesha kwa waliowapa
pesa kuwa wanapambana.
"hili walilofanya Chadema bungeni ni
jambo walilopanga katika mkakati wao wa 'civil disobidiency'
...machafuko ya umma dhidi ya dola, mkakati ambao unaratibiwa kutoka nje
na baadhi ya wale waliokuwa wakoloni katika nchi zetu za Afrika. Lengo
ni kusababisha machafuko na nchi kutotawalika" alisema Nape.
Nape alisema ndio maana CCM
ilisisitiza lazima bunge liendelee kuonyeshwa na televisheni ili
kuonyesha yanayoendelea bungeni kuwawezesha wananchi kuona kinachofanywa
na wawakilishi wao.
"bila shaka wananchi mmeona
kilichotokea bungeni kwa macho yenu, sina haja ya kuwaeleza. Mmeona
wabunge wa upinzani walichofanya,uchaguzi ujao tupunguze idadi ya vichaa
bungeni ili kodi zetu zitumike vizuri,kwani tuliwatuma wakajadili
maendeleo yetu wao wamegeuza bunge uwanja wa masumbwi.
Aidha Nape akifafanua hoja ya upinzani
bungeni juu ya idadi ya wabunge wa bunge maalum la katiba alisema
upinzani hawana hoja ya msingi bali wanasukumwa na ubinafsi na ulafi wa
madaraka.
"Hoja iliyowafanya wapigane bungeni
haina mashiko, wanataka idadi iongezwe ya wabunge wa bunge la katiba
kutoka 357 mpaka 792. Hivi nani anabeba mzigo huu wa kuwalipa hawa
wabunge kama sio mwananchi wa kawaida? Halafu mnajiita watetezi wa
wanyonge? Hamuoni aibu?" alihoji Nape.
Akiendelea kufafanua Nape anasema,
" katika hali ya kawaida tungetegemea
wajenge hoja ya kundi kubwa katika jamii ya kitanzania ambao ni wakulima
na wafanyakazi ndio wawe na uwakilishi mkubwa kwenye hilo bunge kama
tunataka katiba kweli ya wananchi lakini badala yake wao wanapendekeza
wawakilishi kutoka vyama vya siasa ukiacha wabunge waliopo sasa wawe 72
na wakulima wawe 10 tu! Wanataka katiba ya vyama vya siasa badala ya
katiba ya nchi kwa ajili ya wananchi. Wanataka wafugaji wawe 10 tu na
wafanyakazi 40.
Kwa uwiano wa kawaida asilimia 80% wa wananchi wa nchi
hii ni wakulima, tungetegemea wangependekeza idadi yao kuwa kubwa lakini
wao wanawapuuza wakulima na wafugaji kwa kudai wawe kumi tu"!
Nape alimalizia kwa kudai kuwa siku za vyama kama Chadema zinahesabika maana hii ya katiba ndio ilikuwa karata yao ya mwisho.
" Nimalizie kwa kuwatahadharisha
vijivyama hivi vingine kama CUF, NCCR mageuzi na wengine kuwa wenzao
wamepewa mapesa wao wanwaunga mkono kwa ajenda iliyojificha. Na kwakuwa
hili la kuvuruga katiba ndio karata yao ya mwisho basi tutarajie anguko
baya sana kwa Chadema na huo ndio utakuwa mwisho wao"!alimalizia Nape.
No comments:
Post a Comment